Mambo matano yanayombeba Rais Samia madarakani

Thursday July 08 2021
samiapic

Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan

By Jesse Mikofu

Wakati Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan ameshatimiza miezi mitatu akiwa madarakani, wachambuzi wa masuala ya diplomasia, siasa uchumi na wananchi wa kawaida wamesema ndani ya kipindi hicho yapo mengi ya kuigwa ambayo ameyafanya.

Katika kipindi hicho ametajwa kufanya mambo mbalimbali ya kiuhusiano, ushirikiano, umoja na utulivu, diplomasia, biashara na uchumi, muungano na kuteua na kutengua baadhi ya watumishi katika nafasi za kisiasa na kiutendaji.

Rais huyo ambaye aliapishwa Machi 19 mwaka huu, tangu ashike nafasi hiyo ya juu kabisa kitaifa, mbali ya kuteua viongozi katika kada tofauti, lakini wapo pia aliowafyeka na kuwaweka pembeni.

Hata hivyo, tofauti na ilivyo kwa mtangulizi wake, Rais John Magufuli ambaye kwa kiasi kikubwa alikuwa akitaja sababu za kutengua uteuzi, Samia anatengua kimyakimya.

Hivi karibuni Mwananchi lilifanya mazungumzo na baadhi ya watu ili kujua wanavyoutazama uongozi wa Rais Samia.

Miongoni mwao ni Mtafiti na mchambuzi kutoka ofisi ya Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar, Mohamed Mansour.

Advertisement

Anasema Rais ameonyesha weledi mkubwa katika utendaji wake kwa siku chache.

“Ndani ya muda mfupi tangu aape kuwa Rais wa Tanzania, tayari amejipambanua na sasa tunafahamu si mtu wa kuchezewa, anachotaka ni kazi, watu wafanye kazi,” anasema Mansour.

Kiongozi huyo akizungumzia suala la uteuzi, anasema Rais Samia amepanga safu yake anayoamini inakwenda kumsaidia na amelifanya hilo bila kukurupuka.

Rais Samia alianza kwa kumteua Dk Philip Mpango kuwa Makamu wa Rais, mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya. Lakini pia amefanya uteuzi wa watendaji wa taasisi mbalimbali.

Anasema licha ya weledi huo, lakini pia aina ya uongozi anaoenda nao, akitolea mfano kwamba katika uongozi kuna watu wa pwani na bara, lakini staili yake ni ya watu wa Pwani.

Kuunganisha wananchi

Suala la kuwaunganisha wananchi nalo linaonekana kumbeba Rais Samia katika hatua hizi za mwanzo “kuanzia alipoachia mtangulizi wake, alijitahidi sana, amekuwa akisisitiza hoja na ushirikiano ulinzi na usalama, amani na utulivu ambavyo ni muhimu sana.”

Rais Samia amekuwa akitumia utaratibu wa kukutana na Watanzania kupitia makundi mbalimbali, yakiwamo ya wazee, wanawake, vijana, wafanyabiashara, viongozi wa dini na hivi karibuni alikutana na kuzungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.

Akilizungumzia hilo, Mansour anasema Rais analenga kuimarisha umoja na mshikamano sambamba na kusikiliza changamoto na kuzipatia majibu yake kwa kutoa maelekezo ya moja kwa moja kwa wateule wake wayafanyie kazi.

Kiuchumi

Mansour ambaye pia ni mtaalamu wa uchumi, anasema kiongozi huyo amejitahidi kushirikiana kwa karibu na wafanyabiashara.

Wakati anamwapisha Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Rais Samia alimwagiza kwa kushirikiana na waziri wa biashara na viwanda kushughulikia changamoto za wafanyabiashara.

“Unaweza kuona jinsi gani sasa hivi vikwazo vya kibiashara na wawekezaji, masuala ya fedha yanavyokwenda haraka katika maeneo hayo,” anasema.

Diplomasia

Mchambuzi huyo anasema jambo ambalo lina maana kubwa na pengine halionekani moja kwa moja kwa wananchi wengi, ni suala la kushughulikia diplomasia.

“Naweza kusema amekuwa international, yaani amekuwa mtu wa kimataifa hivi, alipoingia madarakani tu aliianza kuibeba agenda ya diplomasia kwa kuiweka mbele,” anasema Mansour.

Ametolea mfano pale alipokwenda ziara ya kikazi nchini Uganda na baada ya kurejea nchini, Rais Samia alimpokea Balozi Amina Mohamed kutoka Kenya na baadaye akaenda Kenya.

“Huko alitoa hotuba iliyosheheni masuala ya uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili ambayo hiyo ni diplomasia ya uchumi,” anasema.

Ukiachilia kwenda huko, lakini kuna viongozi mbalimbali ambao wameshakuja kumsalimia na kuzungumza naye ambao mtaalamu huyo anasema ni kiashiria cha kuimarisha uhusiano mwema na diplomasia ya uchumi nchini.

Mbali na yeye Rais Samia, lakini mawaziri wa wizara ya mambo ya nje wamekuwa wakikutana na wageni na mawaziri wenzao kuzungumza masula hayohayo.

“Kwa hiyo katika diplomasia amejikita kutengeneza na kuimarisha uhusiano na kutoa maelekezo, kushikilia hilo sio suala dogo kabisa.”

Akiendelea kumchambua katika suala hilo, mchambuzi huyo wa diplomasia anasema katika masuala ya vikao vya ulinzi na usalama amekuwa akimtuma Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akamwakilishe kutokana na uzoefu alionao wa kuwa waziri wa ulinzi kwa miaka mingi.

Muungano

Suala lingine ambalo ameshikilia anasema ni kuhakikisha Muungano unadumu, hata Mapinduzi matukufu ya Zanzibar anayasapoti na yanalindwa sambamba na muungano, vikao vinafanywa kila mara vya mawaziri wanaohusika na watendaji wake.

Dk Mpango ameshakwenda kukutana na Rais Mwinyi kwa ajili ya kuratibu mambo mbalimbali katika kuimarisha muungano, wakati naye akihimiza wizara akitaka iendelee kufanya kazi kwa weledi na mambo ya changamoto yakishughulikiwa kwa haraka zaidi.

Wananchi wanavyozungumza

Khalid Said Sued, mkazi wa Mazizini mjini Unguja anasema ndani ya kipindi hiki taifa limeshuhudia mabadiliko makubwa ya kiutendaji na kiuongozi, hivyo wanategemea kuendelea kuona mabadiliko makubwa katika utawala wake.

Alisema wanaona jitihada mbalimbali zinazochukuliwa kuimarisha Muungano ambao uliasisiwa na viongozi wa mataifa hayo mawili, Abeid Amani Karume na Julius Nyerere mwaka 1964.

“Tumeshuhudia kwa kipindi hiki kifupi wakija wataalamu mbalimbali kutoka bara na kuweka vikao hapa Zanzibar kwa ajili ya kutatua kero hizo, kwa hiyo hizi ni jitihada kubwa tunazoona zinafanyika maana yapo mambo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kwa muda mrefu.

Mbali na hilo, Khalid anasema pia katika masuala ya uteuzi amekuwa akichanganya kutoka pande zote mbili za muungano hivyo linawapa faraja.

Naye Zuena Nassor Mohamed, mkazi wa Kiembe Samaki yeye anasema kwamba hata wao wanajiona kama ni viongozi kwa sababu ya kuwa na kiongozi huyo wa kitaifa na kwamba amekuwa akiteua nafasi pia kwa wanawake, jambo linalothibitisha utendaji kazi wao.

“Sawa ile asilimia ya 50 kwa 50 bado haijafikiwa, ila naamini kwa kasi hii na jinsi mama anayokwenda nayo tutaweza kufikia, wanawake tunaweza ila sema tu wakati mwingine tunadharaulika kwa sababu tu ya kimaumbile na tamaduni, kwa kweli mimi hili naona mama kaliweza kwa kiasi kikubwa.

Lakini kwa upande wa Muungano pande zote mbili zitegemee changamoto zote kutatuliwa kwa haraka zaidi, hata Dk Mwinyi amekuwa akisema zinaibuka lakini zinatatuliwa.

Ushauri

Hata hivyo, Mansour anasema bado ipo miradi ya kimkakati ambayo haiwezi kwisha haraka kwa sasa mpaka kuwapo na uratibu maalumu, huku akiwataka wananchi kwanza wajikite kuendeleza amani, mshikamano na utulivu.

Kwenye masuala ya diplomasia, anasema wategemee uhusiano utaimarika na fursa nyingi zitaendelea kutokea katika uchumi ili watu waweze kufanya biashara na mataifa yale yaungane zaidi na sisi ili fursa za uchumi na uwekezaji zitokee tuweze kuuza mazao yetu huko nje.

Lakini viongozi waliochaguliwa na kuteuliwa wawajibike, akitolea mfano ambao wamejaribu kutingisha usawa wa mama wamewajibishwa, kwa hiyo wafanye kazi.

Advertisement