Makala: CCM kitashinda kwa kishindo, atangaza ziara

Muktasari:

  • Sekretarieti itafanya ziarani mikoa sita kuanzia kesho.

Dodoma. Sekretarieti ya chama cha CCM kesho itaanza ziara kwenye mikoa sita kwa malengo manne, ikiwemo maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2025.

 Malengo mengine ni kukiimarisha chama, kusikiliza kero za wananchi na kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Aprili 12, 2024 jijini Dodoma na  Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla wakati wa mapokezi ya sekretarieti ya chama hicho.

“Tunatest mitambo, sisi na katibu wetu mkuu, Dk John Nchimbi kesho tunaanza ziara ya mikoa sita, maandalizi yalishafanyika leo natangaza tu,” amesema.

Amesema kesho wataanza na mkoa wa Katavi, ukifuatiwa na Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na kisha Ruvuma.

Makalla amesema ziara yao ina mambo makubwa manne ambayo ni kwenda katika msingi wa chama hicho ambao ni shina na tawi, lengo likiwa ni kuona uhai wa chama.

“Tunajua tuna mtaji mkubwa, lakini pia tunakwenda kubadilishana uzoefu na wanachama mtatuona huko, tunakwenda kuimarisha chama chetu. Kuna wakati wa usajili unaona timu zinafanya hivyo na matokeo wanayapata,” amesema.

Amesema wakati wao wanapiga kazi na wengine waendelee kupiga domo na kwamba matokeo yake watashinda uchaguzi kwa vishindo.

Amesema lengo jingine ni maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani, hivyo wanakwenda kuandaa umma, ili wajue umuhimu wa kujiandikisha na kupiga kura.

Makalla amesema lengo jingine ni kukagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi na kwamba kuna mambo mengi yamefanywa, lakini msisitizo wao ni kuyatangaza yaliyofanyika.

Pia amesema lengo jingine ni kusikiliza na kutatua kero za wananchi, licha ya kutambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika eneo hilo.