Makombora ya Russia balaa nchini Ukraine

Muktasari:

  • Uamuzi wa Rais wa Russia, Vladimir Putin kuanza mashambulizi ya angani na ardhini nchini Ukraine umezua balaa na kuwalazimu wananchi kukimbia maeneo yao kuokoa maisha huku wanajeshi watano wa Ukraine wakiuawa katika siku ya kwanza.


Kyiv, Ukraine. Uamuzi wa Rais wa Russia, Vladimir Putin kuanza mashambulizi ya angani na ardhini nchini Ukraine umezua balaa na kuwalazimu wananchi kukimbia maeneo yao kuokoa maisha.

Wiki kadhaa za usuluhishi wa diplomasia na Russia kuwekewa vikwazo na mataifa ya Magharibi hazijamzuia Putin, ambaye amekusanya zaidi ya wanajeshi 150,000 kwenye mipaka na Ukraine, kutoa amri hiyo.

“Nimeamua kuendelea na operesheni ya kijeshi,” alisema Putin katika tangazo la televisheni ambalo lilizua shutuma za mara moja kutoka kwa Rais wa Marekani, Joe Biden na viongozi wengine wa nchi za Magharibi.

Uamuzi huo umesababisha soko la fedha duniani kuyumba.

Muda mfupi baada ya tangazo hilo, milipuko ilianza kusikika katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv na miji mingine kadhaa, kwa mujibu wa AFP.

Walinzi wa mpaka wa Ukraine walisema vikosi vya ardhini vya Urusi vimevuka mpaka hadi Ukraine kutoka kaskazini na kusini.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema Russia  inashambulia miundombinu ya kijeshi ya nchi yake, lakini akawataka raia wasiwe na hofu huku akiahidi ushindi.

Mkuu wa jeshi la Ukraine, Meja Jenerali Valeriy Zaluzhny alisema amepokea amri kutoka kwa Zelensky kuzuia uvamizi huo na “kusababisha hasara kubwa dhidi ya mvamizi.”

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kyiv ulipigwa katika shambulio la kwanza la bomu katika mji huo na ving’ora vya mashambulizi ya anga vilisikika alfajiri jana.

“Niliamka kwa sababu ya sauti za mlipuko. Nilifunga begi na kujaribu kutoroka,” alisema Maria Kashkoska, alipokuwa amejihifadhi katika ya Kituo cha Treni Kyiv.

Ksenya Michenka alionekana kutetemeka alipokuwa akijificha na mtoto wake wa kiume.

“Tunahitaji kuokoa maisha yetu,” alisema.

Katika mji wa Chuguiv mashariki mwa Ukraine, mtoto wa kiume alilia juu ya mwili wa baba yake na pembeni ya mabaki ya kombora katika wilaya hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba alisema hali mbaya zaidi ilikuwa ikitekelezwa na kuwa watu kadhaa walikuwa wamepoteza maisha.

“Putin ameanzisha uvamizi kamili wa Ukraine. Miji yenye amani ya Ukraine inashambuliwa,” Dmytro Kuleba aliandika kwenye Twitter.

“Hivi ni vita vya uchokozi. Ukraine itajilinda na itashinda. Ulimwengu unaweza na lazima umkomeshe Putin. Wakati wa kuchukua hatua ni sasa.”

Ndani ya saa chache baada ya hotuba ya Putin, Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema kuwa imepunguza kambi za kijeshi za Ukraine na mifumo yake ya ulinzi wa anga.

Ukraine ilisema vifaru na silaha nzito za Urusi zilivuka mpaka katika maeneo kadhaa ya kaskazini, mashariki na peninsula ya kusini.

Katika masoko ya fedha, hisa za Ulaya zilishuka na bei ya mafuta ilipanda zaidi ya Dola 100 kwa pipa.

Sarafu ya Russia, ruble, pia ilishuka kwa asilimia tisa dhidi ya dola baada ya shambulio hilo na Soko la Hisa la Moscow kuporomoka kwa karibu asilimia 14.

Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni, Putin alihalalisha operesheni hiyo kwa kudai kuwa serikali inasimamia “mauaji ya halaiki” mashariki mwa nchi.

Ikulu ya Kremlin awali ilisema viongozi wa maeneo mawili yanayotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine wameomba msaada wa kijeshi wa Urusi dhidi ya Kyiv.

Biden, ambaye kwa muda wa wiki kadhaa aliongoza muungano wa nchi za Magharibi kumzuia Putin kuivamia Ukraine, alizungumza na Zelensky baada ya operesheni ya Urusi kuanza na aliapa kwamba Marekani itaiunga mkono nchi hiyo na kuipatia msaada.

Biden alilaani shambulio lisilo la msingi la vikosi vya Urusi na kuwataka viongozi wa ulimwengu kuzungumza dhidi ya uchokozi wa wazi wa Putin.

Pia, aliapa kwamba Russia itawajibishwa.

“Rais Putin amechagua vita vilivyokusudiwa ambavyo vitaleta hasara kubwa kwa maisha na mateso kwa wanadamu,” alisema katika taarifa yake.

Jana, Biden alipaswa kujiunga na mkutano wa mtandaoni wa mlango wazi wa viongozi wa G7, nchi za Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan na Marekani.

Mkutano wa G7 huenda ukasababisha vikwazo zaidi dhidi ya Russia, ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ikidai haitaivamia Ukraine, licha ya kuwa na wanajeshi wengi kwenye mipaka ya nchi hiyo.