Mama Mongella: Mwanamke asipewe uongozi kwa kigezo cha jinsia

Rais mstaafu wa Bunge la Afrika na mwanaharakati wa masuala ya wanawake duniani, Getrude Mongella

Muktasari:

Mwanasiasa huyo mkongwe,  mwanadiplomasia na mwanaharakati katika ukombozi wa mwanamke duniani, amesema marekebisho yanayofanyika kisheria Tanzania yasiweke msingi wa kumwezesha mwanamke bila kuzingatia uwezo wake.


Kelvin Matandiko, Mwananchi

Dar es Salaam. Gertrude Mongella, mwanasiasa, mwanadiplomasia na mwanaharakati katika ukombozi wa mwanamke duniani, amesema marekebisho yanayofanyika kisheria yasiweke msingi wa kuwezesha mwanamke bila kuzingatia uwezo wake, kwani “uongozi sio hisani.”

Mama Mongella ametoa kauli hiyo leo Januari 6, 2024 wakati wa mjadala ulioandaliwa na Jukwaa la Tanzania Connection kupitia mtandao wa Zoom, ukihusisha mjadala wa kitaifa kuhusu utoaji maoni ya miswada ya sheria ya uchaguzi, vyama vya siasa na tume ya taifa ya uchaguzi.

Amesema wakati wa mapambano ya kuimarisha usawa wa kijinsia duniani, wanawake walikubaliana kushinikiza usawa kwa lengo la kuionyesha dunia mabadiliko ya kiuongozi chini ya mwanamke bila kutumia rushwa wala shinikizo la upendeleo.

“Tuangalie umuhimu wa nafasi ya mwanamke bila kuhusisha rushwa. Sisi tulisimama kwa uwezo, tusivunje utaratibu.Lazima mwanamke awe na uwezo wa kuongoza, asiingie kwa sababu ni mwanamke, au rafiki, ndugu wa fulani. Itavunja nguvu ya kutafuta usawa,”amesema Mama Mongella.

Mama Mongella aliyepongeza juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika mageuzi hayo, ametaja maeneo mengine ya kutazamwa ikiwamo kipengele cha kufuatilia utekelezaji wa mikakati ya viongozi na kwamba asiyetekeleza mkakati wake asipewe nafasi tena ya kuongoza.

Mengine alitaja ni  kuzingatia umuhimu wa utashi wa kisiasa kwa viongozi wa ngazi za chini badala ya kubakia ngazi za juu pekee.

“Kuhusu tunu za Taifa, amani na umoja, zitakuwa imara kama kutakuwa na amani na umoja kwa wanawake na wanaume wote,” amesema.