Mbunge CCM ahoji mgeni wake kuzuiwa getini kisa kuvaa Kimasai

Muktasari:

  • Mbunge wa Kiteto (CCM),  Edward Lekaita ameeleza kukerwa na kitendo cha mgeni wake kuzuiwa getini wakati akitaka kuingia bungeni kutokana kuvaa mavazi ya Kimasai.

Dodoma. Mbunge wa Kiteto (CCM),  Edward Lekaita ameeleza kukerwa na kitendo cha mgeni wake kuzuiwa getini wakati akitaka kuingia bungeni kutokana kuvaa mavazi ya Kimasai.

Akiomba mwongozo leo Alhamisi Aprili 8,  2021 bungeni mjini Dodoma,  Lekaita amesema kuna mtu huyo ambaye ni mpigakura wake leo alifika bungeni kwa ajili ya kumtembelea  lakini akazuiwa getini  kwa sababu amevaa mavazi ya kabila la Kimasai maarufu nchini Tanzania kwa ufugaji.

“Naomba nipate mwongozo wako kuhusu mavazi haya rasmi kabisa ili na Watanzania wengine walioko huko  wanaovaa mavazi yao ya asili wafahamu kuhusu mavazi ya Bunge lao. Nilinyanyasika kwa kweli,” amesema.

Amesema kama baba yake mzazi mwenye umri wa miaka 80 angekwenda bungeni akiwa amevaa mavazi hayo na akaelezwa kuwa hawezi kumuona kwa sababu amevaa Kimasai, ingekuwa mbaya zaidi huku akitaka kupewa mwongozo kuhusu mavazi.

Akijibu mwongozo huo, Spika Job Ndugai amesema wamejiwekea kanuni za kuendesha mambo na hata yeye mwenyewe akivaa mavazi hayo hataruhusiwa kuingia bungeni.

“Lengo si kubaguana ni utaratibu tuliojiwekea kuvaa mavazi ya heshima na kanuni imeorodhesha. Hii ni changamoto kuangalia tena kanuni zetu kuona inakuaje katika mazingira hayo mavazi hayo,” amesema.

Alitumia nafasi hiyo kuomba radhi kwa kilichotokea na kwamba ni muhimu kwa watu wanaokwenda bungeni kwenda na mavazi yaliyokamilika.