Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MAHUBIRI: Toba siyo udhaifu, ujinga bali ni kujinyenyekeza kwa Mungu

Bwana Yesu asifiwe. Ni neema ya Mungu kukutana kwenye safu hii ya mahubiri kwa mara nyingine. Karibu katika mahubiri ya leo Jumapili ninaamini utapata kitu ambacho kitabadilisha maisha yako na kwenda hatua nyingine.

Ninaitwa Mchungaji na Nabii Martin Bushasho, karibu tujifunze. Somo letu limejikita kuhusu toba.

Toba ni hitaji la kila mwanadamu bila kujali cheo, mali, elimu au umaarufu wake. Mbele za Mungu, wote ni sawa na kila mmoja anapaswa kunyenyekea na kutubu anapokosea.

Katika kitabu cha 2 Mambo ya Nyakati 7:14, Biblia inasema: "Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso wangu, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao."

Maneno haya ya "watu wangu" yanawahusu wanadamu wote bila kujali umri, dini, kabila, kiwango cha elimu, mali au cheo. Kigezo cha kwanza cha toba ni ubinadamu wa mtu.

Sifa za ziada kama mali, madaraka, umaarufu au elimu hazimuondoi mtu katika asili yake ya kibinadamu. Pia kwa kuwa kila mwanadamu ana mapungufu, basi toba inapaswa kuwa sehemu ya maisha yake.

Mwanadamu anapogundua amekosea, njia ya kurekebisha kosa hilo ni kunyenyekea mbele za Mungu na kutubu kwa moyo wa kweli.

Katika kitabu cha Hesabu 14:18 imeandikwa: "Bwana si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa fadhili, akisamehe uovu na makosa."

Hii inaonyesha kwamba mbele za Mungu ukubwa wa kosa siyo kikwazo cha kupata msamaha. Mtu akitambua kosa lake, akalijutia na kutubu kwa dhati, Mungu yuko tayari kusamehe na kumpa nafasi mpya ya maisha.


Kiburi ni adui wa toba

Changamoto kubwa hujitokeza pale mwanadamu anapopata mali, cheo au umaarufu. Mara nyingi kiburi huanza kutawala moyo wake na kumfanya aione toba kama udhaifu au fedheha.

Watu wengi hushindwa kuomba msamaha au kutubu hadharani siyo kwa sababu hawajakosea, bali kwa sababu wanaogopa kupoteza heshima zao mbele za jamii. Hata hivyo, kiburi hicho ndicho kinaweza kumpeleka mtu katika maangamizi.

Bwana Yesu alisisitiza umuhimu wa kutengeneza mahusiano yaliyoharibika kupitia toba na msamaha. Katika Mathayo 5:23-24 alisema:"Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huko ukakumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako hapo mbele ya madhabahu, uende zako kwanza upatane na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako."

Maneno haya yanaonyesha kwamba Mungu anathamini sana upatanisho, toba na msamaha kuliko hata sadaka nyingi zinazotolewa bila moyo safi.

Kanuni hii haiwahusu watu wa kawaida pekee. Inawahusu viongozi wa serikali, viongozi wa dini, viongozi wa kisiasa, matajiri, maskini, wasomi na wasio wasomi. Mradi mtu ni mwanadamu, anawajibika kutubu anapokosea.


Somo kutoka Ninawi

Mfano mzuri wa nguvu ya toba unaonekana katika mji wa Ninawi. Mungu alimtuma Nabii Yona kwenda kuwaonya watu wa Ninawi kwamba kutokana na uovu wao, mji wao ungeangamizwa ndani ya siku 40. Waliposikia ujumbe huo, walichukua hatua ya haraka ya kutubu.

Yona 3:5-9 inasema: "Watu wa Ninawi walimuamini Mungu, wakatangaza saumu, wakavaa nguo za gunia, kuanzia mkubwa wao hata mdogo wao. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akainuka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajifunika gunia, akaketi majivuni."

Kutoka kwa mfalme hadi kwa mtumishi wa kawaida, wote walijinyenyekeza mbele za Mungu. Hakuna aliyedai kuwa cheo chake kilimzuia kutubu.

Matokeo yake yalikuwa makubwa. Mungu aliona unyenyekevu wao, akaondoa hukumu aliyokuwa amepanga kuwaletea.

Kisa hiki kinafundisha kwamba toba haiangalii hadhi ya mtu. Kinachotafutwa ni moyo wa unyenyekevu na uamuzi wa kuacha njia mbaya.


Mfano wa Mfalme Manase

Mfano mwingine muhimu ni wa Mfalme Manase, ambaye Biblia inamtaja kuwa mmoja wa wafalme waovu zaidi katika historia ya Israeli.

Miongoni mwa mambo aliyofanya ni: Aliiacha sheria ya Mungu na kujenga madhabahu za miungu ya uongo, alitoa watoto wake kuwa sadaka, alijihusisha na uchawi, uganga na uaguzi, alimwaga damu nyingi za watu wasio na hatia, alikataa maonyo ya Mungu kwa muda mrefu.

Hata hivyo, baada ya kukamatwa na Waashuru na kutiwa gerezani, Manase alijinyenyekeza na kutubu.

2 Mambo ya Nyakati 33:12-13 inasema: "Katika shida yake alimtafuta Bwana Mungu wake, akajinyenyekesha sana mbele ya Mungu wa baba zake. Naye alipomwomba, akasikilizwa, akarejeshwa Yerusalemu katika ufalme wake."

Baada ya kutubu kwa dhati, Mungu alimrejesha na kumbadilisha maisha yake. Hii inaonyesha kwamba hakuna mtu aliyefika mbali sana kiasi kwamba hawezi kusamehewa na Mungu akitubu kwa kweli.


Mungu anataka unyenyekevu

Katika Mika 6:8 imeandikwa: "Ee mwanadamu, amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu pamoja na Mungu wako?"

Haya ndiyo maisha ambayo Mungu anayatamani kwa kila mwanadamu. Maisha ya haki, rehema na unyenyekevu.

Toba siyo ishara ya udhaifu wala ujinga. Ni ishara ya hekima, ukomavu na heshima kwa Mungu.

Ni muhimu kutambua kwamba toba ndiyo msingi wa kurejesha amani ya kweli katika maisha ya mtu binafsi na katika taifa kwa ujumla.

Hakuna mtu anayepoteza heshima kwa kuomba msamaha au kutubu. Kinyume chake, mtu anayekubali makosa yake na kuyarekebisha hujenga heshima zaidi mbele za Mungu na mbele za wanadamu.

Tujifunze kutoka kwa watu wa Ninawi na Mfalme Manase kwamba mbele za Mungu hakuna mkubwa wala mdogo, mwenye cheo wala asiye na cheo. Wote tunahitaji toba, na wote tunaweza kupata msamaha tukitubu kwa moyo wa kweli. Mungu aliyehai akubariki na kukupa neema ya kufanya toba ili uweze kuwa na ushirika naye kila wakati.


Mchungaji Martin Bashando anapatikana Kanisa la Calvary Assemblies of God Tanzania, tawi la Chamazi. Kwa maombi na ushauri 0757 964805.