Mawakili wa utetezi kesi ya Sabaya wawasilisha pingamizi

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akishuka kwenye gari la Magereza kuingia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

Jopo la mawakili sita wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita wamewasilisha pingamizi mahakamani wakipinga kupokelewa kwa nyaraka nne.

Arusha. Jopo la mawakili sita wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita wamewasilisha pingamizi mahakamani wakipinga kupokelewa kwa nyaraka nne.

Leo Novemba 23, 2021 mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, pingamizi hilo liliwasilishwa na mawakili hao wakiongozwa na Wakili Mosses Mahuna baada ya shahidi wa 10 wa Jamhuri mfanyabiashara Francis Mrosso (44) kuomba nyaraka hizo zipokelewe kama vielelezo.

Shahidi huyo aliomba nyaraka nne ambazo ni leseni ya biashara, namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) na nyaraka mbili za usajili wa jina la kampuni yake ya Mrosso Injector Pump Service zipokelewe kama vielelezo.

Akiwasilisha hoja za pingamizi hilo Wakili Mahuna aliieleza mahakama kuwa wana sababu mbili za kisheria ambapo ya kwanza ni kuhusu nakala halisi ambazo ni TIN namba na leseni ya biashara na ya pili ni kuhusu nakala mbili za vyeti vya usajili wa jina la biashara ambazo siyo halisi hivyo kuomba mahakama isizipokee.

Wakili Mahuna alidai kuwa wanakataa kwa ujumla nyaraka zote nne kwani shahidi hajaweza kuelezea mnyororo wa makabidhiano ya nyaraka hizo kwani awali shahidi alieleza kuwa nyaraka hizo zilichukuliwa na Takukuru na hajaieleza mahakama zilirudije kwake.

Akijibu hoja hizo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ofmed Mtenga aliieleza mahakama kuwa nyaraka hizo za usajili wa kampuni ni nakala halisi na kuhusu hoja ya pili kuwa shahidi hajaeleza namna amepata nyaraka hizo, hoja hiyo haipaswi kuwasilishwa katika hatua hiyo ya upokelewaji.

Awali akiendelea kutoa ushahidi wake mahakamani hapo Mrosso alidai kuwa alikutana na Sabaya na vijana wake siku chache baada ya kuwapatia Sh90 milioni, ambapo Sabaya alimweleza walipanga kwenda kuchukua Sh10 milioni tena kwake.

Mrosso ambaye ni mfanyabiashara na mmiliki wa gereji ya Mrosso Injector Pump Service ameieleza mahakama kuwa akiwa katika sehemu ya kuoshea magari alikutana na Sabaya akiwa na vijana wake ambapo alidai kuwa Sabaya alimweleza kuwa walipanga kwenda kuchukua fedha nyingine ofisini kwake Sh 10 milioni.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27, 2021 watuhumiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Watuhumiwa hao wanadaiwa walimshinikiza Mrosso kuwapa kiasi hicho cha fedha ili wasitoe taarifa ya jinai dhidi yake ambapo kwa wakati huo walikuwa wakimtuhumu amefanya kosa la ukwepaji kodi.

Hakimu Mkazi Patticia Kisinda anayesikiliza kesi hiyo ameiahirisha hadi kesho Novemba 24, 2021 kwa ajili ya kutoa uamuzi mdogo kufuatia pingamizi hizo za mawakili wa utetezi.