Mbaroni akidaiwa kumwagia maji ya moto mke mwenza

Muktasari:
- Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Lugata, Kisiwa cha Kome, wilayani Sengerema, inamshikilia Vumilia Kasembo (32), akidaiwa kumwagia maji ya moto mke mwenzake Mariam Paul (30), walipokutana kwenye msiba wa baba mkwe wao.
Buchosa. Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Lugata, Kisiwa cha Kome, wilayani Sengerema, inamshikilia Vumilia Kasembo (32), akidaiwa kumwagia maji ya moto mke mwenzake Mariam Paul (30), walipokutana kwenye msiba wa baba mkwe wao.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi Agosti 26, Ofisa Mtendaji Kata ya Lugata, Rafael Jangol, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na baada ya kumhoji mtuhumiwa amekili kufanya kosa hilo huku akidai kuwa ni wivu wa kimapenzi baada ya kumwona mke mwenza.
"Tunamshiria kwa sasa huku tukiandaa taratibu za kumpeleka polisi kwa ajili ya taratibu zingine, Mariamu Paul ameumia sehemu mbalimbali za mwili wake huku mkono wa kushoto ukiwa umeungua zaidi, amesema Jangole.
Akielezea tukio kwa mwandishi wetu, Mariamu amesema yeye alitoka nyumbani kwake Kijiji cha Bukokwa na kuelekea Kijiji cha Lugata kwa ajili ya mziba baba mkwe wake, na kwamba baada ya maziko, kumalizika, saa 2:00 usiku alikwenda kulala, na hapo ndipo alipomwagiwa maji ya moto.
"Nilienda kulala kama saa mbili usiku, alikuja na kunimwagia maji ya moto kisha akakimbia. Sijui shida nini hadi animwagie maji ya moto, mimi niko kwangu na yeye yuko kwake tumekutana msibani kumuzika baba mkwe wetu kaniunguza na maji ya moto,” amesema Mariamu.
Kwa upande wake, Ndagabwene Evalist (33), ambaye ndiye mume wa wawili hao, meonyesha kusikitishwa na tukio hilo huku akisema limemtia aibu kwenye jamii iliyokusanyaka kwa ajili ya kumstili baba yake Costantine Sululu aliyefariki dunia na kuzikwa jana.
Amesema anashangwazwa na kitendo hicho kilicholeta fedheha kwa jamii, kwani alikuwa ameishamjulisha mke mkubwa (Vumilia), kuwa ana mke mwingine ambaye anaishi Kijiji cha Bukokwa lakini walikuwa hawajawahi kuonana.
"Nilikuwa nimechukuwa jukumu la kumwadhibu lakini jamii ilinizuia na kunisihi kuiachia Serikali ambayo itachukua hatua stahiki na siyo mimi kujichukulia sheria mkononi,” amesema Ndagabwene.
Kwa upande wa Vumilia ambaye anadaiwa kutenda kosa hilo amesema kichomtuma kufanya hivyo ni hasira baada ya kumwona mke mwenzie akiwa msibani hapo ambaye alikuwa hajawahi kukutana naye wala kitambulishwa rasmi na mume wake.
Shuhuda wa tukio hilo Yustina Evalist, ambaye ni dada wa Ndagabwene, amesema wakiwa wamelala walishitukia mtu akilalamika kuwa amemwagiwa maji ya moto, ndipo walipomwona Vumilia akitoka ndani kisha kukimbilia nje huku akiwa na sufuria mkononi.