Majaliwa ashtushwa na aina mpya ya bangi, watumiaji hubadilika na kuwa 'vichaa'

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwahutubia wananchi  kwenye maadhimisho ya uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru katika Viwanja vya Chuo cha Ushirika Moshi mkoani Kilimanjaro Aprili 2, 2024.

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kumeibuka aina mpya ya bangi yenye kiasi kikubwa cha kikevi


Moshi. Wakati Serikali ikipiga marufuku kilimo cha bangi nchini, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kumeibuka aina mpya ya bangi yenye kiasi kikubwa cha kilevi, watumiaji wakikitumia hubadilika na kuwa vichaa.

Amesema aina hiyo ya bangi ambayo hufahamika kama cha 'Arusha na Skanka' ina sumu nyingi na huchanganywa kwenye sigara huku akiwaonya vijana kuacha ili kunusuru maisha yao.

Majaliwa amesema hayo leo Aprili 2, 2024, wakati wa uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika  katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi(MoCU), mkoani Kilimanjaro.

Amesema Serikali imeendelea kupiga vita kwa kuzuia uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya nchini.

Majaliwa amesema matumizi na biashara ya dawa za kulevya imekuwa ni tatizo kubwa na kwamba dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi zimeendelea kutumiwa kwa wingi nchini.

"Hivi karibuni kumeibuka aina nyingine ya bangi yenye kiasi kikubwa cha kilevi, inayofahamika kama cha 'Arusha pamoja ba Skanka' aina hii ya bangi yenye sumu nyingi, huchanganywa kwenye sigara.

"Lakini ukishaitumia, watumiaji wanabadilika na kuwa vichaa. Ni wakati mzuri sasa wa vijana ambao mmekuwa mkitumika na kutumia muache ili kunusuru maisha yenu.

"Vijana mnahitajika katika Taifa hili, vijana ndiyo mtakaolijenga Taifa hili, vijana ndiyo muelekeo wa Taifa hili, cha 'Arusha na Skanka' vitawapoteza kwenye muelekeo, mtalifanya taifa hili likakosa Watanzania.”

Majaliwa amesema vijana wanaotumia bangi hizo  wanakuwa na uraibu na hatari na waathirika wengi wa matumizi ya dawa za kulevya  ni watoto na vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 24.

Ametaja mikoa inayoongoza kwa kilimo cha bangi nchini kuwa ni Mara, Morogoro, Arusha, Pwani, Kagera na Mwanza na kuonya wakulima kuacha kilimo hicho kwa kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa wale watakaobainika na kukanatwa.

Amesema mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 zitaendelea kutoa hamasa kwa jamii kusitisha kilimo haramu cha mirungi, bangi, biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini.

"Mwenge wa Uhuru 2024 utajielekeza katika kuhamasisha jamii kuondokana na kuachana na kilimo cha mazao haya haramu na badala yake kuhamasisha kilimo cha mazao halali ya biashara na chakula, lakini pia kuhamasisha jamii kushiriki mapambano dhidi ya dawa za kulevya,"amesema Majaliwa.

"Serikali imeongeza kasi ya mapambano yake na kutokomeza uzalishaji, usambazaji, matumizi na biashara ya dawa za kukevya na kuziba mianya yote katika vituo vya mabasi, viwanja vya ndege, vituo vya reli na maeneo mengine,"amesema Majaliwa.