Majaliwa kuanza ziara ya kikazi Mtwara

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Muktasari:
- Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajia kuanza ziara ya siku saba mkoani hapa leo Alhamisi Julai 6, 2023.
Mtwara. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajia kuanza ziara ya siku saba mkoani hapa leo Alhamisi Julai 6, 2023.
Mara baada ya kuwasiri mkoani hapa leo, Waziri Mkuu Majaliwa atashiriki uzinduzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Aidha kuanzia Julai 8, 2023 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atakagua, kuweka mawe ya msingi lakini pia atambelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri za mkoa wa Mtwara.
Miradi hiyo ni pamoja na jengo la wagonjwa wa nje katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Ligula, chujio la maji eneo la Mangamba unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji mkoani hapa (MTUWASA), Hospitali ya Kanda ya Kusini ya Mitengo na Bandari ya Mtwara.
Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa jengo la utawala na ujenzi wa kituo cha afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara eneo la Mkunwa.
Aidha Waziri Mkuu pia atafanya mkutano ya hadhara na kuzungumza na wananchi katika halmashauri za mkoa huu.
Ziara ya Waziri Mkuu mkoani hapa inatarajia kuhitimishwa Julai 14, 2023.