Matatani wakikutwa na magunia ya mirungi

Muktasari:

  • Waliokamatwa ni Abdallah Mohamed (53) na Hamidu Athuman (50) wote wakazi wa kijiji cha Kwadelo wilayani  Kondoa mkoani Dodoma.

Kiteto. Jeshi la Polisi Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, limewakamata watu wawili wakituhumiwa kukutwa na dawa za kulevya aina ya mirungi magunia sita na bunda 300 sawa na kilo 150 wakisafirisha, eneo la kijiji cha Ilkiushbour tarafa ya Makame.

Akizungumza leo Jumatatu Desemba 11,2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, ACP George Katabazi amesema watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa na  bunda 300 sawa na kilo 150 zikiwa zimepakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruser yenye rangi nyeusi.

"Pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa Wilaya ya Hanang katika maafa ya mafuriko, Jeshi la Polisi Manyara bado tunaendelea na msako na operesheni mbalimbali ambapo Desemba 10, 2023 tulikamata watuhumiwa wawili wakisafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi," amesema ACP Katabazi.

Kamanda Katabazi amewataja watuhumiwa Abdala Mohamed (53) na Hamidu Athuman (50) huku akisema walikutwa Kijiji cha Ilikushbour kata ya Makame wakisafirisha kwa gari hilo.


Madhara mirungi

Mwananchi Digital tumezungumza na baadhi ya wananchi kuhusiana na athari za dawa za kulevya kwa jamii.

"Ni kweli vijana wanaathirika na dawa za kulevya, zinaharibu ubongo na wakati mwingine malengo yao yanavurugika," amesema Simon Ibrahimu.

Kwa upande wake, Yona Mahuli amesema: "Nguvu kazi ya Taifa inapotea na watumiaji wengi wa dawa za kulevya, ambao ni vijana  huathirika kiafya," amesema.