Matukio kumi ya uasi wa Mwalimu Nyerere
Muktasari:
Uchambuzi wa Kitabu kipya cha “Development as Rebellion: A biography of Julius Nyerere” umebainisha matukio zaidi ya kumi ya ‘uasi’ katika historia ya maisha ya Mwalimu Julius Nyerere, muasisi wa Taifa la Tanganyika.
Dar es Salaam. Uchambuzi wa Kitabu kipya cha “Development as Rebellion: A biography of Julius Nyerere” umebainisha matukio zaidi ya kumi ya ‘uasi’ katika historia ya maisha ya Mwalimu Julius Nyerere, muasisi wa Taifa la Tanganyika.
Uchambuzi huo umefanyika leo Mei 5, 2022 jijini hapa wakati wa Kongamano la kumbukizi ya miaka 100 ya kuzaliwa Mwalimu Julius Nyerere katika mtazamo wa kiuchumi chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Tasiri ya uasi katika moja ya Juzuu (kitabu) Tatu za kitabu hicho umejikita katika upinzani aliokutana nao ndani na nje ya mfumo dhidi ya imani yake katika usawa, haki na maendeleo.
Profesa Saida Othman, mwandishi wa juzuu hiyo inayohusu maisha yake amesema Mwalimu Nyerere alionekana muasi, akipitia vipindi vigumu hali ambayo ni tofauti na viongozi wa karne hii.
“Hata leo pia tunao waasi wastaafu na waasi watarajiwa, Mwalimu alikuwa na misimamo tofauti katika familia yake, shuleni, kanisani na serikali ya kikoloni,akitaka usawa, haki na maendeleo ya watu,”amesema Profesa Saida.
Aitaja baadhi ya uasi ulioandikwa katika kitabu hicho ni pamoja na uasi wa kujiuzulu mara tatu ikiwamo nafasi ya uwaziri mkuu, uasi wa lugha ya kigeni na kuamini Lugha ya Kiswahili.
Tatu, Mwalimu Nyerere pia aliasi mfumo wa kibepari na kuzindua wazo la Azimio la Arusha huku akiasi mfumo wa Elimu akiamini elimu ya kujitegemea.
Tano, akiwa shuleni aliamua kuwa muasi wa tamaduni za viongozi kukandamiza wanafunzi, kabla ya kuasi mifumo dume iliyokandamiza mwanamke.
“Aliandika kitabu cha kupiga vita mfumo wa kukamdamiza mwanamke lakini hakukitoa kwa sababu ilikuwa ni kutia petroli sana kwa mwanaume kutetea hilo, kwa hiyo tusome hiki kitabu,” amesema.
Profeaa Saida amesema pia alikuwa muasi hata katika mavazi ya suti za kikoloni na kutumia kaunda suti huku akilaani viongozi wa Afrika kuongoza kwa utamaduni wa kutukuzwa.