Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maswali kumi kwa Mbunge wangu: AESHI KHALFAN HILALY

Mbunge wa jimbo la Sumbawanga mjini Aeshi Khalfan Hilaly

Muktasari:

Kimsingi wakati naingia madarakani tatizo la madawati lilikuwa kubwa katika shule zetu za msingi lakini kwa kushirikiana na Serikali, tumejitahidi kulipunguza. Tumetumia fedha za mfuko kukabiliana na changamoto hii japo haijaisha kwa asilimia 100 lakini tumepunguza kwa kiasi kikubwa.

Mbunge Aeshi Khalfan Hilaly ni mbunge wa jimbo la Sumbawanga Mjini kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi amezungumza na gazeti la mwananchi na kujibu maswali kumi aliyoulizwa na wananchi wa jimboni kwake

1. Francis Sebastian mkazi wa Sumbawanga Mjini.

Umefanya jitihada gani katika kusaidia kumaliza tatizo la uhaba wa madawati katika shule za msingi kwenye jimbo lako?

Jibu: Kimsingi wakati naingia madarakani tatizo la madawati lilikuwa kubwa katika shule zetu za msingi lakini kwa kushirikiana na Serikali, tumejitahidi kulipunguza. Tumetumia fedha za mfuko kukabiliana na changamoto hii japo haijaisha kwa asilimia 100 lakini tumepunguza kwa kiasi kikubwa.

2. Sebastian Mapula wa Katandala, Sumbawanga Mjini.
Swali kwa nini usiwajibike kwa kulidanyanga Bunge kwa kusema uongo? Ukiwa bungeni ulidai mchakato wa ununuzi wa magari kwa ajili ya kubeba taka ngumu katika Manispaa ya Sumbawanga umekiukwa na kuna ufisadi wa zaidi ya Sh60 milioni, lakini baada ya timu ya wataalamu kutoka Serikali Kuu kufanya uchunguzi wamebaini hakukuwa na ufisadi wowote.

Jibu: Kweli nilipinga mchakato wa ununuzi wa yale magari ya kuzoa taka ngumu kwa kuwa kulikuwa na udanganyifu kile kilichoamuliwa na Baraza la Madiwani kuhusu aina ya magari tuliyotaka yanunuliwe kwa hiyo wataalamu wao wakaone wanunue magari aina nyingine kwa madai ya kuangalia taratibu za ununuzi lakini hata timu iliyotumwa kufanya uchunguzi kuna kitu ilibaini hivyo kuna watu wamewajibishwa na wengine kuhamishwa vituo vya kazi, kwa msingi hiyo sioni sehemu nilipolidanganya Bunge.

3. Mchungaji Moses Siyame wa Kanisa la FPCT, tawi la Majengo Sumbawanga.
Unatusaidiaje kuhakikisha ardhi inarudi mikononi mwa wananchi na vijiji vilivyoporwa na baadhi ya wawekezaji kiasi cha kusababisha migogoro mikubwa hali iliyosababisha baadhi ya watu kupoteza maisha. Kwa mfano, vijiji vinavyozungukwa na shamba la Efatha Ministry lililopo nje kidogo ya mji wa Sumbawanga?

Jibu: Ni kweli lipo tatizo la mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa vijiji saba vinavyozunguka shamba hilo na wamiliki wake ambao ni Efatha Ministry. Mimi nikishirikiana na mwenzangu Ignas Malocha, tumelipigia sana kelele shamba hili bungeni na Serikali imesikia na Rais ametuhakikishia kwamba litarudi mikononi mwa wananchi hivyo wananchi wawe na subira wakati taratibu za kurudisha shamba hilo mikononi mwao zikifanyika.

4. Phabian Masinde, mkazi wa kitongoji cha Bomani mjini Sumbawanga.

Tueleze kuhusu matumizi ya fedha za mfuko wa jimbo maana zinatolewa lakini hatujui matumizi yake ni yapi na kwa miradi ipi.

Jibu: Naomba ieleweke kwamba ipo miradi ambayo iliibuliwa na wananchi ikashindwa kumalizika, sasa basi tumetumia fedha za mfuko wa jimbo kwa ajili ya kukamilisha miradi hii ambayo ni ujenzi wa madarasa, madawati na zahanati. Fedha za mfuko wa jimbo zinajikita kusaidia miradi kama vile ya elimu, afya na maji. Fedha hizi hazitoki kiholela, ipo kamati husika ambayo mbunge ndiye mwenyekiti wake.

5. Arafa Richard Masingo, mkazi wa Kisiwani, Sumbawanga mjini
Katika kipindi chote ulichokuwa madarakani umesaidiaje kupatikana kwa mikopo kwa wanawake na vijana wajasiriamali ili kusaidia kukuza kipato chao na hatimaye kuondokana na umaskini?

Jibu: Kuna mikopo ya aina mbili ambayo nimeitoa binafsi, wa kwanza ulilenga kusaidia vikundi vya vijana na wanawake na kupitia mfuko wa mbunge, nilitoa mikopo ya zaidi ya Sh20 milioni kwa ajili ya kukopesha wajasiriamali wanawake ambazo nyingine marejesho yake hayajafanyika hadi sasa. Pili kuna vikundi vya wakulima tulivikopesha mbolea msimu wa kilimo uliopita yenye thamani ya Sh80 milioni lakini baadhi ya vikundi vimeshindwa kufanya marejesho kutokana na kutouza mazao yao kutokana na kukosa soko, sasa basi hizo ni sehemu ya jitihada zangu za kutaka kumkwamua wananchi wa Jimbo la Sumbawanga Mjini.

6 Mwalimul Essengo Dulla, mkazi wa Kitongoji cha Kristu Mfalme Sumbawanga mjini.

Umefanya jitihada gani kusaidia bei ya pembejeo za kilimo kupungua sokoni na kuhakikisha zinawafikia wakulima kwa wakati tofauti na sasa?

Jibu: Kwanza pembejeo zipo madukani maana yake kwa mkulima mwenye fedha ameweza kuzipata kwa wakati. Ikumbukwe kwamba, msimu huu wa kilimo Serikali imeachana na mpango pembejeo za ruzuku za kilimo kwa mkulima mmoja mmoja kwani utaratibu huo umeonekana haufai. Sasa, wakulima wanaungana katika vikundi (AMCOS) ili wapate pembejeo za kilimo. Vikundi hivyo vinatoa asilimia 20, Serikali inachangia asilimia 20 wanakwenda kupata mkopo kwa mawakala wa pembejeo za kilimo pindi watakapovuna watalipa. Hilo ndilo lililofanyika.

7.Mwalimu Gishi Milundi, mkazi wa kitongoji cha Kantalamba, Sumbawanga mjini.

Sumbawanga ina kero kubwa ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama, kuna jitihada gani za kumaliza kero hii?

Jibu: Maji ni kero kubwa katika mji huu nyakati za kiangazi, lakini Serikali imesikia kilio hiki cha wakazi wa Jimbo la Sumbawanga Mjini na hivi sasa kuna mradi mkubwa ujenzi wa muindombinu ya majisafi na majitaka unatekelezwa katika ambao utagharimu zaidi Sh30 bilioni. Utakapokamilika Mei mwakani, tatizo la maji katika mji wa Sumbawanga litabaki ni historia. Hizi ndizo jitihada zinazofanyika.

8. Mfanyabiashara Rainer Lukara, mkazi wa Kristu mfalme.

Baadhi wananchi wa jimbo lako wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa huduma muhimu katika sekta ya afya, elimu na maji. Umesaidia vipi kutatua changamoto hizi kiasi cha kuwashawishi wakuchague tena kuongoza jimbo kwa kipindi miaka mitano ijayo?

Jibu: Tuanzie kwenye eneo la afya, kimsingi Ilani ya Uchaguzi ya CCM imetekelezwa vizuri eneo hili kwani kila kijiji tumejenga zahanati kwa nguvu ya wananchi na zangu binafsi, huduma zimeboreshwa hospitali ya mkoa tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma, wataalamu wa afya walikuwa wakilalamikiwa kwa kutojali wagonjwa na kuendekeza rushwa lakini sasa huwezi kukuta malalamiko ya aina hiyo. Pia tayari tumetenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya rufaa hii yote ni katika uboreshaji wa huduma ya afya.

Kwa upande wa elimu, shule zote za sekondari Manispaa ya Sumbawanga tumehakikisha maabara zinajengwa na zimefikia hatua za ukamilikaji kwa asilimia 80, binafsi nimechangia mifuko ya saruji 25 na nondo za linta kila shule moja kati ya 15 zilizopo, hivyo sioni sababu ya kutogombea tena wala kuchaguliwa tena kwa kuwa kazi niliyofanya ni kubwa na inaonekana.

9. Augustino Geofrey Mzindakaya.

Ni jambo gani unaloweza kujivunia la kimaendeleo ambalo umelifanya katika uongozi wako, hasa lile linalogusa maisha ya mtu wa kipato cha chini?

Jibu: Yapo mengi ya kujivunia ambayo nimeyafanya katika uongozi wangu kwa wapigakura wa jimbo langu. Kwanza tumeboresha miundombinu ya barabara za mjini nyingi zinapitika kwa muda wote kwa kuwa ni za kiwango cha lami. Umeme siyo kero tena kama ilivyokuwa kabla sijawa mbunge, sasa tuna umeme wa uhakika hapa mjini na sasa unaelekea vijijini. Kuhusu huduma ya majisafi na taka ndiyo kuna mradi mkubwa unatekelezwa kwa hiyo tatizo la maji litakwisha kabisa na hivi vyote vinagusa maisha ya mtu yoyote.

10. Mathew Zacharia, mkazi Jangwangi Sumbawanga. Kuna taarifa kwamba huna mpango wa kugombea tena ubunge katika Jimbo la Sumbawanga lakini badala yake unataka kwenda kugombea ubunge katika Jimbo la Mpanda Magharibi, taarifa hizi zina ukweli kiasi gani?

Jibu: Hizo taarifa za kwamba nataka kwenda kugombea ubunge Jimbo la Mpanda Magharibi si za kweli ni uongo na uzushi mtupu ambao kuna kundi la watu ambao ni maadui zangu kisiasa wanazieneza ili waweze kuniharibia, nitagombea ubunge kwenye Jimbo la Sumbawanga Mjini kwani sioni sababu ya kuliacha kwa kuwa nimefanya vitu vingi vya maendeleo na vinaonekana Sumbawanga hii ni tofauti na miaka mitano iliyopita. Hilo linajionyesha katika sekta ya afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara.