Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makandarasi wasiomaliza kazi kutopewa zabuni mpya REA

Muktasari:

  • Utekelezaji wa mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili ulipaswa kukamilika ndani ya miezi 18 lakini hadi sasa ni miezi 30 kuna maeneo bado wakandarasi hawajamaliza kazi, hivyo kusababisha vijiji kukosa umeme.

Dar es Salaam. Wakati utekelezaji wa mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili ukifika ukingoni Juni mwaka huu, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetoa angalizo kwa wakandarasi ambao hawatamaliza kazi zao kufikia muda huo wasijisumbue kuomba zabuni za miradi mingine.

Utekelezaji wa mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili ulipaswa kukamilika ndani ya miezi 18 lakini hadi sasa ni miezi 30 kuna maeneo bado wakandarasi hawajamaliza kazi, hivyo kusababisha vijiji kukosa umeme.

Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amesema hayo jana wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa wakandarasi waliofanya vizuri kwa kumaliza kazi ndani ya muda uliopangwa.

Saidy amesema katika mradi wa kupeleka umeme vijijini hawawezi kuendelea na wakandarasi ambao wanashindwa kufuata masharti ya mikataba, hivyo wasijisumbue kuomba zabuni.

“Ni kweli tumefanya kazi na ninyi kwa muda mrefu lakini tunakoelekea tunahitaji kasi na ubora, wananchi wanahitaji umeme sasa kama kutakuwa na ucheleweshaji wa aina hii hatuwezi kuendelea pamoja ndiyo maana nasema wala msipoteze muda wenu kuomba zabuni kwa kuwa hatutawapa,” amesema Saidy.

Amesema pamoja na kutowapa zabuni, wakala utawachukulia hatua wakandarasi wote ambao watakuwa hajakamilisha kazi ya kupeleka umeme kwenye vijiji walivyopewa kufikia Mei, mwaka huu.

“Tuna vitongoji 32,000 ambavyo tunaenda kuvipelekea umeme, sasa kama hujamaliza kazi yako zabuni hizi hazikuhusu. Kazi ilitakiwa kukamilika ndani ya miezi 18 tumefika miezi 30 bado kuna wenzetu hawajamaliza kazi,"amesema.

Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Jones Olotu amesema hadi Aprili 12 mwaka huu, vijiji 479 vilikuwa havijafikiwa na umeme ili kukamilisha lengo la vijiji vyote 12,318 vilivyopo nchini kuwa vimeunganishwa nishati hiyo.

Amesema tathmini iliyofanywa mwaka 2020 inaonyesha hali ya upatikanaji wa umeme vijijini imefikia asilimia 69.9 kutoka asilimia mbili ya mwaka 2007.

Amesema ni matumaini yake kuwa tathmini nyingine itakayofanyika mwaka 2025 upatikanaji wa umeme vijijini utakuwa zaidi ya asilimia 75.

“Kufanikisha hilo tunategemea kila mkandarasi atatekeleza jukumu la kujenga heshima ya kazi yake, tunategemea utekelezaji wa majukumu yenu kwa ufanisi utawezesha kufikia lengo la kufikisha umeme kwenye vijiji vyote,” amesema.

Amesema kwa sasa kuna orodha ya wakandarasi 21 ambao hawajakamilisha kazi kwa asilimia 100 kati yao 13 ni wazawa na wanane kutoka nje ya nchi.

“Tuna wakandarasi watatu wako kati ya asilimia 70 hadi 76, wakandarasi tisa wako kati ya asilimia 80 hadi 89 na wakandarasi 10 wapo kati ya asilimia 90 hadi 99. Matarajio ni kufikia Juni 30 kazi iwe imekamilika,” amesema.

Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Jacob Kingu amewataka wakandarasi kuhakikisha wanamaliza kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa ili kufanikisha lengo la vijiji vyote kuunganishwa na umeme.

“Vijiji ambavyo havijakamilika viwekewe mkakati ili kazi ikamilike, hakutakuwa na kuongezewa muda. Bodi tutapita kukagua lengo ni kuhakikisha Watanzania wanapata umeme,” amesema.