Mbunge alia kukatika katika kwa umeme mbele ya Rais Samia

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea na ziara za kikazi mikoa ya Mtwara na Lindi na leo, mbunge wa Nanyumbu (CCM), Yahya Mhata amefikisha kilio cha kukatika kwa umeme mbele ya mkuu huyo wa nchi zikiwemo pia za afya na elimu.

Dar es Salaam. Mbunge wa Nanyumbu (CCM), Yahya Mhata amemweleza Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu changamoto ya kukatika kwa umeme katika wilaya ya Nanyumbu pamoja na gharama kubwa ya kuunganisha umeme.

Mbunge huyo ameeleza hayo leo Jumapili Septemba 17, 2023 wakati wa ziara ya Rais Samia katika Wilaya ya Nanyumbu ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake katika mikoa ya Mtwara na Lindi.

“Changamoto iliyopo, umeme unakatika sana ndani ya wilaya yetu. Mazingira ya wilaya yetu ni ya kijijini lakini gharama ya kuweka umeme ni Sh350,000, hii bei ni kubwa sana, tunaomba na sisi tulipie Sh27,000 kama hapo kata ya jirani,” amesema.

Mbunge huyo ameeleza pia changamoto kwenye sekta ya afya ambapo amesema wilaya ya Nanyumbu ina vituo vya afya chakavu vya Nanyumbu na Michija kwa sababu vimejengwa tangu mwaka 1995.

“Tunaomba vituo hivi vifanyiwe ukarabati, hali ni mbaya. Pia, vituo vitano tulivyo navyo, havina gari la wagonjwa, tunaomba Ambulance kwa ajili yay a kuwasaidia mama zetu, tukipata hata Ambulance tatu zitasaidia kwani vituo vyetu viko mbali na hospitali ya wilaya,” amesema

Mhata ameeleza pia kuna changamoto ya utekelezaji wa ahadi za viongozi wetu, Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi aliwahi kutoa ahadi ya kujenga kituo cha afya katika kijiji cha Mikuva lakini mpaka leo ahadi ile haijatekelezwa.

Akieleza hatua ambazo Serikali imezichukua, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amekiri kuwepo kwa changamoyo hiyo na kueleza kwamba Serikali imetenga Sh200 bilioni kwa ajili ya mradi wa gridi imara ili kuhakikisha gridi ya Taifa inafika mkoa wa Mtwara. 

Amesema asilimia 40 ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi wa Gridi Imara zinakwenda mkoa wa Mtwara pekee, jambo ambalo linaonyesha umuhimu wa mkoa huo.

“Huu ni mradi wa miezi 18, nawahakikishia wana Nanyumbu, tunakwenda kufuta changamoto ya umeme hapa Nanyumbu na mkoa wa Mtwara kwa ujumla,” amesema Kapinga mbele ya wananchi wajiojitokeza kwenye ziara ya Rais Samia.

Amesema mpango wa muda mfupi ni maboresho ya laini ya msongo mdogo wa umeme kutoka Tunduru kwenda Masasi na kwamba wanategemea kufikia Desemba 2023, changamoto ya kukatika kwa umeme itapungua wilayani humo.
Kuhusu suala la gharama za kuunganishia umeme, Kapinga amesema wizara yake imeweka wataalamu kwa ajili ya kufanya tathmini ya hali halisi ya maeneo nchini ili kuainisha maeneo yanayostahili kuunganisha umeme kwa Sh27,000 na Sh350,000 kulingana na vigezi vilivyowekwa

“Kwa hiyo tunaainisha maeneo yote, nimeshawapa wataalamu maelekezo ya kuja na maeneo ambayo yanastahili kutozwa hiyo Sh35,000 ili wananchi hawa wasipate adha ya kutozwa isivyostahili,” amesema Naibu Waziri huyo.

Kuhusu changamoto kwenye sekta ya afya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali itapeleka gari la wagonjwa matatu katika wilaya hiyo ili zitoe huduma kwa wananchi.

Vilevile, amewagiza mkuu wa mkoa wa Mtwara kufuatilia ahadi iliyotolewa na Rais wa awamu ya pili mwaka 1988 kuhusu kujengwa kwa kituo cha afya katika kijiji hicho. Hata hivyo, amemwagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Nanyumbu kupeleka Sh50 milioni kwa ajili ya kukarabati zahati katika kijiji hicho.

“Nimemwagiza mkuu wa mkoa kutafuta taarifa ambazo Rais wa awamu ya pili alitoa ahadi kwa wananchi wa Mikuva kuhusu kupatiwa kituo cha afya,” amesema Mchengerwa wakati akijibu hoja ya mbunge wa Nanyumbu.