Mapya ‘msoto’ kupata uwakili, LST wafunguka

Muktasari:

  • Baadhi ya wanafunzi wa Shule Kuu ya Sheria Tanzania (LST) waliolazimika kurudia baadhi ya masomo kwa muda mrefu bila mafanikio, wametoa shuhuda zao huku wakiibua mambo mazito kuhusiana na matokeo chuoni hapo.


Dar es Salaam. Baadhi ya wanafunzi wa Shule Kuu ya Sheria Tanzania (LST) waliolazimika kurudia baadhi ya masomo kwa muda mrefu bila mafanikio, wametoa shuhuda zao huku wakiibua mambo mazito kuhusiana na matokeo chuoni hapo.

Wametoa shuhuda hizo kutokana na matokeo ya mitihani yao iliyotoka mwishoni mwa wiki ililopita yanayoonyesha mamia ya wanafunzi washindwa kuendelea huku wengine wakitakiwa kurudia baadhi ya masomo.

Katika mtihani wa uwakili wa shule hiyo uliofanywa na wanafunzi 633 mwaka huu, kati yao ni 26 pekee ndiyo waliofaulu, 342 walitakiwa kurudia (suplimentary) huku 265 walifeli na kukatishwa masomo (discontinued).

Si jambo jipya katika shule hiyo, kwani katika mwaka wa masomo 2018/2019 kati ya wanafunzi 1,735 ni 347 walifaulu kuendelea, 484 walirudia mitihani na 468 walifeli.

Mwaka 2016/17-2017/18 kati ya wanafunzi 2,662 waliofanya mtihani 445 (sawa na asilimia 16.72) walifaulu, 1,611 (sawa na asilimia 60.53) walirudia na 606 (sawa na asilimia 22.76) walifeli.

Matokeo hayo yameibua mjadala maeneo mbalimbali huku Jaji wa Mahakama Kuu, Gabriel Malata akisema jawabu la changamoto zote zinazoikabili hatua hiyo ya taaluma ya sheria litapatikana iwapo utafanyika utafiti.

Hata hivyo, naibu mkuu wa Taasisi anayeshughulikia mafunzo kwa vitendo, machapisho, utafiti na utaalamu elekezi wa LST, Profesa Zakayo Lukumay akizungumzia madai ya rushwa ya ngono, alisema ni vigumu hilo kutokea kwa kuwa mtihani wa mwanafunzi wa taasisi hiyo hausahihishwi na mtu mmoja.

“Kila swali linasahihishwa na mhadhiri wake, unakuta yapo maswali matatu yanasahihishwa na wahadhiri watatu sasa rushwa utawapa wote?” alihoji.

Kuhusu madai ya wanafunzi kufeli, Profesa Lukumay alisema, “tuzungumze kwa lugha nyepesi, tatizo tunacholetewa hakijaiva (hawajaiva kutokea vyuo vikuu).”

Kwa upande wake, Mwandishi mkongwe nchini, Deogratius Mushi alisema “kuna hoja mawakili wamekuwa wengi Tanzania kwa sasa, lakini si kweli. Kuna mawakili vijana wengi wapo nyumbani kwa wazazi wao hapa Dar, lakini huko mikoani na wilayani hakuna mawakili.”

Katibu mtendaji mMwanzilishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Anthony Ngaiza alisema, “tatizo halitokani na wahitimu wa vyuo vikuu kutokaa kwenye ‘law firms’ kwa muda mrefu.”

Ngaiza alisema tatizo ni ubora wa wahitimu, “hawana uelewa unaotakiwa kwa wanasheria. Hawana viwango stahiki vya lugha ya Kiingereza kuweza kumudu. Hata walimu wao wakiwa wazuri namna gani (ingawa naamini asilimia zaidi ya 50 ya walimu wao nao hawana ubora unaotakiwa.”

…arudia mara 13

Lusajo Mwakasege, mmoja wa wanafunzi waliofeli ambaye yuko chuoni hapo kwa mwaka wa tano sasa kwa ajili ya somo moja ambalo hata katika matokeo ya mwaka huu hajafaulu, alisema sasa anakusudia kuandika barua apewe nyaraka zinazomwezesha kuhakiki alama zake kisha akate rufaa na kama atanyimwa atakwenda mahakamani kuiomba mahakama iulazimishe uongozi wa chuo kumwezesha kuhakiki matokeo yake.

Akizungumza na Mwananchi, Mwakasege alisema alijiunga na chuo hicho Machi, 2016 akamaliza 2017, lakini matokeo yalipotoka akatakiwa kurudia masomo manane.

“Kila mwaka nimekuwa nafanya mitihani na nimekuwa napunguza kidogokidogo, lakini nyingine zimekuwa hazipunguziki. Kwa mwaka tunafanya mitihani mara mbili, hivyo mpaka sasa nina miaka mitano na nimeshafanya supp (nimesharudia) mara 13, lakini sijafaulu, kipengele kimoja cha somo moja.

Hata hivyo, alisema alipoona mambo yamezidi kuwa magumu mwaka 2019 alikata rufaa na akafanikiwa kufaulu somo moja, lakini akasema kuwa rufaa pale chuoni ni jambo linaloogopesha sana.

“Inasemekana ukikata rufaa wanakukariri ndo hutakuja kufaulu tena,” alisema Mwakasege.

Mwakasege alisema kuna kila dalili za kuamini wanafunzi wengi wanashindwa kwa mipango na kwamba lengo ni kuwafanya waendelee kuwepo na hivyo kuwa kama sehemu ya kitega uchumi cha chuo. Kurudia kipengele kimoja cha somo ni Sh30,000.

Aliongeza sababu nyingine inayoashiria wanafunzi wafanywa kurudia mitihani kwa makusudi ni kitendo cha kunyimwa alama wanazopata, ili wajumlishe na kujiridhisha kuwa wamepata daraja stahili.

Mwanafunzi mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema amesharudia mitihani hiyo kwa miaka saba sasa na amesharudia kipengele kimoja kwa zaidi ya mara 10, lakini bado hajafaulu.

“Mpaka juzi nilikuwa napiga mahesabu kwamba nikate rufaa au nifanyeje, lakini sasa ukishakata rufaa unaingia kwenye fitina na watu. Kwanza wananakiri namba yako. Nina ushuhuda na watu kama watano hivi.

“Kuna mtu toka court (intake) ya sita alishakata rufaa, lakini mpaka leo ni court ya 35 bado yupo na anachoshukuru tu ni kwamba amepewa uongozi kwenye sehemu tofauti,” alisema.

Alisema alijiunga na chuo hicho mwaka 2015 baada ya kuuza ng’ombe kijijini kwao, lakini katika mtihani wa kwanza alishindwa masomo yote na akalazimika kuanza upya mwaka uliofuata.

Mwanafunzi huyo alisema chuoni hapo kuna mambo mengi yanaendelea ikiwamo ya rushwa na rushwa ya ngono na kwamba kuna mtu mmoja anamjua alitoa hela na akapita.

“Kwa hiyo vitu vingine hivi ndio maana nimekwambia siwezi kuviongelea sana kwa sababu mwisho wa siku utajikuta unaumia.”

Hoja hiyo imeungwa mkono na Alexander Barunguza ambaye tayari amefungua kesi ya kupinga matokeo yake katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki na nyingine ya kikatiba Mahakama Kuu, Masjala Kuu akipinga kanuni za ukataji rufaa kupinga matokeo, huku akidai haki yake kuelekea kukiukwa kwa kutishiwa maisha na mmoja wa walimu kutokana na hatua yake ya kukata rufaa.