Masilahi duni ya walimu yaibua wadau

Muktasari:

  • Wadau wa elimu wamehoji kutoingizwa kwa masilahi ya walimu katika rasimu ya sera ya elimu inayoendelea kujadiliwa, wakitilia shaka ubora wa elimu bila kuwajali walimu.

Dar es Salaam. Mdau wa elimu, mwalimu Peter Kazungu amesema kuna haja ya kuangalia maslahi ya walimu kama kitu muhimu kitakachowezesha kuboresha mfumo wa elimu hapa nchini badala ya kuwekeza kwenye vitu vingine.

Kazungu amebainisha hayo leo Mei 17, 2023 wakati akichokoza mada kwenye mjadala wa Mwananchi Twitter Space uliokuwa ukijadili rasimu ya sera ya elimu na mitalaa ambayo bado inajadiliwa.

Amesema wadau wengi wanazunguka katika kujadili jambo hilo, lakini ukweli ni kwamba ubora wa elimu ni mwalimu, hata ikijengwa miundombinu bora kiasi gani kama hakuna walimu bora ni kazi bure.

“Asilimia zaidi ya 80 ya walimu wa shule za msingi na sekondari hawajitoi zaidi ta asilimia 50 ya uwezo wao kutokana na kutoridhishwa na mazingira ya kazi. Wengi wanafanya kazi kwa sababu hawana kimbilio lingine, mishahara ni midogo kiasi kwamba wanalazimika kuweka nguvu zao kwenye maeneo mengine.

“Hivi inawezekanaje tunakuwa na taifa ambalo posho ya mbunge ya kikao cha siku moja ndiyo mshahara wa mwalimu wa mwaka mzima halafu tunakaa tukisubiri matokeo makubwa kutoka kwa mwalimu,” amesema Kazungu.

Ameongeza kuwa: “Kama tunalipa wabunge milioni 12, hivi kuna dhambi gani kumlipa mwalimu milioni 4. Tunashabikia mitaala na tunasahau kabisa kuhusu mwalimu wakati ubora wa elimu unamtegemea mwalimu.”

Kwa upande wake Mbunge wa viti maalum Nusrat Hanje, ameshangazwa na rasimu ya sera ya elimu kutozingatia masilahi ya walimu.

“Tutakuwa tumefeli sana kama tumetengeneza nyaraka kubwa namna hii halafu watekelezaji ambao ni walimu wakaachwa kando. Ni muhimu walimu wakawezeshwa ili kusimamia kwa ukamilimu utekelezaji wa sera hii,” amesema.