Mbozi wapiga marufuku tozo ya asilimia 10 mauziano viwanja

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Abdallah Nandonde.

Mbozi. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Abdallah Nandonde amepiga marufuku tozo ya asilimia 10 inayotozwa na wenyeviti wa vijiji na watendaji wakati wananchi wanapouziana viwanja au nyumba.

 Utarayibu huo hufanyika baada ya wawili wanapokubali kuuziana ili uongozi wa kijiji au kata kushuhudia mauziano hayo inabidi kutoa asilimia 10 ya fedha ambazo wamekubaliana.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo ya Mfumo wa Uhasibu na Utoaji Taarifa za Fedha kwa Ngazi ya Kituo cha Kutolea Huduma (FFARS) kwa watendaji na baadhi ya watumishi katika halmashauri hiyo, Nandonde amesema utaratibu huo ni batili hivyo viongozi hao wauache.

Mafunzo hayo ya FFARS yametolewa ili kusaidia mambo mbalimbali ikiwemo kudhibiti fedha zinazotolewa na wadau au Serikali ili zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa katika kutoa huduma bora kwa wananchi au jamii kwa ujumla.

Nandonde amesema asilimia hizo wanazotoza watendaji na wenyeviti hazipo kisheria huku akiwahoji watendaji na wenyeviti hao wanakozipe baada ya kulipwa.

"Niwapeni angalizo, unakuta watu wanauziana shamba au nyumba unachaji asilimia 10 unaipeleka wapi na unakatia risiti gani?" amehoji Mkurugenzi huyo na kuongeza.

"Wakati wananchi wanauziana shamba halafu wewe unataka asilimia 10 huoni kuwa unamuumiza mwananchi? Hiyo ni rushwa. Sasa kuanzia leo hicho kitu tuache. Tunaidhalilisha Serikali" amesisitiza Nandonde.

Akizungumza katika mafunzo hayo mkurugenzi huyo amesema mafunzo hayo yatasaidia kutambua mapato na matumizi kupitia mfumo kwa urahisi.

"Baada ya mafunzo haya washiriki wataweza kuandaa malipo yote kupitia mfumo"

Pia, mkurugenzi huyo amewaonya watumishi hao kuwa wasitumie steshenari kuandaa taarifa zao kutokana na unyeti wa taarifa zitakazokuwemo katika mfumo huo.

"Tusije kwenda kufanya kazi hizo katika steshenari, kila kitu kinachofanyika katika serikali ni siri, tukienda katika steshenari zile usiri unakuwa hakuna tena" amesema na kuongeza;

"Lakini pia tukitumia mfumo huu utatusaidia kutambua wadau waliochangia fedha katika miradi ya maendeleo tofauti na ilivyo sasa tunapokea fedha bila kufahamu ni mdau gani ameleta fedha hizo" amesema

Ameeleza kuwa mfumo huo utasaidia kujua mapato katika kila chanzo ikiwemo michango ya maendeleo ambayo ni lazima iingizwe benki.