Mbowe awataka Watanzania kuwa wajasiri
Muktasari:
- Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewataka kuwa wajasiri na hodari katika harakati za kujenga mustakabali bora kwa Tanzania.
Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakiadhimisha miaka 62 tangu kupata uhuru, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewataka kuwa wajasiri na hodari katika harakati za kujenga mustakabali bora kwa Tanzania.
Katika ujumbe wake huo aliouchapisha kupitia mitandao ya kijamii, Mbowe amesisitiza katika kipindi chote hicho Watanzania wamekabiliana na changamoto nyingi lakini walisimama kwa ujasiri na kujiamini walipofanya uamuzi kama Taifa.
“Tunaadhimisha miaka 62 ya Uhuru tukikumbuka pia umaskini wa watu wetu katikati ya wingi wa rasilimali, fursa zilizopotea na ahadi zilizovunjwa kutokana na sera na uongozi ambao haukutumia nguvu na ujasiri wa Watanzania,” amesema.
Amewataka Watanzania kujenga upya mioyo yao na kuahidi kuwa jasiri kupambana katika maendeleo na ustawi.
“Naomba tuwe hodari katika jitihada zetu za kujenga Tanzania inayojumuisha kila mmoja wetu bila ubaguzi, yenye haki kwa kila mmoja wetu, na yenye neema kwa wote.
“Tunaposonga mbele, naomba tukumbuke wale waliotangulia na na kujitoa kulipigania Taifa hili na kuenzi urithi waliotuachia kwa kuendelea kufanya kazi kuelekea mustakabali bora. Naomba tukatae ahadi zisizo na maana, hatua nusu nusu, uongo wa kisiasa na viongozi ambao hawawezi kutumikia matarajio yetu,”amesema.
Amerejea maneno ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela akisema, "nimejifunza kuwa ujasiri si kukosa hofu, bali ni ushindi dhidi yake. Mtu jasiri si yule asiye na hofu, bali ni yule anayeshinda hofu hiyo."
“Naomba tuwe jasiri na hodari katika harakati zetu za kujenga mustakabali bora kwa Tanzania. Heri ya Siku ya Uhuru kwa Watanzania wote!,”amesema.