Mawasiliano na waliomteka Mtanzania Nigeria yanaendelea
Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dk Benson Bana amesema mawasiliano na watu waliomteka nyara Mtanzania, Melkiori Mahinini nchini humo bado yanaendelea kufanyika na kwamba kijana huyo yuko salama.
Dk Bana amebainisha hayo leo Agosti 16, 2023 wakati akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu kuhusu hatua waliyofikia katika kumnasua Mtanzania huyo kutoka mikononi mwa watekaji hao.
Melkiori (27) ni mseminari aliyepelekwa nchini Nigeria na Shirika la Wamisionari wa Afrika, ni mzaliwa wa Kigoma katika Parokia ya Kabanga.
Alikamatwa Agosti 3, 2023 katika jimbo la Minna huko Nigeria akiwa na mwenzake, Padre Paul Sanogo ambaye ni raia wa Burkina Faso.
Watekaji wanataka Naira 100 milioni (sawa na Sh325.1 milioni) kwa ajili ya kuwaachia huru wote wawili. Kwa mtu mmoja, watekaji wanahitajika Dola za Marekani 70,000 (zaidi ya Sh170 milioni).
Akizungumzia jitihada za kumwokoa kijana huyo, Dk Bana amesema jitihada bado zinaendelea na kwamba wanafanya mawasiliano ya siri na watekaji hao ili waweze kuwaachia huru watu hao waliotekwa.
“Kuna mawakili wawili ambao tunawatumia kuwasiliana na watekaji. Hili jambo ni very sensitive (nyeti), tunaenda nalo kwa tahadhari kubwa kwa maana tusipokwenda nao sawa wanaweza kuwadhulu hata kuwaua kabisa, imetokea mara kadhaa,” amesema.
Amesisitiza kwamba wanaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Nigeria pamoja na Kanisa Katoliki nchini na amewahakikishia Watanzania kwamba kijana huyo yuko salama.
“Hadi leo asubuhi nilipewa taarifa na kanisa kwamba wako salama ndiyo maana mazungumzo bado yanaendelea,” amesema Dk Bana katika mahojiano yake na Mwananchi.