Makada Chadema walioshinda rufaa wapewa ng’ombe

Wanachama wa Chadema kata ya Dutwa wilayani Bariadi mkoani Simiyu, Kitala Kikaja (Kulia) na Ng'hulima Ilanga (Kushoto) wakiwa katika Ofisi za chama hicho Kanda ya Serengeti baada ya kushinda rufaa ya kesi yao iliyowafunga kwa makosa ya wizi, kubaka na unyang'anyi wa kutumia silaha. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • "Baada ya dhiki, faraja," ndivyo unavyoweza kueleza kitendo cha wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Serengeti kununua ng'ombe wanne na kuwakabidhi makada wawili wa chama hicho walioshinda rufaa yao mkoani Shinyanga ikiwa ni mkono wa pole kwa matatizo waliyopitia.

Mwanza. "Baada ya dhiki, faraja," ndivyo unavyoweza kueleza kitendo cha wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Serengeti kununua ng'ombe wanne na kuwakabidhi makada wawili wa chama hicho walioshinda rufaa yao mkoani Shinyanga ikiwa ni mkono wa pole kwa matatizo waliyopitia.

Katala Kikaja (27) na Ng’hulima Ilanga (35), wakazi wa Dutwa wilayani Bariadi mkoani Simiyu walihukumiwa kifungo cha maisha jela na mahakama ya Hakimu mkazi wilayani humo kwa kosa la kubaka, wizi na unyang’anyi wa kutumia silaha.

Vijana hao ambao walikuwa mawakala wa mgombea udiwani wa Dutwa kwa tiketi ya Chadema mwaka 2020, Saguda Bulahya walikamatwa baada ya kugomea matokeo wakishinikiza mgombea wao atangazwe mshindi baada ya kumshinda yule wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Msimamo huo ndio ulimfanya mgombea huyo kugoma kusaini fomu ya kukubali kushindwa uchaguzi huo, lakini mgombea wa CCM akatangazwa kwa mabavu,

Oktoba 29 mwaka 2020, Kikaja na Ilanga wakakamatwa na kufunguliwa mashtaka kabla ya kuhukumiwa kifungo cha maisha.

Kwa siku 748, makada hao waliishi gerezani tangu walipokamatwa Oktoba 29, 2020 na kuhukumiwa kifungo Aprili 12 mwaka 2022, kisha Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Athuman Matuma kuwaachia huru Novemba 16, 2022.

Kwa siku 23 nje ya gereza, wanachama wa Chadema Kanda ya Shinyanga walichangisha Sh2 milioni kwa ajili ya kutoa mkono wa pole kwa makada hao waliodai kuponzwa na msimamo wao wa kisiasa.

Akizungumza na Mwananchi jana, Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami alisema fedha hiyo ilitumika kununua ng'ombe wanne na kondoo watatu ambao waligawanywa kwa makada hao.

"Wanachama wetu walichangishana fedha hiyo ili kununua ng'ombe na kondoo ambao wametolewa kama mkono wa pole kwa makada hawa ambao kwa kipindi chote walichosota gerezani hawakuwa wanazalisha kipato hivyo mifugo hii itakuwa mtaji kwao na familia zao," alisema Mnyawami

Makamu Mwenyekiti wa Chadema kanda hiyo, Gimbi Masaba pamoja na kutoa pole kwa familia za makada hao, alisema utoaji wa mifugo hiyo ni mwendelezo wa chama kujali ustawi wa wanachama wake bila kujali changamoto wanazopitia.

"Tumekuwa tulishirikiana kufarijiana wanachama wetu wanapopata changamoto ikiwemo zilizowapata Katala na Ng'hulima. Hivyo niwatake wana Chadema kutokata tamaa, waendeleze mapambano ya kudai demokrasia bila hofu chama chao kipo nyuma yao," alisema Gimbi

Akizungumza baada ya kukabidhiwa mifugo hiyo, Katala Kikaja alisema ng'ombe hao watakuwa mtaji kwake kwani hakuwa na shughuli yoyote ya kumzalishia kipato tangu aachiwe huru huku Ng'hulima Ilanga akisema atatumia ng'ombe hao kwenye shughuli za kilimo.

"Sisi ni wakulima, hawa ng'ombe watatusaidia kwenye shughuli za kilimo lakini pia tutawatumia kama mtaji wa kuanzisha shughuli za kutuzalishia kipato kwa ajili ya kuhudumia familia zetu," alisema Kikaja