Samia, Mbowe watuma salamu Mawlid al- Nabi
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wametuma salamu za kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (Mawlid al- Nabi) wakitaka iwe siku ya tafakari kwa Mungu.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa nyakati tofauti wametuma salamu za kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (Mawlid al- Nabi) wakitaka iwe siku ya tafakari mahusiano yetu na Mungu.
Baraza la Mawlid al- Nabi limefanyika kitaifa jijini Dodoma likihudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyemwakilisha Rais Samia.
Viongozi hao wametoa salamu hizo leo Alhamisi Septemba 28, 2023 kwa nyakati tofauti kupitia mtandao wa X, wakiwataka Watanzania kuwa watu bora kama alivyokuwa Mtume Mohammad (SAW).
Katika ujumbe wake, Rais Samia amesema, "Matokeo ya nia na juhudi katika mambo haya muhimu kwa kila mmoja wetu, yataendelea kutupa nchi yenye kupiga hatua kimaendeleo, nchi salama, yenye uadilifu, yenye amani, umoja na mshikamano," amesema Rais Samia kupitia mtandao wa X.
Siku ya Maulid ni maalumu ambayo waumini wa dini ya Kiisalmu duniani kote wanasheherekea kuzaliwa kwa kiongozi wao Mtume Muhammad (SAW).
Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema ni vema wakajifunza kutoka kwake jinsi ya kuwa watu bora na kuishi kwa amani na upendo.
"Katika Maulid ya mwaka huu, tunakumbuka mchango wa Mtume Muhammad (SAW) katika kueneza ujumbe wa amani, upendo, na haki. Tunajifunza kutoka kwake jinsi ya kuishi maisha yenye maana na kujali wengine.
"Tunapojumuika pamoja katika Maulid, tunashiriki sala, nyimbo, na hadithi za Mtume Muhammad (SAW). Nawatakia siku njema ya Maulid! Mungu awabariki nyote na awape furaha tele katika maisha yenu, tusheherekee kwa pamoja na upendo na umoja," amesema Mbowe.