Wanawake Songwe wapewa mbinu kufikia usawa wa kijinsia
Mbozi. Wanawake wametakiwa kujiimarisha kiuchumi na kuondoa hofu katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kufikia usawa wa kijinsia katika jamii.
Rai hiyo imetolewa leo Machi 8, 2023 na Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Mkoa wa Songwe, mama Tunu Pinda ambeye ni Mke wa Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda ambayo kimkoa yanafanyika katika viwanja vya CCM Vwawa wilayani Mbozi.
Amesema kuwa kama watajiimarisha kiuchumi watakuwa na ujasiri wa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika jamii hivyo kufikia lengo la 50/50 nchini Tanzania.
Mgeni huyo rasmi amesema vipo vikwazo ambavyo vimekuwa vikikwamisha wanawake kujikwamua kiuchumi ikiwamo mila, kutokuthubutu na kukata tamaa.
Amewataka wanawake kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na Serikali ili kuwawezesha kuinuka kiuchumi.
"Kina mama kopeni msiogope maadamu mnarudisha, kutumia fursa zinazopatikana katika maeneo yetu ili kuanzisha viwanda. Mjue mkiwa vizuri kiuchumi mnakuwa na shauku ya kujaribu fursa zingine zikiwemo za uongozi" amesema
Amesema Serikali ipo tayari kuwapa wanawake mikopo nchini kupitia asilimia 10 za mapato ya halmashauri hivyo wanawake watumie fursa hiyo.
"Tuungane pamoja na kufanya kazi kwa bidii na kufikiria nje ya boksi, kila fursa inayotokea mwanamke awe mbele ili afanikiwe. Msijiweke nyuma kabisa. Tamanini kujaribu kwa kuwa nanyi mna haki ya kujiendeleza" ameshauri mgeni huyo rasmi
Amesema kutokana na kutokuwepo usawa wa kijinsia, bado wanawake wanashindwa kujikwamua kutokana na kukandamizwa hivyo amewataka kuungana kupinga mila na tamaduni zinazowakandamiza katika jamii.
Amesema ni wakati wa wanawake kuungana na kupambana kupinga ukatili wa kijinsia.
"Tupambane kupinga ukatili wa kijinsia. Tuhakikishe vitendo vya udhalilishaji vinatokomea nchini" amesema
Amesema kuwa vikundi mbalimbali vikiwemo vikoba ni njia mojawapo ya kujipatia mitaji wanawake hivyo waungane katika vikundi ili kuinuana kiuchumi.
DC Mbozi awapa wanawake siri ya mafanikio
Katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi (DC), Esther Mahawe amewataka wanawake wa mkoa wa Songwe kutokata tamaa wakati wanapoanguka katika safari ya kujikwamua kiuchumi bali wapambane huku akiwashauri wanawake walioteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika nafasi mbalimbali kufanya kazi kwa bidii.
DC Mahawe amesema kuwa mkombozi wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe na hakuna sababu ya kukaa kusubiri kuwezesha wakati fursa zipo nyingi nchini.
Mkuu huyo wa wilaya ameeleza kuwa katika zama hizi mwanamke anatakiwa apambane na pale anapojaribu na kufeli asikate tamaa.
"Tukikaa tukisubiri kuwezeshwa tutachelewa, hizi ni kauli ambazo zimetucheleweshwa kwamba katika mafanikio ya mwanaume mwanamke yuko nyuma" amesema DC huyo na kuongeza;
Tumezubaishwa, sasa hivi ni pembeni ya kila baba aliyeendelea yuko mama na pembeni ya kila mama aliyeendelea kuna baba" amesema
Amesema sababu inayowachelewesha wanawake wengi ni kutokujiamini hivyo kutoa wito kwa wanawake wajiamini.
"Kutokujiamini na kutothubutu, mwanamke unaweza sana, ukianguka nyanyuka anza tena... kufeli ni sehemu ya kukupeleka kwenye mafanikio, feli sana na jaribu sana utafanikiwa" amesisitiza
Ametoa wito kwa wanawake ambao wamepata nafasi hasa za kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika ngazi mbalimbali kufanya kazi kwa bidii ili kudhihirisha kuwa wana uwezo.
"Niwaombe wanawake tulioaminiwa na Rais Samia tusijaribu kumuangusha, tunaweza sana tuamini kuwa tunaweza" ameshauri
"Ni neema Mungu kumchagua Rais Samia ili kuonyesha mfano kuwa wanawake tunaweza" amesisitiza
Aidha Mkuu huyo wa wilaya amewashauri wanawake waliopata nafasi hasa za uongozi kutowadharau waume zao.
"Nafasi ya mwanaume itabaki palepale, sio kuwa mwanamke umepata fursa ndio uwadharau wanaume hapana, hata kama una fedha kuliko yeye, Mungu akupe hekima. Sio una fedha zako nyumbani unataka uwe kiongozi" ameshauri DC huyo huku washiriki wakishangilia.