Nchimbi: Ukishindwa uchaguzi CCM kubali matokeo

Balozi na mwenyekiti wa Shina namba 5, Mtaa wa Paradise, Majengo mjini Mpanda, Hadija Kapena akiongoza kikao na kumkaribisha Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi kuzungumza katika kikao hicho leo Aprili 13. Picha na CCM

Muktasari:

Awataka wagombea wanaoshindwa katika uchaguzi ndani ya chama hicho kutoa ushirikiano kwa washindi badala ya kujenga chuki ambazo hazina msingi.

Katavi. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amewataka WanaCCM kuendesha kwa haki uchaguzi wenye ushindani wa kweli ndani ya chama hicho akiwasihi wanaoshindwa kukubali matokeo na kuwaunga mkono walioshinda.

Dk Nchimbi amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya WanaCCM ikitokea amepata kura chache katika kinya'ng'iro, basi anatafuta mwanachama au wanachama wasiomuunga mkono katika mchakato huo na kuanzisha chuki dhidi yao.

Katibu mkuu huyo ameeleza hayo leo Jumamosi Aprili 13, 2024 akizungumza katika kikao cha ndani na viongozi wa CCM wa ngazi mbalimbali wa mkoa wa Katavi.

Dk Nchimbi na baadhi ya wajumbe wa sekretarieti wameanza ziara kuimarisha chama katika mikoa sita akianzia Katavi.

"Katika chama chetu kuna changamoto moja wanaoshinda mioyoni mwao wanakataa matokeo na walioshindwa mioyoni mwao wanakataa matokeo, si wengi lakini wana madhara makubwa,” amesema.

"Mtu anachaguliwa kuwa mwenyekiti wa tawi, kata, wilaya,  shina au mwenyekiti wa mkoa, lakini akishachaguliwa anaanza kutafuta nani hakumuunga mkono ili aanze kupambana naye, yaani katika akili amejitengeneza kuwa ni mungu-mtu lazima apigiwe kura na kila mtu, ni tabia ya kijinga kabisa,"  amesema.

Amewataka wanaCCM kutambua kuwa wakiingia katika uchaguzi kila mtu ana haki sawa katika mchakato huo, sambamba na kujua kuwa wana dhamira ya uongozi.

Amesema mtu yeyote mwenye dhamira ya utumishi anaikana nafsi yake na kutambua kuwa anakwenda kuwatumikia wote.

"Wakati mwingine usipochaguliwa unahisi umepungikiwa mzigo, lakini watu wetu wasipochaguliwa wanahisi wamepata tatizo au ugonjwa wa kudumu... huu ni ugonjwa na ubinafsi uliokithiri, lazima tuache kwa masilahi ya chama chetu," amesema Dk Nchimbi.

Amesema CCM ndio chama kinachotawala kinachotoa dira na mwelekeo wa nchi,  hivyo yanayofanyika ndani ndio yanayoakisiwa na vyama vingine, akisema vyama vingine vikionekana vinakataa matokeo basi, vinaiga kutoka katika chama hicho tawala.

"Mtu unapigwa mchana kweupe halafu unakataa matokeo, hata vyama vingine inafika wakati vinashindwa kujua vimejifunza wapi chuki, kumbe kuna watu wawili, watatu CCM ndio wamewafundisha tabia ya kukataa matokeo na kuchukia wenzao," amesema Dk Nchimbi.

Amesema CCM inatekeleza demokrasia ya kweli ikiwa ni pamoja na kuhakikisha chaguzi zake zinakuwa huru na kukubali matokeo, akisisitiza kiongozi wa kweli ni yule anayekubali matokeo bila kusita.

"Mimi hapa nimeongea mara 28, nimeshindwa mara nne, tena vizuri sio kidogo, lakini nimegombea nikitambua kuwa ni uchaguzi kuna kushindwa na kushinda," amesema.

Amewataka WanaCCM wote kuheshimu utaratibu wa kidemokrasia uliopo ndani ya chama hicho, kuendesha chaguzi za haki na kukubali matokeo kwa moyo wa dhati na kuwasaidia walioibuka kidedea.

"Niwaombe wanaoshinda uchaguzi katika ngazi zote kiongozi wa kweli ni mnyenyekevu na asiyebagua anaowaongoza na kuwaunganisha watu wote wa chini yako. Huwezi kuwa wewe una vikosi vya upelelezi unawatafuta wanasema nini, binadamu ana haki ya kufikiri anaweza akayaona ya kwako mazuri 100 akayaongelea na mabaya mawili akayaongelea.

Dk Nchimbi amesisitiza viongozi wa CCM wanaochaguliwa kuwa wanyenyekevu na kuwaunganisha watu, akisema watawapima kwa namna wanavyounganisha watu sio kuwagawanya.

Aidha wakati wa ziara hiyo Katibu wa Oganaizesheni wa CCM, Issa Ussi Gavu amewataka WanaCCM kwenda kuwahamasisha wananchi kujiunga na chama hicho ili kuwa na mtaji wa kura utakaokiwezesha chama hicho kuibuka kidedea katika uchaguzi ujao.

"Nenda mkawahamishe ili wawe wafuasi na wanachama wetu, tukiwa na idadi kubwa maana yake ushindi utakuwa mkubwa, twendeni tukawahimize ndugu zetu na watoto wetu ili wawe wanachama dhabiti," amesema.

Pia amewataka viongozi wa CCM wa wilaya kuhakikisha wanatenda haki katika kuwateua viongozi watakaowania nafasi ya uenyekiti wa kijiji, vitongoji na vitongoji.

Gavu amewataka viongozi wa chama hicho kuacha  kupanga safu kwa kuogopa wabunge na madiwani, kwa kuwa wanachohitaji CCM ni ushindi usiotokana na makandokando na kuwa kwa kazi nzuri iliyofanywa na Serikali wakiwa na wagombea wazuri watashinda.

"Viongozi tuliopewa jukumu tutahakikisha tunateua wagombea wenye sifa, tusipofanya hivyo tutawanyima haki. Ndani ya CCM kuna makada wengi wenye sifa hatuna sababu ya kuwakumbatia watu wasiokuwa na sifa.”

Gavu amewataka viongozi wa mkoa kusimamia vema mchakato kuhakikisha wagombea wanapatikana kwa njia ya halali si kwa rushwa au makandokando na kusababisha chama hicho kukosa ushindi katika mtaa, vijiji au vitongoji.