Majaliwa aitangazia neema sekta binafsi, GGML…

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa tuzo kwa waajiri zilizoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na kuahidi ushirikiano.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana kikamilifu na sekta binafsi katika utoaji elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kutosha unaohitajika katika sekta mbalimbali.

Majaliwa alisema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam katika hafla ya utoaji wa tuzo kwa waajiri zilizoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).

Katika tuzo hizo, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) ambayo imekuwa na jitihada za kuwajengea uwezo wahitimu wa vyuo vikuu kwa kuwapatia mafunzo kazini ziliiwezesha kampuni hiyo kuibuka mshindi wa pili.

GGML ilibeba tuzo hiyo katika kundi la waajiri wakubwa kutokana na mchango wake wa uzalishaji wa rasilimaliwatu wenye ubora kwa soko la ajira.

Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya kampuni hiyo kupokea wahitimu 50 kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini ambao wameanza kupatiwa mafunzo kazini mwaka huu.

Kati yao 30 ni wanawake na 20 wanaume. Mwaka jana jumla ya vijana 26 walihitimu mafunzi hayo ndani ya GGML.

Majaliwa aliwapongeza waajiri kwa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo, uanagenzi, utarajali pamoja na namna wanavyoshiriki katika kuandaa mitaala inayotumika kwenye vyuo na taasisi za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

Waziri mkuu alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa waajiri wote nchini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha malengo ya kukuza ujuzi na kuongeza soko la ajira yanafanikiwa kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa.

“Maendeleo ya uchumi wa nchi yoyote yanategemea sana ngazi ya ujuzi wa nguvukazi uliyokuwa nayo. Hivyo, mchango wa wadau ni muhimu,” alisema.

Alisema ushirikiano huo ni muhimu katika kuendeleza ujuzi kwa ajili ya kujenga uchumi wa viwanda.

 “Nataka nitumie fursa hii kuwapongeza lakini Serikali inatambua na inathamini juhudi mnazozifanya katika utoaji wa ajira kwa wahitimu wetu, tunawapongeza sana," alisema

Akizungumzia kuhusu kauli mbiu ya mwaka huu inayosema “Kuimarisha Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa Uzalishaji wa Wafanyakazi Wenye Ujuzi Nchini Tanzania”, Waziri Mkuu alisema kauli hiyo ni thabiti kwani inaweka msisitizo katika ujenzi wa rasilimali watu yenye ujuzi.

Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi (Rasilimaliwatu) kutoka GGML, Charles Masubi aliishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo katika uzalishaji wa vijana bora wanaokubalika katika soko la ajira.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda alisema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Makakati wa Taifa wa Uendelezaji wa Ujuzi wa Mwaka 2016/17-2025/26 ambao moja ya malengo yake ni kuwa na ushirikiano kati ya waajiri, wadau na vyuo au taasisi za elimu.

Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba-Doran alisema ili Tanzania iweze kushiriki kikamilifu katika soko shindani la Afrika Mashariki na dunia ni lazima hatua za makusudi zichukuliwe katika kukuza ujuzi hususani kwa vijana.