Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Baba adaiwa kumuua, kumzika mwanaye wa miaka 5 porini

Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita Safia Jongo Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Muktasari:

  • Elias Bukumie (32) Mkazi wa Kijiji cha Chikobe, Kata ya Butundwe, Wilaya ya Geita anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kumuua mtoto wake mwenye umri wa miaka mitano ambaye ni mlemavu wa viungo.

Geita. Mtoto Dickson Elias (5) mkazi wa Chikobe, Kata ya Butundwe, Wilaya ya Geita mwenye ulemavu wa viungo ameuawa na baba yake mzazi kisha kumzika porini kwa madai ya kushindwa kuendelea kumlea baada ya mama mzazi wa mtoto huyo kurudi kwao.

Kufuatia mauaji hayo Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia Elias Bukumie (32) ambaye ni baba mzazi wa mtoto huyo kwa tuhuma za mauaji.

Akielezea tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Safia Jongo amesema mwili wa mtoto huyo ulionekana porini na wasamaria wema.

“Wasamaria wema wakiwa porini, waliona mwili wa mtoto wa miaka mitano. Taarifa za awali zilisema amechunwa ngozi na kukatwa ulimi. Timu yetu ya upelelezi ilikwenda hadi Kijiji cha Chikobe na kuukuta mwili wa mtoto ambaye inaonekana alikuwa mlemavu wa viungo,”amesema Kamanda Jongo.

Amesema operesheni iliyofanywa na jeshi hilo, ilifanikisha kumkamata baba wa mtoto huyo na kwenye mahojiano alikiri kumuua mwanaye akidai alishindwa kuendelea kumlea mwenyewe baada ya mke wake kumkimbia.

“Huyu baba amedai alikuwa akiishi na mkewe na mwezi mmoja uliopita, mkewe alimuacha akarudi kwa wazazi wake, hivyo aliendelea kuishi na mwanaye. Alipoona anashindwa kuendelea kumlea, alimbeba na kumpeleka kwa mkewe ambaye alikuwa kwa wazazi wake na alipofika wazazi wa mwanamke walikataa kumpokea mtoto na kumtaka arudi naye kwa kuwa ni damu yake,”amesema Kamanda huyo.

 Kamanda Jongo amedai mtuhumiwa huyo alipofika eneo la pori katika kijiji hicho aliamua kumbana pumzi kisha kufariki dunia na kuamua kumfukia hukohuko porini.

“Alimfukia porini na kama mnavyojua mji wetu una wanyama, alikutwa akiwa amefukuliwa na wanyama ambao waliuvuta mwili na ndio maana ngozi yake inaonyesha kama imechunwa. Ulipofanyiwa uchunguzi, unaonyesha umenyofolewa na wanyama na siyo kuchunwa na hata ulimi uliosemekana haupo tumeukuta upo,” amesema.

Kamanda Jongo amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa na taratibu za kisheria zinaendelea ili aweze kupandishwa mahakamani.

Hata hivyo ameitaka jamii kutoa taarifa Polisi pale wanapobaini ukatili dhidi ya watoto.

Mchungaji wa Kanisa la AIC Geita, John Marco amesema matukio ya ukatili yanayotokea mara kwa mara mkoani humo yanachangiwa na jamii kuwa na mmononyoko wa maadili na watu kukosa hofu ya Mungu.

“Kwa hali ilivyo sasa viongozi wa dini wanapaswa sasa kurudi na kuwatengeneza watu kiroho ili kuponya mioyo. Viongozi wa dini tukishindwa kutibu mioyo, hata Serikali haitaweza kwa sababu matatizo haya yanaanzia moyoni lazima tutibu mioyo kwanza ili watu warudi kwenye maadili mema.