Mbowe asema Chadema wataendelea kuhubiri haki, demokrasia
Mwehyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akitete jambo na mkewe, Dk Lilian Mbowewakati wa ibada ambayo imefanyika katika Usharika wa Nshara Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT). Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe amesema kilio chao ni nchi kusimama katika haki, upendo na kwamba hilo wataendelea kulizungumza wakati wote bila hofu.
Hai. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe amesema kilio chao ni nchi kusimama katika haki, upendo na kwamba hilo wataendelea kulizungumza wakati wote bila hofu.
Mbowe ameyasema hayo leo Jumapili machi 20, 2022 wakati wa ibada ya shukrani katika Usharika wa Nshara Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, ikiwa ni ibada yake ya kwanza katika usharika wake huo wa nyumbani tangu aachiwe huru na mahakama.
Amesema wao kama chama kikuu cha upinzani nchini, wamekuwa wakiwaombea viongozi wanaoongoza nchi wafanye kazi kwa uadilifu na haki ili kuleta ustawi katika nchi.
"Tunamshukuru Mungu ametutendea miujiza na mambo ya ajabu sana, kilio chetu siku zote ni kusimama katika haki kusimama katika upendo, hili naomba tulizungunze wakati wowote bila hofu".
Ameongeza kuwa "Hayajawahi kuwa matamanio au maombi yetu washindwe kutekeleza vizuri majukumu yao, tunawaombea wafanye kazi yao kwa uadilifu, wafanye kazi yao kwa haki, nchi yetu ipate ustawi, nchi yetu ikipata ustawi tutaona maisha bora kwa kila Mtanzania na hili ndilo jambo ambalo Chadema tunaliomba".
Mbowe amesema wakati anakutana na Rais baada ya kutoka gerezani, alimwambia nchini kuna watu mioyo yao inavuja damu, lakini pia alimwambia hofu inayojengwa na wasaidizi wa watawala kwamba Wanachadema wana vurugu, hawapendi amani ya nchi hii, ni maneno ya uongo
"Tulikubaliana wote kukutana katika neno haki, wanahubiri amani wakati wanajua uchaguzi haukuwa huru na haki, kuna watu wanateswa, wanafungwa watu kwa kimakosa, wakijua nchi ina ubaguzi, tutoke wote hapo kwenye maneno amani tuzungumze wote haki".
"Wachama wa chama chochote cha siasa waitangulize haki ya taifa, haki ya raia na haki ya wananchi kila haki ina wajibu wake, ni dhahiri tukikubaliana kukutana kwenye haki, wala hatutagombana, Rais na Serikali yako endesha serikali kwa misingi ya haki na sisi wa Chadema ambao ni chama kikuu cha upinzani, tutaendelea kuhubiri demokrasia na misingi yake yote hadi siku ambayo Mungu atatupa kibali na sisi cha kuiongoza Serikali".
"Ili taifa liweze kusimama kwenye haki, lazima taifa liunganishwe, lazima sheria za nchi zinazoongoza taifa ziwe zina maridhiano, pale watu wanapozungumza makundi yote na tukakubaliana kama Taifa ni nini haki ya watu wetu, nini haki za wafanyabiashara wetu, haki hata katika kuwapata viongozi wa kuliongiza Taifa, haki katika uchaguzi".
Mbowe amesema "Najiuliza neno katiba tunagombania wapi na kwa nini hawa wanasema wanataka katiba hawa wanasema tunataka shule, aliyesema ukitaka shule huhitaji katiba bora ni nani, embu tukae tutafute hizo tofauti zetu kwenye kutaka katiba ziko wapi, tukae tuzungumze"