Makalla na mtindo tofauti kusikiliza kero za wananchi

Muktasari:

  • Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetoa wito kwa wananchi kutoa kero za kwa viongozi wa Serikali pindi tangazo linapotolewa badala ya kusubiri viongozi wa chama kufika

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema mtindo wa kusikiliza kero katika mikutano ya hadhara umebadilika hivi sasa wananchi wenye changamoto wataziwasilisha pembeni badala ya hadharani.

Makalla ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Aprili 13, 2024 katika Uwanja wa Kashaulili wilayani Mpanda Mkoa wa  Katavi katika mkutano wa hadhara wa uliohutubiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi.

Kabla ya kuanza mkutano huo, akiwa jukwaani Dk Nchimbi alidokeza kuwa hivi sasa wanasikiliza kero za wananchi na kuzipatia majibu kwa njia ya bora zaidi.

Baada ya maelezo hayo Dk Nchimbi aliwataka wananchi wenye kero kumfuata Makalla aliyeketi pembezoni mwa mkutano huo akiambatana na watalaamu, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za Mkoa wa Katavi.

"Wote wenye kero nendeni kwa Makalla ambaye akimaliza kuzikusanya nitampa nafasi ili zile zenye kumalizwa hapa hapa basi zimalizwe zenye kulala zilale," amesema Dk Nchimbi.

Baada ya Dk Nchimbi kumaliza kuhutubia alimuita Makalla kutoa marejesho kuhusu kero alizozikusanya kutoka kwa wananchi akisema kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya wamefanikiwa kusikiliza kero mbalimbali.

"Mimi mwenyewe nimeratibu majina 27 na kero zao, nataka nikuhakikishie katibu (Dk Nchimbi), hakuna hata kero moja ya kuondokana nayo sisi hapa. Kero zilizopo ikiwamo fidia kupisha barabara ya Stalike- Vikonge zina uwezo wa kutatuliwa hapahapa," amesema Makalla.

Makalla amewataka wote wanaohusika na masuala ya fidia kufungua milango ili kulipa wananchi, endapo wakishinda basi watoe mrejesho ili chama hicho kiingilie kati kutoa msukumo zaidi.

"Kwa hiyo mheshimiwa katibu mkuu leo tumesikiliza kero lakini umesikia makelele yoyote...? Kwa sababu ukisikiliza kwa kelele sana mambo mengine ni ya siri  lazima umpe mtu faragha.

"Tutaendelea kusikiliza kero za wananchi katika mikutano yetu lakini kwa njia nzuri isiyozusha tafrani, lakini usikilizaji utakuwa na mambo mawili lazima tutoe majibu kwa wananchi," amesema Makalla.

Mtindo huo mpya ni tofauti na iliyokuwa ikitumia na mwenezi aliyepita Paul Makonda ambaye aliwataka wananchi kujitokeza mbele ya jukwaa kuu na kutoa kero zao zinazowakabili na watendaji wa Serikali kuzitolea majibu papo.

Zile kero zilizooneka kuhitaji ufafanuzi zaidi Makonda alilazimika kuwapigia simu mawaziri wa sekta husika ili kupata majibu au ufafanuzi unaojitosheleza.

 Hatua hiyo ilifurahiwa na wananchi ila iliwapa wakati mgumu watendaji wa Serikali waliobainika kutotoa majibu sahihi na kufanya Makonda kuingilia kati kuwabananisha.