Malori ya mizigo yakwama mpakani Malawi, barabara yafungwa

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa Mbeya, Juma Homera amekiri kuwepo kwa tukio hilo na tayari Serikali imeanza kuchukua hatua za haraka kuhakikisha yanaachiwa na kuanza kuingia nchini.

Mbeya. Wafanyabishara wa Kasumulu Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya wamefunga barabara inayoelekea kituo cha pamoja cha forodha kati ya Tanzania na Malawi kushinikiza magari zaidi ya 60 yaliyobeba shehena za mizigo yaliyozuiwa nchini Malawi kuachiwa.

Akizungumza na Mwananchi Digital, leo Jumatatu June 5, 2023 Diwani Kata ya Njisi mpaka wa Kasumulu, Omary Rashid amesema kuwa shehena hizo za mizigo zimezuiwa kwa takribani mwezi mmoja na nusu sasa hali inayopelea hofu ya hasara kwa wafanyabishara.

“Tukio hilo ni kweli lipo wafanyabishara wa Tanzania wamezuiwa nchini Malawi kuingiza bidhaa nchini yakiwepo mazao, vyuma chakavu na nyingine nyingi hali ambayo inahatarisha usalama wa chakula kutokana na muda ambao yamezuiwa,”amesema.

Amesema kuna kila sababu Serikali za nchi hizo mbili kukutana kujadiliana na kuona namna bora ya kulimaliza ili kusaidia wafanyabishara kuepuka hasara ambayo inaweza kujitokeza kutokana na mazao kuharibika

Rashid amesema kuwa mpaka sasa ni mwezi mmoja na nusu wafanyabishara wako nchini Malawi na shehena za mizigo zikiwa kwenye magari pasipo kujali  wafanyabishara wana mikopo ambayo marejesho yanayokana na bidhaa wanazoingiza nchini.

Mfanyabishara Diblo Amos amesema ufike wakati Serikali ya Malawi iwe na ushirikiano na Wafanyabishara wa Tanzania na ndio lengo la Serikali kuweka kituo cha pamoja cha forodha ili kuchochea muingiliano wa shughuli za kiuchumi kati ya nchi hizo.

“Kuna ndugu yangu tangu kaenda kufunga mzigo sasa ni mwezi kakwama kurejea na anasema kuna magari zaidi 60 yote yana mizigo yakiwepo mazao yamezuiwa kuingia nchini pasipo sababu za msingi,”amesema.

Alipotafuta Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera kuhusu hali hiyo mpakani hapo amesema amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kwamba Serikali inalishughulikia wakati wowote magari yaliyozuiliwa yataanza kuingia nchini.

“Suala hili kwa sasa linashughulikiwa kwa haraka sana na muda wowote kuanzia sasa magari yenye shehena za mizigo ya wafanyabishara yataanza kuingia nchini,”amesema Homera.