Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msajili atoa kauli sakata la mamilioni ya ruzuku Chadema

Muktasari:

  • Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza amesema Chadema iliwasilisha barua ya kudai fedha hizo wiki hii, hivyo hakuna sababu ya chama hicho kusema juhudi za kuzifuatilia hazijazaa matunda, wasubiri utaratibu wa kuziomba kutoka Hazina unaendelea.



Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikidai kuzuiwa ruzuku yake ya Sh500 milioni, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imekitaka chama hicho kiache kulalamika, kisubiri taratibu.

Ofisi hiyo imefafanua kuwa mchakato wa kushughulikia fedha hizo unaendelea kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa, baada ya chama hicho kuwasilisha barua ya kuomba fedha hizo wiki hii.

Majibu hayo yametolewa siku moja baada ya Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, kuilalamikia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kuwa imezuia fedha hizo kwa muda mrefu kinyume cha sheria.

Mnyika aliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kuingilia kati suala hilo, akisisitiza kuwa fedha hizo ni halali kwa chama hicho na zinahusu kipindi cha Juni hadi Oktoba 2025 kutokana na uwakilishi wa Chadema waliokuwa nao bungeni.

Alisema kuzuiwa kwa fedha hizo kunazua wasiwasi, hasa ikizingatiwa kuwa mwaka wa fedha wa Serikali unakaribia kuhitimishwa Juni 30, 2026, hali ambayo inaweza kusababisha fedha hizo kurejeshwa Hazina.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya Chadema jijini Dar es Salaam, Mnyika alisema chama hicho kimekuwa kikifuatilia fedha hizo kwa muda mrefu kupitia barua mbalimbali na mikutano ya hadhara, lakini hadi sasa hazijaingizwa kwenye akaunti ya chama.

“Tunadai Sh500 milioni kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ambazo zimezuiliwa kati ya Juni hadi Oktoba 2025. Tunaamini fedha hizo zinashikiliwa kama sehemu ya njama za kuidhibiti Chadema na kuinyima haki yake ya kupata fedha zake halali,” alisema Mnyika.

Aliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo inasimamia masuala yanayohusiana na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kuchukua hatua ili kuhakikisha chama hicho kinapata haki yake, akidai jitihada zote za kufuatilia suala hilo hazijafanikiwa.

 “Tunafahamu kuna mchezo unaofanyika ili muda upite hadi Juni 30, 2026, mwaka wa fedha ufungwe na fedha zirudishwe Hazina, kisha tuelezwe kuwa haziwezi kutolewa tena,” alisema.

Mnyika pia alidai kuwa kuendelea kushikiliwa kwa fedha hizo ni kinyume cha sheria. Alisema awali Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilieleza kuwa kulikuwa na zuio la mahakama, lakini zuio hilo liliondolewa Aprili mwaka huu bila fedha hizo kuingizwa katika akaunti ya chama.

“Kabla ya hapo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa walikuwa wakidai hawamtambui Katibu Mkuu wa chama. Mahakama iliweka zuio dhidi ya uamuzi wa Msajili wa kutomtambua Katibu Mkuu, hivyo Sekretarieti ya chama inatambulika kisheria. Tunaamini huu ni mchezo wa hujuma kwa sababu fedha zetu bado hazijaingizwa kwenye akaunti ya chama,” alisema.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dk Jim Yonazi, alipoulizwa alijitenga na suala hilo akisema liko chini ya mamlaka ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Kama wanadai fedha hizo, wanapaswa kutambua kuwa ofisi inayohusika ni Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na si Ofisi ya Waziri Mkuu. Hatuwezi kuingilia suala hilo,” alisema Dk Yonazi.

Akizungumza leo Alhamisi, Juni 18, 2026, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, amesema Chadema iliwasilisha barua ya kudai fedha hizo wiki hii, hivyo hakuna sababu ya kusema juhudi zao hazijazaa matunda.

“Chadema waache kutoa lawama wakati suala lao linafanyiwa kazi. Fedha za ruzuku hazikai tu katika Ofisi ya Msajili; hutolewa na Hazina na kupelekwa kwa chama husika. Hivyo si sahihi kusema fedha hizo zipo ofisini tu, kwa kuwa ni lazima kwanza tuziombe kutoka Hazina,” amesema Nyahoza.

Nyahoza amesema mchakato wa kuomba fedha kutoka Hazina una taratibu zake, na kwamba barua ya Chadema inaendelea kufanyiwa kazi.

“Kimsingi wawe na subira. Barua yao inafanyiwa kazi. Waache kulalamika wakati wamewasilisha barua wiki hii tu,” amesema Nyahoza.