Marais Magufuli, Kagame waomboleza miaka 22 ya mauaji ya kimbari Rwanda

Muktasari:
Watu laki nane waliuawa wengi wakiwa wa Kabila la Watutsi na Wahutu katika machafuko yaliyolitia doa taifa hilo lililopo katika eneo la Maziwa Makuu.
Dar es Salaam. Rwanda inaadhimisha miaka 22 leo tangu kutokea mauaji ya kimbari mwaka 1994, huku taifa hilo likijitokeza katika sura mbili kuhusiana na siasa za kimataifa.
Rwanda ambayo mwishoni mwa mwaka jana ilifanya kura ya maoni ambayo ilimwezesha Rais Paul Kagame kuendelea kuongoza Taifa hilo, ina mengi ya kujifunza.
Maadhimisho hayo yanafanyika wakati hali ya uchumi ikiwa imeimarika. Wananchi wamekuwa chachu ya amani na mshikamano. Pia, kuna maridhiano yanayojitokeza ndani ya mioyo ya Wanyarwanda.
Wengi wanaendelea kusifu utawala wa Rais Paul Kagame, lakini wachache wananung’unika. Wanamtaja Rais Kagame kama mpatanishi aliyefanikiwa kuzika uhasama na chuki. Wanamwona kama mwanasiasa aliyejaa ujasiri wenye kuwatisha wale wanaohubiri chuki
Ingawa baadhi ya wakosoaji wanasema kuwa uchumi wa Rwanda bado umeendelea kuwa kwenye makaratasi, huku wananchi wake wakiwa kwenye maisha ya dhiki lakini taifa hilo limepiga hatua.
Hata hivyo, Rais Kagame aliyetajwa kuwa kipenzi cha nchi za magharibi, sasa anatazamwa kama mwanasiasa kinyonga. Hatua ya kuanzisha mchakato wa marekebisho ya katiba ili aendelee kuwa madarakani, iliibua mvutano ndani na nje ya nchi hiyo.
Nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani na Umoja wa Ulaya zilimkosoa mwanasiasa huyo ambaye huenda akawa miongoni mwa viongozi wachache wa Afrika watakaosalia madarakani kwa kipindi kirefu zaidi.
Hata hivyo, Rais Kagame amezipuuza shutuma hizo na kuwataka wananchi kushikamana ili kuliletea maendeleo taifa lao.
Wengi wanaitaja Rwanda kama taifa lililofanikiwa kuweka bayana dira yake ya maendeleo katika eneo la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Pia, maadhimisho hayo yanatoa picha mbili kuhusu uhusiano wa taifa hilo na majirani zake.
Rwanda bado inajuta kuendelea kuwa na uhusiano tete na jirani yake Burundi.
Kwa miaka kadhaa mataifa hayo yamekuwa na mgogoro kuhusu kile kinachoelezwa ni njama za kila upande kutaka kuvuruga ustawi wa mwenzake.
Rais Kagame amekuwa akijitokeza hadharani mara kwa mara na kukosoa matamshi ya mwenzake, Rais wa Burundi, Pierre Nkuzuriziza anayeituhumu Rwanda kufadhili makundi ya wapiganaji.
Ingawa kila pande umejaribu kujizuia kutoa matamshi makali, lakini bado kuna hali ya wasiwasi.
Burundi imekuwa ikipata nguvu kutoka jumuiya za kimataifa na wakati wote inalitumia nafasi hiyo kujiimarisha kiuchumi na usalama katika mipaka yake.
Ijapokuwa mgogoro wa Burundi unafungamana na mataifa mengine kama Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Uganda, lakini Burundi inaelekeza lawama kwa Rwanda. Umoja wa Mataifa umewahi kuyataja mataifa hayo matatu kuwa sehemu ya wale wanaosambaza silaha kwa makundi ya waasi.
Ingawa mataifa hayo yamekuwa yakikanusha kuhusu taarifa hizo, lakini ripoti ya Umoja wa Mataifa inasisitiza kuwa, waasi wa Burundi wamekuwa wakipata msaada mkubwa kutoka kwa mataifa jirani.
Wakati huu Rwanda inaadhimisha miaka 22 tangu kutokea mauaji hayo, Rais Paul Kagame amefaulu kuchanga vyema karata zake kwa upande wa pili.
Amefanikiwa kutunza ‘tunu’ ya ushirikiano na Tanzania.
Ingawa kwa upande mmoja anaonekana kama kiongozi aliyeshindwa kumaliza mgogoro na jirani yake Burundi, lakini anajitokeza kwenye maadhimisho hayo akiwa amefanikiwa kuimarisha ushirikiano na Tanzania.
Rais John Magufuli ametua Rwanda ikiwa ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu aingie madarakani.
Wachambuzi wa masuala ya kidiplomasia wanasema, ziara ya Rais Magufuli nchini Rwanda ni ishara kwamba wanataka kuimarisha ushirikiano ulioanza kulegalega hapo awali.
Hivi karibuni wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika Mashariki uliofanyika hapa nchini, Rais Kagame alionyesha wazi kuunga mkono sera za Rais Magufuli.
Historia inaonyesha kwamba Tanzania na Rwanda zimewahi kutumbukia kwenye malumbano ya kisiasa na yalimalizwa kwa njia ya mazungumzo.
Kitendo cha rais aliyepita, Jakaya Kikwete kuitaka Rwanda kuzungumza na makundi ya waasi, kilitafsiriwa na utawala wa Rais Kagame kama ‘usaliti wa kimipaka’.
Tangu wakati huo uhusiano wa pande hizo mbili ulitumbukia nyongo kiasi cha hata kuzidisha wasiwasi kwa wananchi wake.
Diplomasia ya kimkakati iliyotekelezwa na viongozi hao ilifanikiwa kuzika tofauti na hatimaye ilishuhudiwa viongozi hao wakiwa katika meza moja.
Jambo la kuvutia zaidi ni pale Wanyarwanda wakiadhimisha miaka 22 ya mauaji ya kimbari huku Rais Kagame akiwa katika meza moja na Rais Magufuli.