Mauaji ya askari wa Suma JKT yatikisa Kilimanjaro

Wakazi wa kijiji cha Kiyungi wakiwa wamekusanyika sehemu ambayo askari wa ulinzi wa Suma-JKT aliuawa na mwenzake akiwa lindoni kwenye kituo cha kupoozea umeme wa Tanesco Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro. Picha na Dionis Nyato

Muktasari:

Ni mwendo wa askari kuuana kwa risasi, hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya Askari wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma-JKT), kudaiwa kumuua mwenzake kwa risasi katika wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Moshi. Ni mwendo wa askari kuuana kwa risasi, hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya Askari wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma-JKT), kudaiwa kumuua mwenzake kwa risasi katika wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Amon Kakwale kuthibitisha tukio hilo hazikufanikiwa, baada ya simu yake kupokelewa na msaidizi wake aliyesema kamanda huyo hakuwa tayari kuzungumza kwa wakati huo.

Hata hivyo, Meneja wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Abdulrahman Nyenye alipoulizwa kwa simu alikiri kutokea tukio hilo, lakini akamtaka mwandishi wa habari kumtafuta ofisa uhusiano wake.

Hata hivyo, ofisa huyo alipotafutwa hakupokea simu.

Taarifa ilizozipata Mwananchi zilisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika eneo la Kiyungi linalomilikiwa na Tanesco, baada ya mlinzi mmoja wa Suma JKT kudaiwa kumnyang’anya mwenzake bunduki aina ya Shotgun na kummiminia risasi nne.

Hili ni tukio la pili la askari kuuana kwa kupigana risasi katika kipindi cha takribani siku 20, baada ya askari wa upelelezi wa Jeshi la Polisi wilaya ya Mwanga, Linus Nzema kuuawa usiku wa Mei 31, 2021 na mtu anayedaiwa ni askari mwenzake.

Uchunguzi wa kina wa gazeti hili umebaini tayari askari saba wanashikiliwa na polisi katika vituo mbalimbali vya polisi katika wilaya za Rombo, Moshi na Same, huku gololi tano za bunduki aina ya Shotgun zikidaiwa kupatikana eneo la tukio.

Wananchi walioshuhudia mauaji hayo walidai kumuona polisi mmoja kati ya sita waliokuwapo, akienda kuchukua bunduki chini ya kiti mbele kwa dereva na kumfyatulia risasi ya shingo marehemu na kisha akasema “Nimeua nimeua.”

Tukio la kuuawa kwa polisi huyo lilitokea saa 7 usiku Mei 31, 2021 nje ya baa ya Ndafu Kijiji cha Kituri, muda mfupi kabla ya polisi waliokuwa wamepiga kambi eneo hilo kwa ajili ya operesheni ya kukamata mirungi, walipokuwa wakijiandaa kuondoka.


Tukio la Suma-JKT lilivyokuwa

Taarifa kutoka eneo la tukio zinadai askari wawili wa Suma JKT waliotajwa kuwa ni Emmanuel Mallya na Eric Mollel walikuwa lindo katika kituo cha kupooza umeme cha Kiyungi na katika eneo hilo, askari Emmanuel ndiye aliyekabidhiwa silaha.

Hata hivyo, inadaiwa usiku wa kuamkia leo, wawili hao waliingia katika ugomvi ambao chanzo chake hakijafahamika na inadaiwa askari Mollel alimnyang’anya mwenzake bunduki aina ya Shotgun na kumminia risasi nne.

“Inavyoelezwa kulitokea kutokuelewana baina yao na kulikuwa na dalili zote za purukushani za kunyang’anyana silaha kwa sababu hata shati la marehemu linaonekana kuchanika,” kilieleza chanzo chetu cha kuaminika.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, moja ya risasi hizo ambazo zilimpata marehemu maeneo mbalimbali ya mwili wake iliingia eneo la moyo na kusababisha jeraha lililosababisha kutokwa na damu nyingi hadi kufariki dunia.

Taarifa zaidi zinadai baada ya mauaji hayo, mtuhumiwa aliweka bunduki pembeni ya mwili wa marehemu na kutokomea kusikojulikana na uchunguzi unaendelea, huku mwili wa marehemu ukihifadhiwa hospitali ya mkoa ya Mawenzi.

Mmoja wa mashuhuda katika eneo hilo alidai kusikia milio ya risasi, lakini kwa kuwa eneo hilo lina mazingira ya watu kutolifikia hakuna mtu aliyejua nini kimetokea hadi mpita njia mmoja alipoona mtu amelala kwenye dimbwi la damu.