Mawasiliano Ileje-Rungwe yarejea
Muktasari:
- Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Songwe, umefanikiwa kurejesha mawasiliano ya barabara inayounganisha Wilaya ya Ileje mkoani Songwe na Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.
Songwe. Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Songwe, umefanikiwa kurejesha mawasiliano ya barabara inayounganisha Wilaya ya Ileje mkoani Songwe na Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.
Mawasiliano kati ya wilaya hizo yalikatika kutokana na mvua zilizonyesha kwa muda mrefu.
Barabara hiyo ya Ibungu-Kafwafwa, ilikata mawasiliano katika Kata ya Luswisi wilayani Ileje, baada ya magema ya udogo kuangukia barabarani.
Akizungumza na mwananchi Digital leo Jumatano Aprili 4, 2024 Meneja wa Tanroads mkoani Songwe, Mhandisi Suleiman Bishanga amesema, wamelazimika kuweka kambi wilayani humo na kufanikiwa kurejesha mawasiliano hayo.
amesema barabara hiyo ni muhimu kwa kuwa inaunganisha mikoa ya Songwe na Mbeya, hivyo kulikuwa na kila sababu ya kurejesha mawasiliano haraka ili wananchi waendelee kusafiri.
''Asilimia kubwa ya sehemu muhimu iliyoharibiwa tumeitengeneza, bado sehemu ndogo pekee ambayo tunaendelea na ujenzi,''amesema Mhandisi Bishanga.
Aidha, amesema licha ya kurejesha mawasiliano hayo kwa wilaya ya Ileje, pia Tanroads inaendelea na jitihada za kuzitembelea barabara zingine katika wilaya za Mbozi, Momba na Songwe ili kuhakikisha zinapitika bila shida.
Mashaka Kibona na Sofia Mwala ambao ni watumiaji wa barabara hiyo wilayani Ileje, wameipongeza Tanroads kwa kufungua barabara hiyo, na kwamba waendelee kuwa karibu kipindi hiki cha mvua ili kutatua changamoto za kukatika kwa mawasiliano.