Mama Shamsudini akamatwa akituhumiwa kumuua mwanaye kwa moto
Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro Simon Maigwa akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, limemkamata Semen Feruz Alfan (45), mkazi wa Reli Juu, Wilaya ya Mwanga, mkoani humo, kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mwanaye Shamsudini Jamadu Msemo (13).
Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, limemkamata Semen Feruz Alfan (45), mkazi wa Reli Juu, Wilaya ya Mwanga, mkoani humo, kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mwanaye Shamsudini Jamadu Msemo (13), ni baada ya kudaiwa kujificha kwa zaidi ya siku 50.
Shamsudini alifariki dunia Oktoba 3, mwaka huu wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), baada ya kupata majeraha ambayo yanadaiwa kusababishwa na mama yake mzazi, kwa kumchoma moto.
Inadaiwa kuwa, Agosti 31, 2023; baada ya mama yake kumtuhumu mwanaye huyo kuchukua fedha Sh20, 000; kisha kununua chips pale alipohisi njaa.
Inadaiwa kitendo hicho kimgadhibisha mama huyo ambapo inadaiwa kuwa alimfunga mikono na miguu kwenye mti ambao upo nyumbani hapo, baadaye inadaiwa kuwa mama huyo alimwagiza mtoto wa jirani kwenda kumnunulia mafuta ya taa.
Baada ya mafuta hayo kuletwa, inadaiwa kuwa mama huyo alimwagia mafuta hayo mtoto wake (Shamsudini), kisha kumchoma moto.
Hata hivyo, baada ya mtoto huyo kufikishwa KCMC kwa ajili ya matibabu, wataalam wa majanga ya moto hospitalini hapo walibaini kuwa, mwili wa mtoto huyo ulikuwa umeungua kwa asimilia 65.
Akizungumzia kukamatwa kwa mwanamke huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema baada ya mama huyo kudaiwa kufanya ukatili huo, alitokomea kusikojulikana mpaka alipokamatwa Ifakara, mkoani Morogoro alikokuwa amejificha.
"Tumefanikiwa kumkamata mwanamke mmoja aitwaye Semeni Feruzi Alfan, (45) mkazi wa Kitongoji cha Reli Juu, Wilaya ya Mwanga; kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mwanae wa kumzaa aitwaye Shamsidin Jamadu Msemo (13),” amesema RPC huyo na kuongeza;
“...kwa kumwagia mafuta ya taa na kumchoma moto huku akiwa amemfunga kamba na kusababisha majeraha makubwa yaliyopelekea kifo chake wakati akiendelea na matibabu katika hospitali ya Rufaa KCMC Moshi Oktoba 03, 2023."
Kamnada Maigwa ameongeza kusema: "Tukio hilo lilitokea Agosti, 31, 2023 majira ya 11:00 jioni nyumbani kwa mtuhumiwa ambapo kijana huyo ambaye kwa sasa ni marehemu alituhumiwa kuchukua Sh20, 000 kisha kwenda kununua chips bila ruhusa ya mama yake.”
Bosi huyo wa Polisi mkoani humo amesema kuwa baada ya juhudi za muda mrefu za kumtafuta mtuhumiwa huyo, huku likishirikiana na wananchi wema, lilifanikiwa kumkamata mama huyo huko Ifakara mkoani Morogoro ambako inadaiwa alikwenda kujificha.