Makonda: Naweza kuwa kiongozi mnayemtaka

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul, Makonda amesema anaweza kubadilika na kuwa kiongozi wa aina yeyote ambaye wananchi wanamhitaji, huku akieleza kuwa wakitaka kasi ataongoza kwa kasi.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema anaweza kuwa aina yeyote ya kiongozi ambayo wananchi wanataka, jambo ambalo anajivunia na kumshukuru Mungu.

 Makonda ametoa kauli hiyo leo, Jumatatu ya Aprili 8, 2024 jijini Arusha alipokuwa akikabidhiwa ofisi tangu alipoteuliwa na kuapishwa kwa ajili ya kuongoza mkoa huo akitoka katika nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Naweza kujifunza na kuwa kiongozi wa aina yoyote, ukitaka niwe kiongozi anayekaa na Kadinali Polycarp Pengo tunasoma sala nitakuwa, ukitaka kiongozi anayekaa na Jenerali tukaenda kwa kwata nitakuwa, kokote kule unapotaka nitakuwa,” amesema Makonda.

Amesema yeye kama kiongozi hubadilika kutokana na mahitaji ya wananchi na kasi atakayokuwa nayo huku akisema mahitaji yakiwa makubwa naye anakwenda kwa mwendo huo na mahitaji yakiwa kidogo, atashindwa kwenda kwa kasi kubwa, ili asiwaache wengine nyuma.

“Nafikiri moto mmeuona katika nafasi yangu ya uenezi, kwa hiyo kasi yenu tu, mkitaka Arusha ibadilike kuwa mji wa amani na utulivu na hata mwananchi anaweza akasahau simu yake mahala akaitiwa utakuwa, mkitaka Arusha uwe mji wa kibiashara watu hawafungi maduka saa 11 jioni wanakesha wanaweza kufanya biashara kama wanavyofanya Kariakoo na sehemu nyingine Dubai itakuwa,” amesema Makonda.

Amesema hata wakitaka barabara zipitike kwa lami itakuwa hivyo na hata chochote watakachotaka kitakuwa, huku akisema sababu moja ni uwepo wa Mwenyezi Mungu anayesema ‘Ombeni chochote mnachotaka mtapewa’ na Rais Samia Suluhu Hassan katika nafasi ya pili anayeipenda Arusha hadi kuamua kumtoa yeye kwenye nafasi ya uenezi na kumfanya mkuu wa mkoa.

“Huo ni upendo wa aina gani jamani, maana yake ameitazama Arusha hadi akasema hapana, kuna mambo nataka yafanyike pale na hata katika historia, Arusha ni mkoa ambao ameutembelea mara nyingi kuliko mkoa wowote,” amesema Makonda.

Amesema kudhihirisha hilo, Aprili 12, 2024 Rais Samia atatembelea tena Arusha, ikiwa ni ishara kuwa ana jambo analotamani litokee.