Mama Sauli asimulia alivyowasiliana na mwanawe kabla ya ajali
Muktasari:
- Katika ajali, Sauli alikuwa na mtoto wake wa kiume wa miaka mitatu aliyejeruhiwa na anaendelea kupatiwa matibabu
Chunya. “Aliniambia anikute hapa,” ni kauli ya Hilda Mwasenga, mama mzazi wa aliyekuwa mmiliki wa Kampuni ya Mabasi ya Sauli, Solomon Mwalabila akielezea namna alivyowasiliana na mwanawe kabla ya ajali ya Agosti 4, 2024 eneo la Mlandizi mkoani Pwani.
Mwalabila maarufu Sauli ambaye ni mtoto wa tano katika famili yao, alifariki dunia baada ya gari alilokuwa akiliendesha kugongwa na lori lililokuwa limebeba mchanga.
Hata hivyo, katika ajali hiyo, alikuwa na mtoto wake wa miaka mitatu na nusu (Adrich Solomon) aliyejeruhiwa na anaendelea kupatiwa matibabu.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Agosti 7, 2024, mama mzazi wa Sauli, amesema kabla hajaanza safari ya kuelekea Dar es Salaam akitokea Chunya, Sauli alimuaga akimuomba asiondoke nyumbani kwake Chunya kwenda Kijiji cha Godima anakoishi mpaka atakaporejea.
Amesema alimwambia mambo anayoenda kuyafanya angekaa kwa siku chache huku akimtaka kubaki nyumbani hapo kutokana na afya yake.
"Mimi naumwa, ila aliniambia nisiondoke hapa nimsubiri aje, ndiye alikuwa ananiuguza, nashindwa nielezeeje, niliambiwa amekufa kwa ajali ila mtoto ameumia, sasa sijui ni kama nimechanganyikiwa," amesema Hilda.
Naye mke wake, Evaline Bahati amesema pamoja na maumivu ya kumpoteza mume wake, lakini haelewi namna mtoto alivyonusurika na kwamba, itakuwa historia kwa maisha yake.
Amesema mara ya mwisho kuwasiliana na mumewe alimuambia amepanga kusafiri kwenda Dar es Salaam kushughulikia baadhi ya mambo yake ya biashara.
"Nashindwa cha kuzungumza, naumia sana, nashukuru Mungu kwa yote huyu mtoto imekuwa muujiza tu kupona kwake, ukiitazama ile gari, hii ni historia maishani mwake, baadhi ya mambo kushughulikia kumbe ndiyo kifo,” amesimulia mkewe huku akibubujikwa machozi.
Mwili wa Sauli unazikwa leo nyumbani kwao Kijiji cha Godima saa 11 jioni, huku ikitanguliwa shughuli za ibada na salamu za rambirambi kutoka kwa viongozi na wadau mbalimbali.
Mpaka muda huu, baadhi ya wageni kutoka maeneo mbalimbali wameanza kufika nyumbani kwa marehemu huku vilio na simanzi vikitanda na kila mmoja anamuelezea Sauli namna alivyoishi naye.