Mahakama yagoma kuwafutia mashtaka ya utakatishaji fedha

Sehemu ya vipande vya meno ya tembo vilivyokamatwa mkoani Mbeya.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imetupilia mbali pingamizi la kufuta mashtaka matatu ya utakatishaji fedha yaliyowasilisha na upande wa utetezi katika kesi ya kusafirisha vipande 413 vya meno ya tembo, inayomkabili mshtakiwa Hassan Likwena na wenzake watano.

Likwena na wenzake wanakabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu kwa kuuza, kukusanya, kununua na kusafirisha nyara za Serikali ambazo ni meno 413 ya tembo na meno mawili ya viboko yenye thamani ya Sh4.4 bilioni, mali ya Serikali.

Mbali na Likwena, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 70/2022 ni Oliver Mchuwa, Haidary Sharifu, Joyce Thomas, Abdul Abdallah na Salama Mshamu.

Uamuzi huo wa kutupilia mbali pingamizi hilo, umetolewa leo Jumatatu Aprili 15, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Aaron Lyamuya, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi mdogo na kisha kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka.

Katika uamuzi wake, Hakimu Lyamuya amesema anawaachia upande wa mashtaka kufanya upelelezi wa kujua iwapo mshtakiwa Likwena na Abdallah walihusika katika utakatishaji fedha ua laa.

“Nawachia upande wa mashtaka walete udhibitisho mahakamani hapa, iwapo mnahusika katika kutakatisha fedha ua laa,” amesema Hakimu Lyamuya na kuongeza:

“Kwa sasa, hamtatolewa mashtaka yenu ya utakatishaji fedha mnayotuhumiwa nayo, mpaka upande wa mashtaka watakapoleta udhibitisho mahakamani hapa, kwa sababu baadhi yenu walikutwa na mali ikiwemo magari ambayo yamepatikana kwa njia haramu.”

Machi 2024, wakili wa washtakiwa hao, Nehemia Nkoko, aliwasilisha pingamizi mahakamani hapo akitaka mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo (Likwena) na mshtakiwa wa tano (Abdallah) waondolewe mashtaka matatu ya utakatishaji fedha yanayowakabili, kwa madai kuwa hakuna ushahidi unaonyesha kuwa nyara hizo za Serikali ziliuzwa.

Kutokana na pingamizi hilo, Mahakama hiyo iliahirisha kesi hiyo na kupanga kutoa uamuzi wake leo Jumatatu.

Hata hivyo, baada ya kutolewa uamuzi huo, kesi hiyo imeshindwa kuendelea na usikilizwaji wa upande wa mashtaka kutokana wakili wa washtakiwa hao, Nehemia Nkoko kuwa na udhuru na kushindwa kufika mahakamani.

Kutokana na hali hiyo, wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga akishirikiana na Frank Rimoy, wameomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Hakimu Lyamuya ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 29, 2024 itakapoendelea kusikilizwa na washtakiwa watano wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria, huku mshtakiwa Sharifu akiwa nje kwa dhamana.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Agosti 28, 2019 na Agosti 30, 2019 jijini Dar es Salaam, ambapo walijihusisha na genge la uhalifu kwa kuuza, kukusanya, kununua na kusafirisha meno 413 ya tembo na meno mawili ya viboko yote vikiwa na thamani ya Sh4.4 bilioni.