Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mavunde aagiza kufuata sheria, kufunga migodi isiyo salama

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akizungunza kwenye kikao kazi cha menejimenti ya Tume ya Madini. Picha na Rajabu Athumani

Muktasari:

  • Mavunde ametoa agizo hilo leo Jumapili Septemba 15, 2024 alipokuwa akizungumza kwenye kikao kazi cha menejimenti ya Tume ya Madini na maofisa wa madini wa mikoa kinachofanyika jijini Tanga

Tanga. Waziri wa Madini Anthony Mavunde amewaagiza maofisa madini nchini kufuata sheria kwa kusimamisha na kufunga migodi isiyo salama kwa wachimbaji.

Mavunde ametoa agizo hilo  leo Jumapili Septemba 15, 2024 alipokuwa akizungumza kwenye kikao kazi cha menejimenti ya Tume ya Madini na maofisa wa madini wa mikoa kinachofanyika jijini Tanga.

Waziri Mavunde amesema uhai wa Mtanzania unapaswa kulindwa kwa njia yoyote ile, kusudi aendelee kuzalisha mali kwa maendeleo yake na ya nchi.

"Msione ugumu kuchukua hatua za kisheria kusimamisha na kufunga migodi kama usalama wa Watanzania hawa wachimbaji upo hatarini, hii ndio changamoto kubwa ambayo tunayo wale wenzetu mtu akishapata mapato leo ukisimamisha hapo wataandamana nchi nzima, lakini ninyi ndio wataalamu, msiongozwe na hisia kwenye hili,” amesema waziri huyo.

Hivyo, amewaambia hawapaswi kuhofia malalamiko au lawama kutoka kwa wamiliki wa migodi kama kuna dalili hasi za kuhatarisha maisha ya watu.

Mavunde amesema sekta ya madini ni muhimu kwa uchumi wa Taifa na ustawi wa wananchi, hivyo amesisitiza kuwa jukumu la msingi ni kuhakikisha usalama wa watu.

Amesema migodi mingi isiyo salama inapotakiwa kufungwa, mara nyingi husababisha maandamano na malalamiko kutoka kwa wachimbaji, lakini akasisitiza wataalamu wanapaswa kuongozwa na sheria badala ya hisia.

Mavunde amesema mwaka wa fedha wa 2023/24, Serikali imekusanya Sh753 bilioni kutoka sekta ya madini na Sh196 bilioni zilikusanywa ndani ya miezi miwili tu ya mwaka mpya wa fedha.

“Hii inaashiria mafanikio makubwa katika usimamizi wa sekta hii,” amesema Waziri Mavunde.

Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Radhamani Lwamo akizungumza katika kikao kazi hicho amesema  wanaendelea kufanya ukaguzi wa migodi na kusimamia masoko ya madini, huku wakitoa elimu kwa wachimbaji kuhusu umuhimu wa usalama kazini.

Amemhakikishia Waziri Mavunde kuwa juhudi hizo zinaendelea ili kuhakikisha wachimbaji wanazingatia taratibu za usalama wanapokuwa kazini.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Buriani amesema mkoa huo una aina mbalimbali za madini, ikiwAmo chokaa, vito na madini ya ujenzi.

“Hii imewezesha mkoa huu kufikia lengo la makusanyo ya asilimia 118 hadi sasa na hivyo kuongeza pato la mkoa,” amesema Buriani.

Amesema mkoa huo tayari una masoko mawili ya madini yanayosaidia wachimbaji kuuza madini yao kwa usalama zaidi, yakiwa yamepangwa Handeni na Kilindi.