Mbaroni kwa kumchoma mikono mtoto wake kisa kula wali bila ruhusa

Muktasari:
Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia Grace Godwin (23) Mkazi wa Mtaa wa Sido Kata ya Ibinzamata Manispaa ya Shinyanga kwa tuhuma za kumchoma moto mikono yote miwili mtoto wake kwa tuhuma za kula wali uliobakia bila ruhusa.
Shinyanga. Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia Grace Godwin (23) Mkazi wa Mtaa wa Sido Kata ya Ibinzamata Manispaa ya Shinyanga kwa tuhuma za kumchoma moto mikono yote miwili mtoto wake kwa tuhuma za kula wali uliobakia bila ruhusa.
Tukio hilo lilitokea Jana April 27, 2023 baada ya mama huyo kumchoma moto mtoto wake mwenye umri wa miaka saba anayesoma darasa la kwanza kwa madai ya kula wali bila kuruhusiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amesema tayari wanamshikilia mtuhumiwa huyo kwa hatua zaidi za kisheria na upelelezi utakapokamilika atafikishwa Mahakamani.
“Kweli tunamshikilia mtuhumiwa ambaye anaitwa Grace ni mama mzazi wa mtoto anayedaiwa kuchomwa moto mikono yake yote miwili, tukio hili ni baya na vitendo hivyo vya ukatili tunalaani vikali visijirudie”amesema Magomi
Mwenyekiti wa Mtaa wa Sido Kata ya Ibinzamata, Emmanuel Kayange amesema alipata taarifa za tukio hilo na kuamuwa kufuatilia na kubaini kweli mtoto kachomwa moto na mama yake mzazi kama inavyodaiwa.
Amesema kutokana na tukio hilo walimuita mama mzazi wa mtoto pamoja na bibi yake, Agnes Mgaya na kuwahoji ambapo walibaini mtoto huyo ana siku mbili amechomwa moto wakiendelea kumpa matibabu nyumbani.
Akielezea tukio hilo mtoto aliyechomwa moto amesema mama yake alimchoma kwa kutumia mfuko ambao aliuwasha na kumuwekea mikononi kwa sababu alikula wali uliokuwa umebaki.