Mapendekezo manne muswada bima ya afya kwa wote

Msemaji wa sekta ya uwezekezaji, mashirika ya umma na hifadhi ya jamii, Mwanaisha Mndeme (kushoto).Kulia ni msemaji wa sekta ya afya Ruqayya Nassir.
Muktasari:
- Wakati Kamati ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii ikitarajia kupokea maoni ya wadau kuhusu muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote, Chama cha ACT- Wazalendo kimetoa mapendekezo manne yanayopaswa kufanyiwa kazi ili mfuko huo uwe na tija kwa wananchi.
Dar es Salaam.Wakati Kamati ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii ikitarajia kupokea maoni ya wadau kuhusu muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote, Chama cha ACT- Wazalendo kimetoa mapendekezo manne yanayopaswa kufanyiwa kazi ili mfuko huo uwe na tija kwa wananchi.
Tayari miswada minne ya sheria imesomwa bungeni ikiwemo muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote na kamati hiyo imewaalika wadau wa sekta ya afya kuanza kutoa maoni ifikapo Octoba 19 mwaka huu.
Akizungumza leo Jumapili Oktoba 9, 2022 Msemaji wa Sekta ya Uwekezaji, Mashirika ya Umma na Hifadhi ya Jamii wa chama hicho, Mwanaisha Mndeme amesema chama hicho, kinapendekeza Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) isimamie na kudhibiti skimu ya bima ya afya badala ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (Tira).
“Mtu yeyote ambaye ni mnufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ( Tasaf ), alipiwe mchango wake kwa Hifadhi ya Jamii na Serikali moja kwa moja kwenye NSSF ( Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii ) kwa asilimia 100.
"Hata hivyo Mfuko wa Hifadhi ya Jamii uanzishe fao maalumu la kuwawezesha kuzalisha kipato ili kufikia kundi la kuchangiwa theluthi tu,”amesema Mndeme.
Mndeme ambaye ni Katibu wa Ngome ya Vijana ya ACT- Wazalendo, amesema pendekezo jingine ni kila mwananchi mwenye ajira rasmi na kukatwa michango ya hifadhi ya jamii apate fao la matibabu.
Pia, kimependekeza kila mwananchi aliyejiajiri kwenye sekta ya kilimo, biashara au shughuli nyingine yeyote na ni manachama wa wa hiari katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii anayechangia kwa kiwango cha chini cha Sh30,000 kwa mwezi achangiwe na Serikali theluthi moja kila mwezi
“Hii itakuwa kivutio kwa watu walio kwenye sekta isiyo rasmi kujiunga kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Bima ya afya,”amesema Mndeme.
Wakati Mndeme akieleza naibu msemaji wa sekta ya afya wa ACT- Wazalendo, Ruqayya Nassir amesema chama hicho, hakikubaliana na muswada huo, kwa madai ya kwamba haujalenga wala kukidhi mahitaji ya kumkomboa Mtanzania katika suala la afya.
" Tutakwenda Dodoma kuyafikisha maoni haya tuliotoa hapa na mengine tutakayoyakusanya kwa wananchi.Tutaiambia Serikali kwa nini hatukubaliani na muswada na mapendekezo yetu ili kuleta ahueni kwa wananchi kuhusu sekta ya afya,"amesema Ruqayya.