Maofisa usafirishaji, madereva wa Serikali wafundwa kuhusu wajibu

Baadhi ya Maafisa uendeshaji na madereva wa Serikali, mamlaka za halmashauri, mashirika na taasisi za umma kutoka mikoa ya Kanda ya Magharibi inayoundwa na Kigoma, Tabora na Katavi wakifuatilia mada wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kutambua majukumu na kutimiza wajibu wao katika utunzaji na ulinzi wa magari ya umma. Mafunzo hayo yanatolewa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT). Picha na Robert Kakwesi 

Muktasari:

Maafisa Usafirishaji na Madereva wa Serikali, mamlaka za halmashauri, mashirika na taasisi za Umma wametakiwa kutambua wajibu na kutekeleza dhamana ya ulinzi na matumizi mazuri ya magari wanayokabidhiwa kuokoa fedha za umma.

Tabora. Maafisa Uendeshaji na Madereva wa Serikali, mamlaka za halmashauri, mashirika na taasisi za Umma wametakiwa kutambua wajibu na kutekeleza dhamana ya ulinzi na matumizi mazuri ya magari wanayokabidhiwa kuokoa fedha za umma.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Profesa Zacharia Mganilwa wakati wa hafla ya ufunguzi wa mafunzo kwa maofisa uendeshaji na madereva wakuu wa Serikali, halmashauri, mashirika na taasisi za umma kutoka mikoa ya Kanda ya Magharibi.

Ametaja maeneo yanayohitaji uwajibikaji na usimamizi makini kulinda fedha za umma kuwa ni gharama za matumizi ya mafuta ,vilainishi na matengenezo ya magari ya umma.

“Maofisa uendeshaji na madereva wakitimiza wajibu wao wataokoa mamilioni ya fedha za umma zinazotumika kwenye mafuta, vilainishi na matengenezo ya magari ya umma kwa sababu haya ndiyo maeneo makuu yanayotumia fedha nyingi katika uendeshaji,’’ amesema Profesa Mganilwa

Amesema kwa kutambua umuhimu wa kudhibiti matumizi ya fedha za umma katika maeneo hayo, NIT kwa kushirikiana taasisi nyingine inaendesha mafunzo ya kikanda kwa maofisa uendeshaji na madereva wa Serikali kuwapa elimu ya kujitambua kwa lengo la kuwakumbusha wajibu wao.

"Kupitia mafunzo hayo tunawakumbusha madereva kuwa wanaendesha magari yenye thamani zaidi ya Sh500 milioni; hivyo wanao wajibu wa kuyalinda na kuyatunza kuokoa fedha za umma,"  amesema Profesa Mganilwa.

Amesema NIT imeandaa mtaala mahususi wa mafunzo kwa maafisa uendeshaji na madereva wakuu yatakayofanyika kikanda nchi nzima.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian, Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Simon Chacha amepongeza uamuzi wa NIT wa kuandaa na kuendesha mafunzo hayo akisema itasaidia kuokoa mamilioni ya fedha za umma zinazotumika kwenye mafuta, vilainishi na matengenezo ya magari ya Serikali.

‘’Uelewa wa madereva kuhusu utunzaji wa mali ikiwemo magari ya umma utaokoa mamilioni ya fedha za umma. Hii inatokana na baadhi ya madereva kutozingatia umuhimu wa kutunza magari wanayokabidhiwa ndio maana magari wanayokabidhiwa yanaharibika ndani ya muda mfupi,’’ amesema Dk Burian kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake

Mkuu huyo wa mkoa amewataka maofisa usafirishaji kufuatilia na kutambua tabia ya madereva wanaowasimamia kama sehemu ya wajibu wa kulinda magari ya Serikali waliyopewa dhamana ya kuyasimamia.

‘’Naamini mafunzo haya kwa maofisha uendeshaji na madereva wakuu wa Serikali itasaidia kutatua tatizo la uharibifu wa magari na matumizi yaliyopitiliza ya mafuta, vilainisha na gharama ya matengenezo,’’ amesema mkuu huyo wa mkoa

Mafunzo hayo ya siku tano yanahudhuriwa na maafisa usafirishaji na madereva wakuu wa Serikali, mamlaka za halmashauri, mashirika na taasisi za uma kutoka mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora.