Mbowe , wenzake wafikishwa Mahakamani, kesi bado haijaanza

Muktasari:
- Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu tayari wamefikishwa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa ajili ya kuendelea na ushahidi katika kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya msingi.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu tayari wamefikishwa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa ajili ya kuendelea na ushahidi katika kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya msingi.
Ni baada shahidi wa kwanza katika kesi hiyo ndogo, ACP Ramadhani Kingai, kumaliza kutoa ushahidi wake jana, mahakamani hapo.
Mbowe na wenzake wamefikishwa mahakamani hapo, leo Ijumaa Septemba 17, 2021, saa 3:40 asubuhi na kupelekwa moja kwa moja katika mahabusu ndogo iliyopo mahakamani hapo.
Hata hivyo kesi hiyo ilipangwa kuanza saa 4:00 asubuhi, lakini mpaka sasa bado haijaanza usikilizwaji.
Leo shahidi wa pili wa upande wa mashtaka katika kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya msingi atatoa ushahidi wake ili kudhibitishwa kielelezo lilichopingwa na upande wa utetezi.
Chimbuko la kuwepo kwa kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya msingi kunatokana na mawakili wa upande wa utetezi kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Adamu Kasekwa, kutolewa Mahakama hapo na upande wa mashtaka, kama kielelezo katika kesi hiyo.
Mawakili hao wakiongozwa na Peter Kibatala, Septemba 15, 2021, walipinga maelezo hayo yasipokewe na Mahakama kwa sababu yalichukuliwa nje ya muda kisheria.
Mshtakiwa anapokamatwa anatakiwa kuchukuliwa maelezo yake ndani ya saa nne tangu anapokamatwa na sio vinginevyo.
Sababu nyingine, mshtakiwa Kasekwa kabla na wakati wa kuchukuliwa maelezo yake katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salam, anadaiwa kuteswa na askari Polisi jambo lililosimamiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Ramadhani Kingai, wakati huo akiwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha.
Kutokana na hali hiyo, Jaji Mustapha Siyani anayesikiliza shauri hilo, aliitisha usikilizwaji wa kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya msingi kwa ajili ya upande wa mashtaka kuleta mashahidi ili kudhibitishwa maelezo hayo.
Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa, wa tatu Mohamed Abdillahi Ling'wenya.