Majaliwa afungua Kongamano la Kimataifa la Nishati

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amefungua Kongamano la tano la Nishati, ambalo limekutanisha kampuni za mafuta, gesi na nishati jadidifu, watalaamu, wabunifu, asasi za kiraia wa ndani na nje. Kongamano hilo linatafuta mawazo, kuibua fursa na uzoefu wa kuendeleza nishati rafiki kwa mazingira.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekaribisha kampuni za kimataifa kuja kuwekeza nchini katika sekta ya nishati.

 Amesema Tanzania ina sera nzuri, mazingira rafiki ya kibiashara. Amesema jukumu kubwa la sera ya nishati inajikita kuongeza ufanisi wa huduma pamoja na ushirikishaji wa sekta binafsi.

“Nishati ni muhimu na nguzo katika kukuza shughuli za kiuchumi na kijamii kwa taifa lolote. Tanzania itaendelea kuhakikishia mazingira rafiki ya kibiashara na uwekezaji nchini,” amesema Majaliwa.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Septemba 20, 2023 wakati akifungua Kongamano la tano la Kimataifa kuhusu Nishati. “Niwahakikishie tunatoa mazingira rafiki ya kiuwekezaji kupitia sera rafiki za uwekezaji, Blue Print imeweka mazingira yanayorahisisha huduma rafiki kwa wawekzaji,” amesema.

Kwa mwaka huu kongamano hilo lililokutanisha maelfu ya watalaamu wa nishati, kampuni za mafuta, nishati, gesi, nishati jadidifu na taasisi za umma litaendesha mijadala mbalimbali kutafuta mbinu na mtazamo ya uwekezaji wa nishati jadidifu pamoja na nishati safi ya kupikia.

Mratibu wa kongamano hilo, Abdulsamad Abdulrahim  amesema tangu mwaka 2017, kongamano hilo limefanikisha uzalishaji wa ajira zaidi ya 2,000 moja kwa moja na ajira zisizo za moja kwa moja, mahudhurio ya rekodi ya 5,000, ushiriki wa mataifa 25 zilizokuwa na kampuni za mafuta 20.