Mahakama yakataa kupokea video kesi ya mke wa Bilionea Msuya

Mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita

Muktasari:

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeikataa video ya maelezo ya mshtakiwa Miriam Mrita, mke wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini Mirerani mkoani Arusha, Erasto Msuya maarufu kama Bilionea Msuya kutokana na kukiuka matakwa ya kisheria ya kuwasilisha mahakamani hapo

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeikataa video ya maelezo ya mshtakiwa Miriam Mrita, mke wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini Mirerani mkoani Arusha, Erasto Msuya maarufu kama Bilionea Msuya kutokana na kukiuka matakwa ya kisheria ya kuwasilisha mahakamani hapo.


Umauzi huo umetolewa leo Jumatano Machi 9, 2022 na Jaji Edwin Kakolaki anayeisikiliza kesi hiyo, baada ya kukubalina na hoja moja kati ya tano za pingamizi zilizoibuliwa na wakili wa mshtakiwa huyo, Peter Kibatala kuwa kielelezo hicho kilichokuwa kinaombwa kupokelewa mahakamani hapo hakikuwahi kuorodheshwa wala kusomwa katika hatia ya uhamishaji wa kesi hiyo kutoka Mahakama ya chini kwenda Mahakama Kuu, kama sheria inavyoelekeza.


Upande wa mashtaka katika kesi hiyo kupitia kwa shahidi wa sita, Mkaguzi wa Polisi (Inspekta), Alistides Kasigwa, kutoka Makao Makuu ya Jeshi ya Polisi, Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi, alieleza mahakama kuwa alimrekodi mshtakiwa huyo wakati akitoa maelezo yake akihojiwa na askari Inspekta Ratifa katika kituo kidogo cha Pilisi Uwanja wa Ndege, Dar es Salaam, Agosti 8, 2016.


Mbali na Miriam ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo namba 103 ya mwaka 2018, mshakiwa mwingine ni mfanyabiashara Revocatus Myella.


Wote wanakabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia, wakidaiwa kumuua, mdogo wa marehemu Bilionea Msuya wa kike, Aneth Msuya nyumbani kwake, Kibada, Kigamboni jijjini Dar es Salaam, Mei 25, 2016.


Soma hapa uamuzi ulivyotolewa

Jaji Edwin Kakolaki: Jana upande wa mashtaka kupitia kwa shahidi wake wa sita Mkaguzi wa Polisi (Inspekta), Alistides Kasigwa kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi, uliomba kuwasilisha mahakamani mkanda (tape) ndogo ya video (Min DV) inayodaiwa kurekodiwa na shshidi huyo wakati mshtakiwa wa kwanza Miriam Mrita akitoa Maelezo yake mbele ya Askari Inspekta Ratifa,

Maelezo hayo yanadaiwa kuwa yalichukuliwa Agosti 8, 2016 matika kituo cha Polisi Uwanja wa Ndege Dar es Salaam.

Lakini upande wa utetezi wakili Peter Kibatala alipinga kuwa matakwa ya kisheria hayakuzingatiwa, akitoa sababu tano

1: Nyaraka hiyo inayokusudiwa kutelewa hakipaswi kwa kuwa kilikiuka masharti ya kifungu cha 18 cha Sheria ya Miamala ya Kielektroniki.

Kwamba haikueleza taratibu za uchukuaji wa video hiyo, kwamba ilitunzwaje lakini hawakueleza hayo.


2: Kwamba shahidi huyo hakuwa na mamlaka kutoa kielelezo hicho kwani kwa mujibu wa kifungu Cha 9 Cha Sheria ya Huduma za Mashtaka alikuwa akifanya kazi chini ya usimamizi wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

3: Kwamba kiutaratibu na kwa msingi wa kisheria katika mashauri mbalimbali, katika kutoa nyaraka au ushahidi wa kielektroniki ni lazima kwanza kuleta uthibitisho mahakamani kwa hati ya kiapo au maelezo kuthibitisha uhalisia wa kielelezo hicho lakini hakuna hati iliyoletwa wakati washtakiwa wanasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo au hata sasa, kinyume Cha kifungu Cha 246 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA)

4: Kwamba nyaraka hiyo haikuwahi kuorodheshwa wala kusomwa wakati washtakiwa waliposomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo, kinyume cha Kifungu Cha 246 (CPA)

Kwamba upande wa mashtaka wangweza kutumia kifungu Cha 289 CPA kuomba kuwasilisha ushahidi wa nyongeza lakini hawakufanya hivyo.

5: Kwamba kielelezo hicho hakina uhusiano na shauri kwani kimepatikana kwa utaratibu usio sahihi.

Hoja za Kibatala ziliungwa mkono na wakili wa mshtakiwa wa pili, Revocatus Myella; Wakili Nehemia Nkoko, akiongeza kwamba shahidi huyo hakuweza hata kutaja vifaa alivyotumia kuchukua picha hizo na alivyotumia kuzitunzia.


Majibu ya Serikali


Wakili wa Serikali Mwandamizi, Genes Tesha alidai kuwa hoja zote za pingamizi hazina mashiko kwa kuwa shahidi alichukua kielelezo hicho chini ya kifungu cha 40A ambacho hakina hitaji la hayo yaliyoelezwa na mawakili wa utetezi.

Kwamba shahisi alikuwa chini ya usimamizi wa DPP, wakili Tesha alidai kuwa si sahihi kwani alifanya kazi hiyo chini ha kifungu Cha 59 CPA, hivyo alikuwa chini ya usimamizi wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI.

Kuhusu hoja ya kuwasilisha uthibitisho wa uhalali wa kielelezo hicho alidai kuwa takwa hilo halipo katika mashauri ya Jinai bali katika mashauri ya madai na kwamba kuwa yeye shahid ni gazette officer ( ametangazwa kwenye gazeti la Serikalj) hivyo halazimiki kuwasilisha uthibitisho.


Kielelezo kutosomwa awali, wakili Tesha alidai kuwa katika maelezo ya shahidi yalibainisha kuwa kielelezo hicho kingetolewa na kwamba hata wakati wa usikilizwaji wa awali (PH), walieleza kuwa wangewasilisha vielelezo halisia.

Pia wakili Tesha alidai kuwa shahidi alieleza katika ushahidi wake wa msingi jinai alivyofanya kuchukua kielelezo hicho na hata namna alivyovitunza.

Hivyo alidai kuwa nyaraka hiyo inastahili kupokewa na akaiomba mahakama ione kwamba mapingamizi yaliyowasilishwa hayana mashiko.


Wakili Kibatala alisisitiza hoja zake za awali kuwa kielelezo kufungwa tu mwa lakiri kama shahidi alivyoeleza haitoshi bila kueleza mazingira yote ya upatikaji na mtiririko wa utunzaji wake.


Alisisitiza kuwa kielelezo hicho hakikusomwa mahakama ya chini na kwamba hati ya uthibitisho inatumika kwa mashauri yote.

Aliongeza kuwa hata Kama kilelelezo hicho kilichukuluwa chini ya kifungu cha 57 bado masharti yake hayakuzingatiwa kwani mshtakiwa hakupewa nakala yake kama kinavyoelekeza.

Kuhusu matumizi ya kifungu Cha 40A, wakili Kibatala alidai kuwa hutumika pale tu Polisi wanapofanya kazi yao katika mazingira yasiyo ya wazi.

Kutokana na hoja hizo mahakama iliona kuna hoja kama kielelezo hicho kinastahili kutolewa.

Mahakama iluamua kuangalia kwanza hoja ya nne, kwamba katika Mahakama ya chini wakati shauri hilo likifanyiwa maandalizi kuletwa Mahakama Kuu nyagraka hiyo haikuorodheshwa kama moja ya vielelezo na wala haikusomwa ili mshtakiwa aweze kujua kilichomo.


Hoja ilipingwa vikali na wakili Tesha akidai kuwa katika ukrasa wa 43 wa mwenendo wa shauri hilo ilitajwa kwenye maelezo ya shahidi na kwamba pia katika hatua yabusikilizwaji wa awalj walieleza kuwa watakiwasilisha.

Ni takwa la kisheria chini ya kifungu cha 246 CPA kwamba kielelezo au nyaraka yoyote inayokusudiwa kutolewa kama kielelezo na upande wa mashtaka ni lazima iorodheshwe na isomwe kwenye committal ( uhamishaji shauri toka mahakama ya chini kwenda Mahakama Kuu) na kutokufanya hicho kunaweza kusababisha kielelezo hicho kisipokewe.

Kifungu hicho kinataka maelezo ya mashahidi au kielelezo viwekwe wazi na kusomwa.


Mahakama hii imejiuliza kama hiyo original tape ni kielelezo.


Kifungu cha 3 cha Sheria ya Ushahidi kinaeleza kuwa nyaraka yoyote inayotunzwa kwenye kompyuta katika mfumo wa kielektroniki inaweza kusomwa au kutunzika kwa matumizi ya baadaye hiyo inachukuliwa kuwa ni nyaraka.

Kwa maana nyingine kitu hicho kinachobishaniwa kikiwa katika vigezo hivyo, hiyo ni nyaraka.

Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake iliwahi kusema kuwa hata flash disk na simu licha ya kwamba zinaonekana kwa misingi wa ushahidi wa kielektroniki ni nyaraka kwani vinaweza kutunza vitu ambavyo vinaweza kusomeka.


Hivyo hata hiyo min video tape nayo ni nyaraka kama nyaraka nyingine.


Swali sasa ni kwamba nyaraka hiyo ilipaswa kuorodheshwa na kusomwa kwenye committal.

Nakubaliana na wakili Tesha kuwa maelezo ya shahidi yalisomwa kule mahakama ya chini yalijumuisha nyaraka hiyo. Lakini hata hii pia kwa kuwa ilikuwa ni nyaraka nayo ilipaswa kuorodheshwa na kusomwa.

Sharti hilo ni la lazima ili kumpa mshtakiwa haki ya mazingira ya usawa kusikiliza shauri lake na kutompa mazingira ya kushtukizwa.


Mshtakiwa anapaswa kujua undani wa ushahidi dhidi yake ili kuweza kuandaa utetezi wake kwa usahihi.


Mahakama ya Rufani katika mazingira haya ilisema kutoorodhesha kielelezo na kukisoma kunaondoa mazingira ya usikilizwaji wa haki.


Hivyo mahakama hiyo iliona kuwa nyaraka zilizokuwa zinabishaniwa hazikuwahi kuorodheshwa achilia mbali kusomwa na ikasisistiza kuwa umuhimu wa kufanya hivyo ni kumpa mshtakiwa maandalizi ya utetezi wake.


Mahakama haikubaliani na hoja ya wakili Tesha kuwa nyaraka hiyo ni kielelezo halisi kwa sababu huu ni ushahidi wa kielektroniki, na siyo physical exhibit. Physical exhibt inaweza kuwa labda mapanga.


Mahakama hii katika kufuatilia iliona kwamba kweli kuna kielelezo kilitajwa katika maelezo ya shahidi na iliyotajwa ni CD video record sasa mahakama inajiuliza hiyo CD Video record ndio hii original DV tape? CD Video record inaweza kutayarishwa kutokana na min DV original.


Mahakama hii imepatwa tashwishwi kujua ni hati gani kati ya hizo mbili ambayo ilisomwa.


Hivyo Mahakama katika shauri hili haijawekwa wazi kuwa CD video tape inamaanisha min DV tape, inapata wakati mgumu kuamini kwamba kielelezo hiki kikisomwa wakati wa usikilizwaji wa awali.


Katika mazingira hayo kwa kuwa kielelezo hicho hakikusomwa hata wakati wa usikilizwaji wa awali kulikuwa na ukiukwaji wa kifungu cha 246 CPA basi kurubusu kielelezo hiki itakuwa na madhara kwa mshtakiwa kwa kuwa itamnyima haki ya maandaliI ya utetezi wake kwa kuzingatia shauri linalomkabili ni serious na kama akipatikana na hatia adhabu yake ni adhabu ya kifo.


Baada ya kukubaliana na hoja hii Mahakama inaona kuwa inatosha inaweza kumaliza ugomvi huu wa kupokea kielelezo hiki, hivyo hakuna sababu ya kuangalia hoja nyingine.


Kwa hiyo mahakama hii imeona kwamba kielelezo kilichorekodiwa tarehe 8/8/2016 hakiwezi kupokewa kwa kuwa kimekiuka mashariti ya kifungu Cha 246 Cha CPA.


Mwisho wa uamuzi


Sasa shahidi wa sita Inspekta Alistides anaendelea na ushahidi wake akiongozwa na wakili wa Serikali Mwandamizi, Tesha.

Shahidi: Baada ya kurekodi nilizalisha CD mbili nikaiseal min DV na vielelezo vilitunzwa.

Msawali

Kibatala: Shahidi wakati unatoa ushahidi wako ulisema tarehe 8/8/2016 katika kituo cha Polisi Airport ulimuona Askari Ratifa akiwa na mshtakiwa wa kwanza ni sahihi?


Shahidi: Ni sahihi


Kibatala: Shahidi tufafanulie jiografia, ni sahihi kwamba kituo cha Polisi Airport ni mbali kabisa na polisi Chang'ombe?


Shahidi: Ni sahihi


Wakili Nehemia Nkoko: Shahidi ni sahihi kwamba kituo cha Polisi Airport kiko Wilaya ya Ilala na Chang'ombe kiko Temeke?


Shahidi: Ni sahihi.


Tesha: Mheshimiwa upande wa Jamhuri hatuna re-examination.


Wazee wa Baraza


Wote: mmojammoja, sina swali Mheshimiwa.

Wakili Tesha: Mheshimiwa, kwa leo upande wa mashtaka hatuna shahidi mwingine, tunaomba tarehe nyingine ya kuendelea.


Kibatala: Mheshimiwa hatuna pingamizi la ahirisho ila tuna ombi dogo tu kwa mahakama kwamba itufanyie hisani kwa tarehe ya karibu kama nafasi ikipatikana sisi tuko tayari kuja kuendelea.


Wakili Nkoko: Mheshimiwa nami sina pingamizi


Jaji Kakolaki: Tunakusudia kuendelea kesho kama itawezekana.


Wakili wa Serikali Tesha: Mheshimiwa mimi ndio mwenye kesi na ndio najua mashahidi wangu nawapataje na kuwaandaa, kwa kesho hatutaweza sababu mashahidi wangu wanatoka mbali.


Kibatala: Mheshimiwa kuna shahidi mmoja ambaye yuko chini ya onyo na sijaona akiletwa nadhani ameamua mwenyewe tu kukaa nyumbani.


Tesha: Ni kweli alionywa lakini kwa sasa hayupo.


Jaji Kakolaki: Muda uliopangwa kwa mashauri haya unakwisha. Tulikuwa tunajaribu kuangalia muda unaoweza kupatikana kwa mashauri mengine ulikuwa ni kesho na keshokutwa.


Kwa kuwa Upande wa mashtaka hawako tayari kwa madai kwamba mashahidi wao wako mbali, tunaahirisha shauri hili hadi litakapopangwa tena.