Mchakato Nyerere kuwa Mtakatifu kuanza na Kardinali Pengo

Hayati Mwalimu Julius Nyerere

Dar es Salaam. Wakati mahakama maalumu ya mchakato wa kumtangaza aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Julius Nyerere kuwa mtakatifu ikizinduliwa rasmi, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo anatarajiwa kuwa wa kwanza kuhojiwa na mahakama hiyo Januari mwakani.

Mahakama hiyo iliyoundwa na Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, inapokea kijiti kutoka Jimbo Katoliki la Musoma ili kuendeleza mchakato ambao ulihamishiwa kutoka huko tangu mwaka 2013.

Uzinduzi wa mahakama hiyo ulishuhudiwa na watu mbalimbali, akiwemo mke wa hayati Mwalimu Nyerere, Maria Nyerere.

Akizungumzia suala hilo, Askofu na kiongozi wa mahakama hiyo maalumu, Henry Mchamungu alisema mchakato umehamishiwa Jimbo Kuu la Dar es Salaam kutokana na kile kilichoelezwa kuwa maisha ya Mwalimu Nyerere kwa muda mrefu aliyaishi katika jimbo hilo.

"Mchakato huu ulianzia Jimbo la Musoma ambako Mwalimu Nyerere alizaliwa na ulianza rasmi mwaka 2005 na baadaye ilionekana kuwa Dar es Salaam aliishi zaidi, hivyo walifikia uamuzi wa kuuhamishia huku, sehemu ambayo ina mashahidi wengi kumhusu," alisema Mchamungu.

Alisema Kanisa Katoliki lina utaratibu wa kumtangaza mtu kuwa mtakatifu. Hayati Mwalimu Nyerere alikuwa Mkatoliki na baada ya kifo chake mwaka 1999 ilionekana kuwa aliishi maisha mazuri mbele za watu, hivyo kusukuma kufanyika mchakato huu.

Alisema baada ya Musoma kufanya kipande chao, Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, aliliomba Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kuuendeleza na TEC ikaliomba Jimbo Kuu la Dar es Salaam kuendelea nao.

Alisema mpaka mchakato huo unahamishiwa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ulikuwa umefikia hatua Hayati Nyerere kutambuliwa kama mtumishi wa Mungu kabla ya kutangazwa kuwa mwenyeheri, hatua ambayo ni ya mwisho kabla ya kutangazwa mtakatifu.

Alisema kamati hiyo imetangazwa sasa kwa sababu mchakato ulipohamishwa lazima mambo yatendeke kwa mfumo rasmi ambao unakwenda sambamba na kutangazwa maofisa watakaofanya kazi katika mahakama ambayo itakuwa ikiwahoji mashahidi waliomjua Mwalimu Nyerere.

Maofisa hao walitangazwa rasmi na kula kiapo cha uadilifu Jumanne wiki hii (Novemba 14) na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa'ichi, ambapo naye pia alikula kiapo kama mkuu wa jimbo aliyeiteua mahakama hiyo.

"Hiki ni kitu kilichofanyika rasmi, baada ya kiapo mahakama itaanza rasmi kuhoji mashahidi wanaojua maisha ya Nyerere. Shahidi wa kwanza ni Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo atakayehojiwa Januari, mwakani," alisema Mchamungu.

Alisema baada ya kukamilika kumhoji, maofisa wa mahakama hiyo watapanga ratiba kuendana na mashahidi watakaopatikana ili kuwahoji kimahakama, watoe maelezo yao yatakayokusanywa na kuwasilishwa makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani, Vatican.

"Sisi kazi yetu ni kuhoji na kazi ya Roma baadaye ni kupitia yote hayo na wataona cha kufanya ili kufikia hatua ya pili ya Nyerere kutangazwa Mwenyeheri, waumini jitokezeni kushiriki suala hili, kwani litahitaji mambo mengi, zikiwamo fedha. "Fedha itahitajika kwa sababu mahakama kuna wakati itatakiwa kusafiri kwenda sehemu tofauti au watu wanaotakiwa kusafiri kuja kutoa ushahidi," alisema Mchamungu.

Kwa upande wa Ruwa'ichi aliitaka mahakama hiyo kutenda kazi kwa kusimamia kiapo chao ili kufanikisha kile walichoaminiwa.

Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga alisema katika kipindi cha uhai wa Hayati Julius Nyerere aliishi maisha ya imani, matumani huku akijitolea kupigania haki na mageuzi ndani ya jamii na akiwa miongoni mwa wale waliopigania uhuru wa nchi nyingi za Afrika.

“Pia alikuwa kiongozi aliyekataa kuishi sehemu yenye hadhi kubwa, badala yake alichagua nyumba ndogo ambayo watu wanaweza kumfikia kwa ajili ya ushauri na msaada,” alitoa ushuhuda wake.


Historia kwa ufupi

Nyerere akiwa Rais mara zote alipigana na maadui watatu ambao ni umasikini, ujinga na maradhi. Alizaliwa Aprili 13, 1922 katika kijiji cha Butiama karibu na Pwani ya Ziwa Victoria, na kwa mujibu wa historia, wakati wa utoto wake alikuwa akiwasaidia wazazi wake shambani ikiwa ni pamoja na kuchunga mifugo.

Mwalimu Nyerere alikuwa mtoto wa pili kati ya wanane waliozaliwa na Christina Mugaya ambaye alikuwa kati ya wake 22 wa Mtemi Nyerere Burito (1860-1947) wa kabila la Wazanaki.

Historia inasema katikati ya Aprili 1934 Nyerere alilazimika kutembea zaidi ya maili 25 kutoka Butiama kwenda Musoma kwa ajili ya kujiunga na Shule ya Msingi Mwisenge, iliyoko Musoma aliyoianza rasmi Aprili 20, 1934 na alihitimu mwaka 1936.

Baada ya kumaliza shule ya msingi aliendelea kusoma shule ya Wamisionari Wakatoliki mkoani Tabora.

Alipofikisha miaka 20, alibatizwa akawa Mkatoliki hadi mwisho wa maisha yake.

Mapadri walibaini kipaji alichonacho hivyo walimsaidia kusomea ualimu katika Chuo Kikuu cha Makerere, Kampala, Uganda kuanzia 1943 hadi 1945.

Akiwa Makerere alianzisha Tawi la Umoja wa Wanafunzi Watanganyika na pia akajihusisha na Tawi la Tanganyika African Association (TAA). Baada ya kumaliza masomo ya ualimu alirudi Tabora akawa Mwalimu katika Shule ya Sekondari ya St. Mary´s.

Mwaka 1949 alipata nafasi ya kwenda kusoma kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh, Uingereza akisomea Shahada ya Uzamili ya Historia na Uchumi na alihitimu mwaka 1952.

Aliporejea Tanganyika kutoka masomoni, Nyerere alifundisha historia, Kiingereza na Kiswahili katika Shule ya Sekondari ya St. Francis (Dar es Salaam) ambayo kwa sasa inajulikana kama Shule ya Sekondari Pugu.

Mwaka 1953 alichaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Tanganyika African Association (TAA), Chama ambacho alisaidia kukijenga alipokuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Makerere.

Mwaka 1954 alikibadilisha Chama cha TAA kuwa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) ambacho kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko ilivyokuwa TAA.

Katika kipindi cha mwaka mmoja, Chama cha TANU tayari kilikuwa chama cha siasa kinachoongoza Tanganyika, huku uwezo wa Mwalimu Nyerere ukiwashtua viongozi wa kikoloni na kumlazimisha achague kufanya kazi ya siasa au abaki na ya ualimu, hapo ndipo Nyerere alisikika akisema kuwa alikuwa mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati mbaya.

Alijiuzulu ualimu na kuzunguka nchini Tanganyika kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta muungano katika kupigania uhuru.

Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Baraza la Udhamini na Kamati ya Nne ya Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani, uwezo wake wa kuunganisha watu ili wawe na umoja na mshikamano kutetea haki zao pamoja na kipaji chake cha kujenga hoja, kutetea na kuzungumza kwa ufasaha ulimwezesha kufanikisha Tanganyika kupata uhuru bila umwagaji wa damu.

Ushirikiano mzuri aliouonyesha kwa aliyekuwa Gavana wa wakati huo, Richard Turnbull ulisaidia pia kuharakisha upatikanaji wa uhuru.

Kuanzia Ijumaa ya Septemba 2, 1960, Nyerere alianza kuhudumu kama Waziri Kiongozi na ndani ya siku 241 alipanda tena cheo na kuwa waziri mkuu kuanzia Jumatatu ya Mei, 1961.

Alipokuwa waziri mkuu, Nyerere aliteua Baraza lake la mawaziri ambapo alimteua Rashid Mfaume Kawawa kuwa Waziri asiye na wizara maalumu kabla hajawa waziri wa Serikali za mitaa, Abdallah Fundikira aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi Upimaji Ramani na Maji.

Sir Ernest Vasey Waziri wa Fedha, Amir Habib Jamal, Waziri wa Viwanda, Tewa Said Tewa aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi na Upimaji, Paul Lazaro Bomani (Waziri wa Ukulima na maendeleo ya ushirika), Oscar Salathiel Kambona kuwa Waziri wa Elimu, Derek Noel Maclean Bryceson (Waziri wa Afya na masuala ya wafanyabiashara).

Clement George Kahama kama waziri wa Usalama na amani ya Nchi (waziri wa mambo ya ndani), Job Malecela Lusinde, waziri wa Serikali za mitaa.

Jumatatu ya Januari 22, 1962 Nyerere alijiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu ikiwa ni miezi michache baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo na baadaye Rais.

Baada ya kuhudumu kama Rais kwa miaka 24 hatimaye Oktoba 14, 1984 aling’atuka madarakani ikiwa ni baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 27 na mgombea pekee wa urais, Ali Hassan Mwinyi aliibuka mshindi.