Majaliwa ataka ufugaji wa kisasa, kilimo chapigiwa chapuo

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa hafla ya 'Uwekezaji Day' ya Benki ya CRDB iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Asema Serikali imefanya mageuzi ya kisera, kanuni na sheria ili kuwawezesha wanaojihusisha na sekta za mifugo, kilimo na uvuvi kunufaika

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekitaka Chama cha Wafugaji Tanzania kutoa elimu ya ufugaji kwa wanaojishughulisha na sekta hiyo ili waifanye kitaalamu.

Maelekezo hayo ya Majaliwa yametokana na kile alichoeleza, kumekuwa na utaratibu mbaya wa ufugaji nchini, unaoondoa thamani ya mifugo.

Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam leo Aprili 28, 2024, alipohutubia katika hafla ya Siku ya Uwekezaji iliyoandaliwa na Benki ya CRDB, ambayo hufanyika kila mwaka.

Katika maelekezo yake, Majaliwa amesema ni muhimu chama hicho kiendelee kuwajumuisha wafugaji na kuwaelimisha kuhusu ufugaji bora.

“Badala ya kuwazungusha ng’ombe nchi nzima, ng’ombe anatoka Tabora, anaenda Chunya mkoani Mbeya, kisha anaishia Masasi kule Mtwara, huo si ufugaji bora kwa sababu ng’ombe huyo hatakuwa na thamani maana misuli hailiki,” amesema.

Umuhimu wa elimu kwa wafugaji, unatokana na kile alichoeleza, tayari Serikali imefanya mageuzi ya kisera, kanuni na sheria ili kuwawezesha wanaojihusisha na sekta za mifugo, kilimo na uvuvi kunufaika.

Sambamba na mageuzi hayo, Majaliwa amesema wadau wa maendeleo, ikiwemo Benki ya CRDB imekuwa ikiwawezesha kwenye mnyororo wa thamani wa sekta hizo kukuza mitaji kwa kuwapa mikopo.

“Mkurugenzi ameniambia hapa ana mabilioni ya fedha anatafuta wakopaji, na nimearifiwa hapa na msanii wetu Mrisho Mpoto kwamba, hakuna taasisi iliyopunguza riba kutoka dijiti mbili hadi moja kama hii,” amesema.


Kuhusu kilimo

Katika sekta ya kilimo, Majaliwa ameeleza kufahamu juu ya uwepo wa kilimo cha muda mrefu, kinachofanywa kwa kutegemea hali ya hewa.

Ili kuondokana na hilo, amesema tayari Serikali imefungua milango kwa wawekezaji watakaowekeza kwenye maeneo ya utekelezwaji wa miradi ya umwagiliaji ili kuwezesha kilimo kufanyika muda wote.

Kwa upande wa sekta ya uvuvi, amesema vifaa mbalimbali vimegawiwa kwa wadau wanaojishughulisha na shughuli hizo ili kuwafaidisha Watanzania.

“Naipongeza CRDB kwa kuwaunga mkono vijana kwa kuwanunulia boti mpya zitakazowawezesha kupata mitaji na kuwawezesha kurudisha mikopo waliyochukua,” ameeleza.

Majaliwa ametumia jukwaa hilo kueleza umuhimu wa siku hiyo kufanyika Zanzibar mwakani, akisema zipo sekta zinazoguswa ikiwemo uchumi wa buluu.

Amesema Zanzibar imeiwekea sekta ya uvuvi wizara maalumu ili kuipa nafasi.

Majaliwa amewataka wadau wanaoshiriki semina hiyo kuhakikisha wanatoka na mapendekezo kwa ajili ya kuyawasilisha serikalini, huku akiahidi kuyafanyia kazi.

Katika hotuba yake, ameipongeza CRDB kwa kuendelea kufanya hafla kama hizo, akiisisitiza iendelee.

“Endeleeni kuandaa semina hizi si hii tu na nyingine na nyingine ili Watanzania wapate fursa ya kuielewa benki yao,” amesema.


Waziri Ulega

Awali, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema kwa sasa pamoja na mambo mengine shughuli hiyo imelenga kujadili kuhusu sekta ya kilimo na wadau waliopo katika mnyororo wa thamani.

Ili kuifanya sekta ya mifugo na uvuvi iendane na matakwa ya sasa, amesema mapitio ya sera, sheria na kanuni, ikiwamo kuhuishwa kwa sera ya mifugo ya mwaka 2006.

Pamoja na hilo, amesema wizara inaendelea na programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) katika sekta ya mifugo kwa ajili ya vijana wanaofanya shughuli ya unenepeshaji.

Katika programu hiyo, Ulega amesema ng’ombe 2,348 walikabidhiwa kwa vijana na sasa wamewauza 2,300 na kupata faida ya zaidi ya Sh100 milioni.

Si hivyo tu, amesema uchumi wa buluu haukuachwa nyuma, akieleza bandari ya uvuvi imejengwa Kilwa mkoani Lindi kwa ajili ya kuimarisha rasilimali za uvuvi.

Amesema Benki ya CRDB imekuwa mdau muhimu katika sekta ya mifugo na uvuvi kwa kuwa inaendelea kuongeza thamani na idadi ya mikopo kwa wadau wa sekta hiyo kila mwaka.

“Hapa juzi benki imesaini mkataba na Chama cha Wafugaji Tanzania kwa ajili ya kuwapa mikopo ya kunenepesha ng’ombe na hatimaye kuwaingiza kwenye biashara,” amesema.

Ameeleza benki hiyo pia, imetoa mikopo kwa wavuvi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam kuwawezesha kuboresha boti za uvuvi.

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Shaaban Ali Othman amewasihi wadau wa maendeleo na taasisi za kifedha kuwekeza Zanzibar, hasa kwenye uchumi wa buluu na kilimo.

Amesema hadi sasa CRDB ina mchango wa Sh30.9 bilioni kutokana na uwezeshaji mbalimbali katika wizara hiyo.

"Hii yote imewezekena kutokana na jitihada, utayari wa Serikali katika kukuza uchumi kwa kushirikisha sekta binafsi na ukuaji mtambuka ukiwamo wa kilimo na mifugo kupitia benki hii," amesema.

Amesema sekta ya kilimo inakua haraka kwa Tanzania Bara kwa sababu ya matumizi ya ardhi ambayo kwa upande wa Zanzibar wanalima kwenye bahari.

Amesema kwa utashi wa Serikali zote mbili uwekezaji umeendelea kufanyika kwa kuruhusu sekta binafsi kuwekeza.

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesisitiza taasisi za fedha ziendelee kutoa mikopo kwa wadau kwenye sekta za kilimo kwa kuwa matunda yake yameanza kuonekana.

Amesema sekta hiyo pekee imeingiza Dola za Marekani 2.3 bilioni zilizotokana na mauzo ya nje.

Amewataka wananchi kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya kilimo kwa kuwa manufaa yake ni makubwa.

"Tumekuwa tukipoteza mazao hususani kwenye mazao ya mbogamboga kwa asilimia 11 hivyo tukiwekeza kwenye eneo hili tutaongeza kipato," amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema Sh26 bilioni zimetengwa kwa ajili ya sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

Amesema sekta hizo ni miongoni mwa zinazofanya vizuri katika ulipaji wa mikopo.

"CRDB itaendelea kushirikiana na sekta hizo kwa kuhakiki mnyororo wa thamani unafikiwa na hatimaye kukuza uchumi wa nchi," amesema.

Amesema mfumo uliobuniwa na Wizara ya Kilimo kwa miaka mitatu iliyopita kwa ajili ya kukopesha na kulipa wanunuzi wa mazao wa kawaida hawakuendelea nao katika sekta za mifugo na uvuvi na hata kuwakifia wavuvi wengi zaidi kwenye mikopo japo haukuwa rasmi.

"Ahadi yetu tumejipanga mahususi kutoa mchango kusaidia sekta za uvuvi na kilimo, na mafanikio yetu yatakuwa imara zaidi tukiwa karibu na wizara husika kwa kuangalia changamoto kwa pamoja, lakini kuunda mnyororo wa pamoja kusaidia sekta hii," amesema.