Mahakama yabatilisha Profesa Kudoja kusimamia mirathi ya dada yake

Muktasari:
- Profesa Kudoja aliteuliwa na Mahakama Kuu kuwa msimamizi wa mirathi ya dada yake, lakini Mahakama ya Rufani imebatilisha uteuzi huo.
Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imebatilisha na kutengua uteuzi wa Profesa William Kudoja katika usimamizi wa mirathi ya marehemu dada yake, Salome Canisius Mbussa, aliyefariki miaka 13 iliyopita, baada ya kubaini alipata utezi huo kwa njia isiyo halali.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo katika hukumu yake iliyotolewa Juni 5, 2024 na majaji watatu – Winfrida Korosso, Ignas Kitusi na Amour Khamis, kufuatia rufaa aliyoikata mwakilishi na msimamizi wa mirathi ya marehemu Mbussa; Julius Peter Nkonyi.
Profesa Kudoja aliteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi hiyo na Mahakama Kuu Dar es Salaam, katika hukumu iliyotolewa na Jaji Edson Mkasimongwa, Desemba 15, 2015, kufuatia shauri la mirathi namba 09/2012, alilolifungua Profesa Kudoja, baada ya kutupilia mbali pingamizi la mume wa marehemu.
Hata hivyo, Nkonyi hakukubaliana na uamuzi huo, hivyo alikata rufaa Mahakama ya Rufani kuipinga hukumu hiyo, na Mahakama ya Rufani imekubaliana na rufaa hiyo na kutengua uteuzi wa Profesa Kudoja.
Katika hukumu hiyo Mahakama ya Rufani imesema kwa mujibu wa kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi Mirathi, mtu yeyote anayestahili anaweza kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi.
Imesema kuwa msimamizi huyo anaweza kuwa miongoni mwa warithi, ndugu wa karibu wa marehemu au mtu mwingine yeyote itakayeona anafaa kutekeleza wajibu huo, kwa masilahi warithi wa marehemu.
Hata hivyo, imebainisha kuwa, mahakama inaweza kubatilisha uteuzi wa msimamizi wa mirathi kutokana na sababu kadhaa, miongoni mwazo ni pamoja na mwombaji kuficha taarifa muhimu zinazohusika na kesi.
“Katika kesi hii mjibu rufani (Profesa Kudoja) aliificha mahakama ya awali ukweli kwamba marehemu Salome Mbussa alikuwa ameolewa na Canisius Ng’wandu Mbussa na alimuacha hai mumewe huyo,” imesema mahakama hiyo.
Mahakama hiyo imesema kuwa imechunguza kumbukumbuku za mahakama na kubaini kuwa haimtaji kabisa mume wa marehemu (Mbussa), isipokuwa baba yake Michael Theodor Makoba, dada zake wawili, Noela Wenceslaus Bategeki na Agusta Sule Mfuko pamoja na kaka yake, Profesa Kudoja.
“Mbaya zaidi, jaji aliyesikiliza shauri la msingi aliweka msisitizo kwa baba huyo (wa marehemu), dada na kaka wa marehemu kama watu wenye masilahi makubwa katika mirathi ya marehemu na kumweka mumewe katika daraja la chini, katika kundi la kadhalika (wengineo)”, imesema mahakama.
Pia Mahakama ya Rufani imesema imebaini kuwa mwombaji Profesa Kudoja alitoa madai ya uongo Mahakama Kuu kwamba nyumba iliyoko katika kitalu namba 88, Barabara ya Guinea, Bloku MS-OY 543, Oysterbay, Dar es Salaam ilikuwa inamilikiwa na marehemu Salome pekee.
Mahakama hiyo imesema kuwa madai hayo yalikuwa yanakinzana na ushahidi kwenye kumbukumbu ambao ulithibitisha kwa uzito kuwa nyumba hiyo ilinunuliwa na wenza hao wakati wa uhai wa ndoa yao.
Mahakama hiyo imebainisha kuwa kwa mujibu wa ushahidi huo baada ya kununua nyumba hiyo kwenye mnada uliondeshwa na dalali wa mahakama waliifanya makazi ya wanandoa.
Kutokana na sababu hizo na kwa kuzingatia ugomvi na kutokuelewana baina ya Profesa Kudoja na marehemu, mahakama hiyo imesema kuwa haiwezekani Profesa Kudoja kuendelea na usimamizi wa mirathi ya marehemu bila kuathiri masilahi ya mume wa marehemu.
Badala yake imesema kuwa ni muhimu kumteua mtu asiye na upande ili kuepuka uwezekano wa upendeleo ambao upande wowote unaweza kulalamikiwa na kwamba inashawishika kuwa Kabidhi Wasihi Mkuu yuko katika nafasi nzuri kusimamia mirathi hiyo.
Hata hivyo mahakama hiyo imebainisha kuwa jukumu hilo liko kwa Mahakama Kuu, kwa mujibu wa Sheria ya (PAEA) na chini ya kifungu cha 5 (1) (e) na 52 vya Sheria ya Kabidhi Wasii Mkuu (Mamlaka na Shughuli), Sura ya 27 kama ilivyorejewa mwaka 2019.
“Kwa hiyo tunatengua na kutupilia mbali hukumu ya Mahakama Kuu (iliyomteua Profesa Kudoja),” imesema Mahakama ya Rufani na kuhitimisha:
“Na tunarejesha kumbukumbu kwa Mahakama Kuu kuendelea na uteuzi wa msimamizi wa mirathi ya marehemu Salome Mbussa kwa mujibu wa sheria.”
Kuibuka kwa mvutano wa mirathi
Kwa mujibu wa kumbukumbu za mahakama Salome ambaye alikuwa mtumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) alifunga ndoa na Canisius Ng’wandu Mbussa, lakini hawakubahatika kuzaa mtoto hata mmoja wakati wa uhai wao katika ndoa yao.
Salome alifariki dunia Desemba 8, 2011 na akamuacha mumewe Mbussa pamoja na mali walizochuma pamoja kama wanandoa ikiwemo nyumba iliyoko Oysterbay walimokuwa wanaishi.
Muhtasari wa kikao cha familia kilichomhusisha mwenyekiti wa Mtaa wa Oysterbay, ndugu wa mzee Mbussa na ndugu wa marehemu Salome cha Desemba 13, 2011 ulimtambua Mbussa kuwa mume halali wa marehemu (Salome) na kwamba mali zote zilimilikiwa kwa pamoja.
Hata hivyo, mwaka 2012 Profesa Kudoja ambaye ni kaka wa marehemu Salome alifungua shauri la mirathi akiomba kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi ya dada yake akidai aliteuliwa na kikao cha ukoo wa marehemu Februari 5, 2012, ambacho hakikumhusisha Mbussa.
Hivyo, Mbussa aliweka pingamizi akipinga hatua hiyo iliyofanywa na shemeji yake bila kumshirikisha, akidai
Yeye alikuwa mume halali wa marehemu Salome, huku aliambatanisha na cheti ndoa kwa uthibitisho.
Pia alidai kuwa shemeji yake huyo, alikuwa amemwondoa katika nyumba yao ya Oysterbay na kumsababisha kukamatwa na kuwekwa katika mahabusu ya Polisi kwa tuhuma za jinai zisizo za kweli.
Vilevile alitoa nyaraka kuonyesha kuwa mali zilizokuwa zimeorodheshwa kwenye shauri hilo na Profesa Kudoja zilinunuliwa kwa pamoja yeye na mkewe wakati wa ndoa yao.
Hata hivyo, wakati wa mwenendo wa pingamizi hilo mzee Mbussa naye alifariki dunia na Nkonya akateuliwa na kushika nafasi yake, kama msimamizi wa mirathi ya marehemu Mbussa.
Wakati wa usikilizwaji wa shauri la msingi la mirathi, Profesa alidai wakati Salome anafariki walikuwa wametengana na mumewe kwa takribani miaka miwili.
Alidai kuwa marehemu aliwaacha hai baba yake Michael Theodor Makoba, dada zake wawili, Noela Wenceslaus Bategeki, Agusta Sule Mfuko na yeye kaka yake, yaani yeye mwenyewe.
Pia alitaja mali alizoziacha marehemu kuwa ni magari matatu, mafao kutoka BoT alikokuwa akifanya kazi, pesa katika akaunti tatu za benki, samani, ardhi na nyumba moja kitulu namba 88, Barabara ya Guinea, Oysterbay Dar es Salaam, alizodai kuwa zilikuwa zinamilkiwa na marehemu pekee.
Hata hivyo, Julius kwa upande wake aliieleza mahakama kuwa marehemu Salome na Mbussa waliishi katika nyumba moja waliyoimiliki pamoja kama wanandoa ya Oysterbay mpaka mauti yalipowatenganisha.
Alieleza kuwa wanandoa hao hawakuwahi kutalikiana wala kutengana na walimiliki mali hizo kwa pamoja na kwamba mzee Mbussa alishindwa kushiriki katika mazishi ya mkewe Salome yaliyofanyika Nzega, mkoani Tabora kwa kuwa alikuwa mgonjwa.
Julius alidai kuwa orodha ya mali ziliorodheshwa katika mirathi zilimilikiwa kwa pamoja na wenza hao – Salome na Mbussa.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake ilikubaliana na maelezo ya Profesa Kudoja ikatupilia mbali pingamizi la mume wa marehemu, kisha ikamteua Profesa Kudoja kuwa msimamizi wa mirathi hiyo, ndipo Julius akakata rufaa Mahakama ya Rufani.
Katika rufaa hiyo mrufani Nkonya aliwakilishwa na Wakili Dk Aloyce Rugazia, huku mjibu rufaa, Profesa Kudoja akiwakilishwa na wakili Daibu Kambo, nadi huku ilipotenguliwa.