KUTOKA LONDON : Je, bangi plastiki (“skunk”) inayozusha wazimu uzunguni itazagaa Afrika?

Muktasari:

  • Mwaka 2015 mtaalamu na mtafiti wa tumbaku na adha zake, Christian Chevalier, alionya kukua kwa desturi hii. Mfaransa, Chevalier alisema miaka 10 iliyopita ongezeko Afrika limeshafikia asilimia 70.
  • Takwimu zinatazamiwa kugonga asilimia 110 mwaka 2030. Ubaya nini?
  • Vijana wetu ndiyo waathirika wakubwa.

Kama kawaida mambo yakishazoeleka uzunguni baadaye husambaa ulimwenguni. Uvutaji sigara kwa vijana nchi za kizungu unaenea Afrika.

Mwaka 2015 mtaalamu na mtafiti wa tumbaku na adha zake, Christian Chevalier, alionya kukua kwa desturi hii. Mfaransa, Chevalier alisema miaka 10 iliyopita ongezeko Afrika limeshafikia asilimia 70.

Takwimu zinatazamiwa kugonga asilimia 110 mwaka 2030. Ubaya nini?

Vijana wetu ndiyo waathirika wakubwa.

Juu ya fegi sasa ni bangi.

Huku uzunguni bangi inavutwa utadhani lawalawa. Oktoba 2016, nilidokeza namna serikali ya Uingereza inavyopambana na kukua kwa dawa za kulevya. Wiki hii jopo la wanasayansi na waganga London limeonya kuwa bangi inayouzwa siku hizi siyo ile asilia.

Miaka 50 iliyopita, walitathmini wataalamu hawa, bangi ilitoka shamba na madhara yake hayakuwa mazito mbali ya “nishai” na usahaulifu unaoongozana nayo njia moja. Wavutaji bangi maarufu kama waimbaji wa Reggae (Marasta) wakiongozwa na Bob Marley waliandika hadi nyimbo na kuuita bangi “herb” yaani mmea au mboga. Leo , waganga wanasema bangi inayouzwa ina dawa maalumu zisizotokana na mimea na hurarua rarua ubongo mara moja.

Bangi hii ya plastiki - “skunk”- inauzwa kwa wingi wa asilimia 90 zaidi ya bangi asilia.

Hebu turejee katika misingi.

Kawaida, bangi ni jani lenye madhara; vile vile tiba likitumiwa sawasawa. Utafiti uliofanywa na waganga na watalamu uzunguni umeafiki tiba hii inasaidia baadhi ya aina ya magonjwa ya saratani, ulemavu wa sehemu fulani mwilini, mishipa ya fahamu nk. Hata hivyo, tiba hiyo inatakiwa jicho na usimamizi wa mganga. Sasa hivi Marekani ipo baadhi ya mikoa na halmashauri za jiji inayoruhusu tiba hii kwa leseni maalumu.

Hapo hapo wafanya biashara na wauza wa dawa za kulevya wanasambaza habari kuwa bangi ni tiba. Bangi nzima (“Cannabis”) siyo tiba. Ni kama vidonge vyovyote tunavyokunywa tukiugua. Vidonge hivi huchomolewa toka mimea iliyofanyiwa utafiti. Maarufu ni Quinine ya Malaria. Haina maana ukila Quinine inayotokana na ganda la mti wa Cinchona (kule Marekani ya Kusini) utapona Malaria.

Bangi ina madhara mengi ikiwemo usahaulifu, kutoamua mambo sawasawa na ulemavu wa akili. Ndiyo maana leo wengi wa Waafrika wazawa wa huku Uzunguni wenye matatizo ya akili (kama kusikia sauti au kelele zinazoasa kufanya vitendo viovu) walivuta bangi awali.

Tatizo la “skunk” yaani hii bangi mpya yenye kemikali ni zaidi. Profesa Robin Murray wa Kituo cha Saikolojia na Sayansi ya Mishipa ya Fahamu , Kings College, London ameonya juma hili kuwa bangi asilia humdhuru mtu baada ya miaka kadhaa ilhali ya sasa (“skunk”) ni kesho yake. Ugonjwa huu wa fahamu unaitwa “psychosis”....(tamka “saikosizi”)

Mgonjwa wa “psychosis” kupoteza kabisa ukweli wa hali halisi, kuwa na tabia za ajabu ajabu, juu ya kushindwa kuwasiliana na watu wengine.

“Skunk” ni tatizo kubwa Uzunguni.

Woga ni “skunk” ikienea Afrika, itakuwa na waathirika wengi kama yalivyo matumizi ya sigara.

Tovuti : www.freddymacha.com