Wafanyabiashara waandamana baada kuzuiwa kuvusha mahindi Kenya

Shehena ya magari yenye mahindi kwenda nchi jirani ya Kenya ikiwa imekwama katika mpaka wa Holili uliopo Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro katika mpaka wa Kenya na Tanzania baada ya magari hayo kuzuiwa kuingia nchi jirani. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Wafanyabiashara wa mahindi katika soko la Kimataifa la mazao Holili, lililopo Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro leo asubuhi Juni Mosi wameandamana mpaka ofisi za Forodha mpakani mwa Kenya na Tanzania, baada ya shehena zao za mahindi kuzuiwa katika mpaka huo.

Rombo. Wafanyabiashara wa mahindi katika soko la Kimataifa la mazao Holili, lililopo Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro leo asubuhi Juni Mosi wameandamana mpaka ofisi za Forodha mpakani mwa Kenya na Tanzania, baada ya shehena zao za mahindi kuzuiwa katika mpaka huo.

Wafanyabiashara hao wameeleza kukwama katika mpaka huo kwa siku nne baada ya kuzuiliwa kupita katika mpaka huo kupeleka mahindi katika nchi jirani hali ambayo imezua sintofahamu kwa wafanyabiashara hao.

Mwananchi limefika katika eneo hilo na kushuhudia magari yenye shehena ya mahindi yakiwa kwenye foleni ambapo muda mfupi baadaye magari hayo yaliruhusiwa kuendelea na safari.

Kufuatia hali hiyo, Gazeti hili lilimtafuta Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro, James Jilala kujua ni kwa nini magari hayo yenye shehena hiyo yamezuiliwa ambao amesema wao wamepata maelekezo kutoka juu kusitisha mahindi kutokutoka nje ya mpaka huo.

"Tulipata taarifa kutoka kwa viongozi wa juu kwamba tusitishe mahindi yasitoke nje ya nchi ya Tanzania na baadaye tumeletewa taarifa hilo zoezi limeahirishwa kwa muda wa siku kadhaa na wameambiwa ni baada ya muda gani ndio sasa litakuwa limekuja zuio," amesema Jilala.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyabiashara hao, wamesema kukwama kwao kwa siku nne wamepata hasara kubwa kwa kuwa mahindi yao bado yalikuwa hayajakauka vizuri.

Frank Kachema, ambaye ni mfanyabiashara wa mahindi katika mpaka huo amesema zuio hilo ambalo limedumu kwa siku nne limewaathiri kwa kuwa wengi wao wamechukua mikopo na kila siku wanapaswa kurejesha mikopo.

"Kuna watu tulikuwa na mahindi ambayo ni mabichi hayajakauka na hapa tuko kwa siku nne fikiria hapa ni namna gani ambavyo watu watapata hasara, hapa mahindi yameshaanza kuharibika maana yalikuwa na baridi, kwa hiyo zuio hili la mahindi limetupa hasara kubwa mpaka sasa,"

"Magari yamerundikana hapa mpakani kwa kuwa kuna zuio la mahindi kutovuka mpaka kwenda upande wa pili, tunaomba serikali iangalie jambo hili maana wafanyabishara tunazidi kupata hasara na tunaumia, wengi wetu tuna mikopo hapa na hizi siku tumekaa hapa hatujui tunarejeshaje,"

Mfanyabishara mwingine wa mahindi, Twamsifu Kiangi, ambaye mahindi yake yalikwama katika mpaka huo amesema mpaka sasa hajaweza kuuza mahindi yake zaidi ya magunia 360 kutokana na zuio hilo.

"Kuzuiwa kwa mahindi kumetupa hasara kubwa kwasababu mahindi haya yanapokaa kwa muda mrefu na yana hali ya ubichi ni hasara kwetu, unakuta mtu umechukua mkopo na unatakiwa kurejesha kila siku, sasa hapa unarejeshaje wakati mzigo hautoki na mzunguko wa fedha umekwama, hapa nilipo nina gunia zaidi ya 360 na zilikuwa hazijavuka na mpaka sasa sijaweza kuuza mahindi yangu,"

Akizungumzia adha ambayo wamekumbana nayo baada ya kusitisha mahindi kupita katika mpaka huo, Makamu Mwenyekiti wa soko hilo, Zuberi Shango amemtaka Waziri Bashe kuingilia katiĀ  kwa kuwa hali hiyo inawaumiza wakulima pamoja na wafanyabaishara wa bidhaa hiyo ya mahindi.

"Kila siku Waziri Bashe unapotetea wakulima tunakusikia sana, lakini kuna vitu vinatokea hatuvielewi kwasababu leo wakulima wameleta mahindi hapa yako kwenye magari lakini ya mezuiwa kwenda Kenya na leo ni siku ya nne," amesema na kuongeza;

"Zuio hili la mahindi hatujui limetoka wapi na watu hawalifahamu maana watu wamelipa ushuru, baada ya kukaa hapa kwa siku nne tumeenda ofisi za Forodha wanatuambia wametupa wiki mbili tuvushe magari yetu lakini tunataka kujua mahindi yanashida gani watufahamishe maana sisi ndio tunaolipa ushuru"

"Tunamwomba Waziri Bashe aliweke hili jambo sawa maana alisema hatafunga mipaka na sisi tumechukua hii kauli kama bango letu, sasa hatuelewi ni nini kimetokea,"