Mauaji ya mtoto ndani ya hifadhi
Muktasari:
Mtoto mwenye umri wa miaka 17 na mkazi wa kijiji cha Pangaroo mkoani Kilimanjaro, Ngatipa Parmao amefariki dunia akidaiwa kupigwa risasi na askari wa wanyamapori katika Hifadhi ya Mkomazi.
Mwanga. Mtoto mwenye umri wa miaka 17 na mkazi wa kijiji cha Pangaroo mkoani Kilimanjaro, Ngatipa Parmao amefariki dunia akidaiwa kupigwa risasi na askari wa wanyamapori katika Hifadhi ya Mkomazi.
Mtoto huyo jamii ya kifugaji ya Kimasai anadaiwa kupigwa risasi hiyo Julai 6 kwa madai ya kuswaga mifugo ndani ya hifadhi hiyo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za hifadhi.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa wilaya hiyo, Abdallah Mwaipaya alikiri kutokea kwa kifo cha mtoto huyo jana katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya kaskazini (KCMC) alikokimbizwa kwa ajili ya matibabu.
Kutokana na tukio hilo, Mwaipaya alisema Jeshi la Polisi mkoani humo linamshikilia askari huyo kwa uchunguzi, ili kujua hasa ni nini kilichotokea na kusema baada ya hapo taratibu nyingine za kisheria zitachukuliwa.
“Ni kweli tukio limetokea na tumepata taarifa za huyu mtoto kuwa amefariki, lakini taarifa za awali ni kwamba waliingiza ng’ombe kwenye hifadhi, wale askari wakakamta zile ng’ombe na baada ya kumkamata huyu mtoto akawa ameita wenzake.
“Wakaja na masime jambo ambalo liliwafanya wale askari warushe risasi angani kama 15 hivi kutokana na kwamba wale wafugaji walikuwa wanawafuata,” alisema.
Alisema kuwa wanamshikilia askari huyo na uchunguzi unaendelea, ili kujua hasa nini kilichotokea.
“Polisi wakishakamilisha uchunguzi wao taratibu nyingine za kisheria zitachukuliwa,” alisema Mwaipaya.
Kamishna msaidizi wa uhifadhi Mkomazi, Emanuel Moirana alisema baada ya askari hao kukamata mifugo iliyokuwa ikiswagwa ndani ya hifadhi hiyo, wananchi waliwavamia askari hao ambao walikuwa ni watano na kwamba wakati wakijihami walirusha risasi angani kwa kuwa wananchi hao walikuwa wamebeba masime.
“Taarifa nilizonazo ni kwamba askari walikamata mifugo ndani ya hifadhi ndipo wananchi walipovamia na askari wakafyatua risasi ndipo ilipompata huyu mtoto kwa bahati mbaya kwenye zile purukushani.
“Kiutaratibu huwa mtu haruhusiwi kuingiza mifugo ndani ya hifadhi, hivyo mifugo ikikamatwa huwa kuna taratibu zinafanywa lakini hawa wananchi wakawa wamewavamia askari,” alisema Moirana.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Katibu wa chama cha wafugaji wilayani humo, Peter Martine alidai baada ya askari kukamata mifugo hiyo walimtaka mtoto huyo kukabidhi sime na baada ya kukabidhi askari wale wakataka kuondoka na mifugo ile na ndipo palipotokea tukio hilo.
“Jana ng’ombe walikamatwa wakaondoka na nusu ya ng’ombe waliokuwepo, wakawa wananyang’anyana na mchungi ng’ombe ndani ya hifadhi.
“Hawa askari wakawa wanaongea na mchungaji, baada ya muda kidogo wakamtaka atoe sime lake pamoja na simu, vyote akawa ametoa baada ya muda wale askari wakaswaga ng’ombe kuondoka nazo mchungaji kuwakatalia ndipo wakampiga risasi,” alisema Katibu huyo.
Machi 24 mwaka huu, mkazi wa Kibosho Kundi katika Wilaya ya Moshi, Prosper Munish (48) aliuawa kwa kupigwa risasi na mmoja wa maofisa wa wanyamapori akidhaniwa kuwa ni mbwa wanaozurura mitaani.
Mtuhumiwa wa mauaji hayo alitajwa na polisi kuwa ni Honest Ninja (35).
Mei 17 mwaka 2021 katika Wilaya ya Same, Dainess Josephat mkazi wa kijiji cha Mheza alidaiwa kuuawa na askari wa wanyamapori wakati akienda shambani kwake.